1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkurugenzi wa shirika la Care atimuliwa Sudan

Jane nyingi27 Agosti 2007

Mkurugenzi wa shirika la kimataifa la kutoa msaada la Care nchini Sudan Paul Barker amefukuzwa nchini humo. Barker hakupewa sababu hasa ya kufukuzwa kwake bali aliarifiwa kuwa hayo yaliafikiwa na maafisa wakuu wa serikali ya Sudan.

https://p.dw.com/p/CB1h
sudan
sudan

Barker ni afisa mkuu wa tatu wa kigeni kufukuzwa nchini sudan chini ya wiki moja.Siku ya alhamisi balozi wa Canada na umoja wa ulaya waliamuriwa kuondoka nchini humo lakini kisha baadaye serikali ya sudan ikabadili uamuzi wake na kumruhusu balozi wa jumuiya ya ulaya kuendelea na kibarua chake hadi kumalizika kwa kipindi chake mwezi ujao.

Barker alisema mkurugenzi wa halmashauri ya misaada ya kiutu alimpigia simu na kumweleza kuwa alikuwa na barua kutoka kwa maafisa wakuu wa sudan inayosema hawatarefusha kibali chake cha kufanya kazi na pia amepewa hadi muda wa saa 72 kuondoka nchini Sudan.

Barker anasema pengine uamuzi huo ni kutokana na serikali kutofurahishwa na barua pepe aliyowaandikia wafanyikazi wa shirika la Care mwezi October ambayo kisha iliingia kisiri mikononi mwa wanahabari nchini humo mapema mwaka huu. Serikali ilihisi kuwa barua hiyo ilichambua hali ya kisiasa nchini humo jambo lisiloruhusiwa kwa mashirika yasiyoyakiserikali.

Wafanyikazi kutoka mashirika ya kutoa misaada nchini sudan ambao waliyabana majina yao wanasema hatua hiyo inawadia wakati ambapo kuna mvutano kati ya maafisa wa mashirika hayo na serikali ya Sudan

Waziri wa maswala ya nje nchini sudan katika mahojiano na kituo cha utangazaji kinachomilikiwa na serikali alisema mabalozi wa canada na umoja wa ulaya wanafukuzwa kwa kuyaingia maswala ya ndani ya sudan.

Shirika la kimataifa la kutoa misaada la Care lilo na makao yake nchini marekani limetumia dolla milioni 184 katika miradi mbalimbali nchini Sudan tangu lilowasili nchini humo mwaka 1979.Katika muda wa miaka mitatu limetumia dolla millioni 60 hasa katika jimbo linalokabiliwa na mgogoro la darfur.

Taarifa nyingine ni kuwa mahakama ya jinai nchini sudan imefutilia mbali kesi dhidi ya watu tisa kuhusiana na kukatwa kichwa kwa mwandishi habari maarufu nchini humo. Watu kumi na tisa wakiwemo wanawake wawili walikuwa wameshtakiwa kwa mauji ya kikatili ya Mohammed Taha mhariri wa gazeti la kiarabu la al-wifaq.

Maiti ya Taha ilipatikana barabarani katika mji mkuu September mwaka jana, mikono na miguu ikiwa imefugwa na kichwa chake kando ya maiti . Taha alisababisha maandamano makubwa kutoka kwa makundi ya kiislamu mwaka 2005 kutokana na misusuru ya makala yake iliyotilia shaka asili ya mtume mohammed.