1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano bila ya matokeo

Nina Werkhäuser / Maja Dreyer22 Februari 2007

Hakuna matokeo thabiti ya mkutano wa pande nne zinazoshughulikia mzozo wa Mashariki ya Kati uliomalizika jana usiku mjini Berlin, nchini Ujerumani. Pande zote lakini zimekubali kuwaunga mkono Wapalestina katika kuunda serikali mpya. Ili kuweka ishara, mkutano ujao wa washirika hawa utafanyika katika nchi ya Kiarabu kwenye eneo la mzozo huo.

https://p.dw.com/p/CHJY
Condoleezza Rice na Frank-Walter Steinmeier
Condoleezza Rice na Frank-Walter SteinmeierPicha: AP

Waliopanda jukwaani walikuwa wanasiasa maarufu sana, lakini hata hivyo, mkutano huo ulikuwa mfupi sana. Wajumbe kutoka pande nne wakiwemo mawaziri wa nchi za nje wa Marekani, Urusi na Ujerumani, walishindwa kutoa habari nzuri za kuendelea na utaratibu wa amani. Ban Ki Moon, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, alisoma taarifa ya pamoja, ambayo ilizungumzia hasa matarajio na miito.

Pande zote zilisifu mazungumzo ya hivi karibuni kati ya waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, na rais wa Palestina, Mahmoud Abbas. Hata ikiwa matokeo hamna, bado ni dalili nzuri kuwa pande zote mbili ziko tayari kwa mazungumzo, alisema waziri wa nchi za nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier: “Tunajua kuwa utaratibu huo wa kukaribiana ni mgumu, na ndio sababu tunataka kuuunga mkono ili kutafuta njia nzuri ya kufika pahali ambapo zamani hatukuweza kufika.”

Mwakilishi wa siasa ya nje ya Umoja wa Ulaya, Javier Solana, alisema, maendeleo yatategemea hasa ikiwa serikali mpya ya Palestina itachukua msimamo wa kishirikiana katika kutafuta amani. Alisema: “Natumai kuwa serikali hii itachangia katika kusuluhisha matatizo na siyo chanzo cha matatizo haya.”

Chama cha msimamo mkali wa Kiislamu cha Hamas kitakachokuwa na usemi mkubwa katika serikali mpya, bado hakijatambua haki ya kuwepo taifa la Israel. Hilo lakini ni jambo moja ambalo pande nne zilizokutana Berlin zinalidai kwa nguvu pamoja na kutambuliwa mikataba ya amani ambayo tayari ipo na vile vile kuacha mapigano. Waziri Condoleezza Rice wa Marekani: “Haiwezekani kufanya mazungumzo ya amani kama upande mmoja hauutambui upande mwingine.”

Hadi sasa ni chama cha Fatah tu cha rais Abbas ambacho kinakubali madai ya pande nne. Abbas lakini anawakilisha sehemu ndogo tu ya Wapalestina, kwa hivyo mazungumzo yoyote na Abbas peke yake hayataleta suluhisho. Ikiwa Hamas kitabadilisha msimamo wake, hali hiyo itaonekana tu baada ya serikali kuundwa.

Juhudi hizo mpya za pande nne, yaani Umoja wa Mataifa, Marekani, Urusi na Umoja wa Ulaya, za kusaka amani ya Mashariki ya Kati, hazijasaidia pakubwa kuleta maendeleo katika eneo hilo. Licha ya hayo lakini wajumbe wa baraza hilo la mapatanisho wanataka kukutana tena haraka. Mkutano huo ujao umepangwa kufanyika katika nchi ya Kiarabu ili kuhamasisha uungaji mkono zaidi.