1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano juu ya kuleta amani mashariki ya kati wafanyika Washington

2 Februari 2007

Wawakilishi wa Umoja wa Mataifa,Marekani,Urusi na Umoja wa Ulaya leo wanakutaka mjini Washington katika juhudi za kuufufua mchakato wa kuleta amani katika mashariki ya kati.

https://p.dw.com/p/CBHT
Mkutano juu ya Mashariki ya Kati
Mkutano juu ya Mashariki ya KatiPicha: AP

Lengo la mkutano wa leo mjini Wshington ni kuutia msukumo mpya mchakato wa kuleta amani baada ya kuzorota kwa muda wa miezi kadhaa.

Mkutano wa mjini Washington unafuatia mazungumzo yaliyofanywa hivi karibuni baina ya Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na waziri wa mambo ya nje wa Marekani bibi Condoleeza Rice.

Hatua ya kuitisha mkutano huo pia inatokana na kuzidi kushtadi kwa hali mbaya baina ya waisraeli na wapalestina.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa mataifa makubwa pamoja na Umoja wa Mataifa yana deni kubwa la kidiplomasia katika mashariki ya kati hasa kwa kuzingatia kwamba nchi hizo zimekuwa zinazungumzia juu ya kuleta usalama na demokrasia katika eneo zima la mashariki ya kati.

Suala la mashariki ya kati limeibikwa kwa muda mrefu na vita vya nchini Irak. ambapo Marekani imeelekeza kiasi kikubwa cha muda na raslimali zake kama anavosema mwandishi wetu Peter Philiip.

Mazungumzo ya kuleta amani katika mashariki ya kati yamekuwa yanafanyika kwa dahari za miaka sasa na hakika hatua kadhaa muhimu zimechukuliwa japo kwa muda mfupi kwani mapendekezo,mikataba na makubaliano takriban yote yaliyofikiwa yamekuwa yanakiukwa na pande mbili muhimu zinazohusika na mgogoro, yaani Waisraeli na Wapalestina. Ni jambo gani linaloweza kuamuliwa kwenye mkutano huo wa mjini Washington?

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani bwana FrankWalter Steinmeir anahudhuria mkutano huo wa mjini Washington amesema anafurahi kwamba angalau

mkutano huo unafanyika kwa kutambua kwamba hadi kiasi cha muda wa nusu mwaka tu uliopita , hakuna aliefikiri kwamba lingekuwa jambo rahisi kuandaa mkutano huo. Kwa upande wake Ujerumani ilijaribu kuchukua hatua kadhaa za kidiplomasia ili mkutano kama huu uweze kufanyika.

Tokea kumalizika vita nchini Lebanon, mwaka jana, waziri Steinmeier amekuwa anafanya bidii kwa lengo la kufufua jitihada za jumuiya ya kimataifa katika kuanzisha tena mchakato wa kuleta amani katika mashariki ya kati.

Juhudi hizo zinaungwa mkono na Kansela wa Ujerumani bibi Angela Merkel pamoja na rais G. Bush wa Marekani japo nchi yake kwa sasa imetingwa na vita vya nchini Irak.

Hatahivyo yafaa kutilia maanani kwamba mkutano huo wa mjini Washington unafanyika wakati ambapo vyama vya Hamas na Fatah vinamalizana na wakati ambapo mshambuliaji wa kujitoa mhanga aliwaripua waisraeli katika kitongoji cha Eilat nchini Israel.

Na Abdu Mtullya