1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano juu ya usalama wa nyuklia.

Halima Nyanza13 Aprili 2010

Rais Barack Obama wa Marekani jana amefungua mkutano mkubwa, kwa kuwakaribisha viongozi na maafisa wa ngazi za juu kutoka nchi zaidi ya 40 kujadili mpango wa kuzuia malighafi hatari za nyuklia kuangukia kwa watu wabaya.

https://p.dw.com/p/MuyK
Rais Barack Obama wa Marekani, mwenyeji wa mkutano mkubwa wa usalama wa nyuklia unaofanyika mjini Washington.Picha: AP
Rais Barack Obama wa Marekani jana aliufungua  mkutano  huo kwa kuwaandalia chakula cha jioni wageni wake hao kabla ya kuanza kikao kamili cha mazungumzo leo. Rais Obama atawataka viongozi hao kusaini mpango wake wa kuimarisha usalama katika  ulinzi  wa  malighafi za kinyukilia, ambazo haziko katika hali ya usalama, katika kipindi cha miaka minne ili zisiweze kuangukia katika mikono ya watu wabaya. Viongozi na maafisa waandamizi kutoka mataifa 47 duniani wanashiriki katika mkutano huo mkubwa ulioitishwa na Rais Obama ambao ni mkubwa kuitishwa tangu mwaka 1945, ambapo viongozi walikutanika mjini San Francisco kwa ajili ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa. Ukraine nayo yaunga mkono: Saa kadhaa kabla ya kuanza kwa mkutano huo, Ukraine ilitangaza kwamba inadhamiria kuondoa madini ya nyuklia yaliyorutubishwa kwa hali ya juu ambayo yanaweza kutengeneza mabomu ya nyuklia ifikapo mwaka 2012. Akitangaza matokeo ya mkutano wa pande mbili kati ya Rais Victor Yanukovych wa Ukraine Barack Obama, uliotoa taarifa hizo, Msemaji wa Ikulu ya Marekani Robert Gibbs, alisema Ukraine imetangaza uamuzi muhimu kuondoa hifadhi yake yote ya uranium iliyorutubishwa kwa kiwango cha juu hadi wakati wa mkutano ujao wa nyuklia mwaka 2010.
Nuklear Konferenz Obama und Viktor Yanukovich
Rais Barack Obama (kushoto) na Rais wa Ukraine(kulia) mjini Washington.Picha: picture alliance / dpa
Amesema hatua hiyo ni kitu ambacho Marekani imekuwa ikijaribu kukifanya kitokee kwa zaidi ya miaka 10. na kuongeza kuwa malighafi hiyo inatosha kutengenezea silaha kadhaa za nyuklia. Mkutano huo wa leo utaelezea pia usalama wa wa silaha za nyuklia pamoja na hatari ya mafuta  ambayo yanatumika kwa nishati ya matumizi ya kiraia, ambayo inaweza kutumika katika silaha na pia mkutano huo unalenga kuzuia biashara ya magendo ya teknolojia ya nyuklia na ujuzi wake. Wasiwasi mkubwa ni kwa  makundi ya kigaidi kama vile AlQaeda kuweza kupata malighafi kama hizo na kutumia kufanyia mashambulizi. Hata hivyo baadhi ya mataifa yamekuwa na shaka kuhusiana na uzito wa vitisho hivyo na kuangalia kama ni jinsi Marekani inavyotaka kulishughulikia jambo hilo baada ya kukumbwa na mashambulio ya kigaidi Septemba 11, 2001. Lakini mshauri wa ngazi ya juu wa Rais Obama, katika masuala ya ugaidi John Brennan ameonya kwamba  Al Qaeda imekuwa ikijaribu kupata  malighafi hizo katika masoko ya wazi na katika biashara za kihalifu. Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ambaye amethibitisha kuunga mkono, malengo ya Rais Obama juu ya usalama wa nyuklia ameelezea kutokuwepo kwa mfumo wa sheria wa kuzuia dola kutoweza kuzipajumuia za kigaidi malighafi za kutengeneza silaha za nyuklia.
Nuklear Konferenz Obama und Angela Merkel
Rais Barack Obama akisalimiana na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.Picha: AP
Na katika hatua nyingine, leo, Marekani na Urusi zitasaini pia mkataba juu ya kuweka sawa hifadhi yake ya madini ya sumu kali yanayotumika katika silaha za nyuklia. Hata hivyo mkutano huo wa siku mbili mjini Washngton umegubikwa na kuongezeka kwa wasiwasi juu ya Iran, ambayo Marekani na washirika wake wanailaumu kwa kutengeneza kwa siri silaha za nyuklia. Iran yenyewe imekuwa ikikana tuhuma hizo dhidi yake na kusema kwamba inafanya hivyo kwa matumizi ya kiraia tu. Katika hatua nyingine Rais Barack Obama na Rais Hu Jintao wamekubaliana kwamba ujumbe wao utafanya kazi pamoja katika Umoja wa Mataifa  juu ya juhudi zinazoongozwa na Marekani kuiwekea vikwazo Iran. Mwandishi: Halima Nyanza(dpa,reuters) Mhariri:  Sekione  Kitojo.