1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkurugenzi Mtendaji IEBC achukua likizo

20 Oktoba 2017

Afisa mkuu mtendaji wa Tume yaUuchaguzi IEBC, Ezra Chiloba, amesema anachukua likizo ya wiki tatu wakati uchaguzi mpya wa rais ukitarajiwa kufanyika Oktoba 26. Upinzani ulitaka Chiloba ajiuzulu.

https://p.dw.com/p/2mEM0
Mkurugenzi wa IEBC, Ezra Chiloba
Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Kenya inasherehekea Sikukuu ya Mashujaa kuwakumbuka vigogo walioshirikiana kuikomboa nchi hiyo kutokana na ukoloni. Kwa mara ya kwanza siku hii inakumbukwa kukiwa na sintofahamu za kisiasa kuhusu uchaguzi mpya wa rais. Sherehe hizi zinafanyika katika mazingira magumu ya kisiasa Kenya inajiandaa kwa uchaguzi mpya wa rais uliopangiwa Alhamisi ijayo. Pindi baada ya kuwasili kwenye bustani ya Uhuru, Rais Uhuru Kenyatta alikaribishwa kwa gwaride la heshima aliloandaliwa na vikosi vya wanajeshi.

Kumbukumbu hizi  zinafanyika wakati ambapo uchaguzi mpya wa rais unasubiriwa kufanyika tarehe 26 Oktoba. Sherehe zilianza kwa ibada kutoka madhehebu mbalimbali kabla ya hotuba rasmi kutolewa. Tume ya Uchaguzi IEBC imekuwa ikiendelea na maandalizi ya uchaguzi ila katika mazingira ya changamoto nyingi kwani maafisa wao wamekuwa wakivamiwa katika baadhi ya maeneo yanayoaminika kuwa ngome za upinzani. Kwa sasa makaratasi ya kupigia kura yanasubiriwa kuwasili hapo kesho kutokea Dubai yalikokuwa yanachapishwa. Duru zinaeleza kuwa majina ya wagombea wote 8 wa urais yamo kwenye makaratasi hayo.

Yote hayo yakiendelea afisa mkuu mtendaji wa tume ya IEBC Ezra Chiloba amechukuwa likizo ya  wiki tatu zijazo kwa alichokitaja kuwa sababu za binafsi. Haya yanajiri siku chache baada ya Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi iebc Wafula Chebukati kusisitiza kuwa maafisa waliotajwa vibaya kwenye uchaguzi mkuu uliopita wa Agosti 8 wasogee pembeni. Kwa sasa Kenya inajiandaa kwa siku ya ibada ya kitaifa ya Jumapili iliyotangazwa na Uhuru Kenyatta madhumuni yakiwa kuiweka nchi katika hali salama.

Kwa upande mwengine viongozi wa kisiasa wa upinzani wa NASA wanajumuika kwenye uwanja wa Ogango eneo la kaunti ya Kisumu ili kuwakumbuka waliopoteza maisha yao mikononi mwa polisi wakati wa maandamano ya kupinga tume ya iebc ya siku chache zilizopita. Viongozi hao wa NASA walihudhuria maziko eneo la Bondo la kaunti ya Siaya ya waliouawa wakati wa maandamano hayo. Wito unaendelea kutolewa kwa Viongozi wa Jubilee na NASA kuwataka kuepusha shari wakati uchaguzi mpya wa rais unasubiriwa wiki ijayo. Mwangi Guchu ni mwenyekiti wa kamati ya muungano wa vyama vya kisiasa na anasisitiza kuwa la muhimu ni amani nchini Kenya.

Mwandishi: Thelma Mwadzaya

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman