1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano kati ya Afrika na Ufaransa wamalizika leo Nice

1 Juni 2010

Mkutano wa kilele kati ya viongozi wa mataifa ya Afrika na Ufaransa unamalizika hii leo huko Nice Ufaransa.

https://p.dw.com/p/NeZy
Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy,mwenyeji wa mkutano kati ya Afrika na UfaransaPicha: AP

Viongozi wa Afrika wanatarajiwa kuweka mitazamo yao katika vita dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani.

Mwenyeji wa mkutano huo, Rais Nicolas Sarkozy katika kauli inayoonekana kuwafurahisha viongozi hao wa kiafrika, aliyataka mataifa yanayoendelea kutimiza ahadi zao yaliyozotoa katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Copenhagen za mabilioni ya dola kwa ajili ya nchi masikini.

Katika mkutano huo wa Copenhagen, Disemba mwaka jana, mataifa hayo yalikubaliana kutoa kiasi cha dola billioni 30, kwa muda wa miaka mitatu, ili kuzisadia nchi masikini kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Baadhi ya fedha hizo zitatumika kwa ajili ya uhifadhi ya msitu wa kongo ambao ni wa pili kwa ukubwa duniani baada ya ule wa Amazoni nchini Brazil.

Waziri Mkuu wa Ethiopea Meles Zenawi ndiye atakayekuwa mwenyekiti wa mjadala katika kikao cha leo kuhusiana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Mapema Rais Sarkozy alitaka Afrika kupatiwa nafasi katika mashirika ya kimataifa likiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

´´Hatuna tena muda wa kupoteza, nani rafiki wa afrika, Afrika ni lazima iwe na nafasi katika mashirika kote duniani.Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lazima lifanyiwe mabadiliko, Siyo kawaida kuwa Afrika haina nafasi ya kudumu katika baraza hilo´´

Naye Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini aliishutumu Ufaransa kwa kuwaalika viongozi waliyoingia madarakani kwa kupindua serikali, kutoka Guinea na Niger.

Süsafrika Jacob Zuma nach der Wahl
Rais Jacob Zuma wa Afrika KusiniPicha: AP

Zuma amesema hatua hiyo ni kuhamasisha mapinduzi barani Afrika.Amesema kuwa wanataka viongozi hao wasitambuliwe na jumuiya ya kimataifa.

Kwa upande wake msemaji wa Shirika la kutetea haki za binaadamu duniani la Human Right Watch, kanda ya Ulaya, Reed Brody, alikosoa mada zilizochaguliwa katika mkutano huo, na kwamba masuala kama ya haki za binaadamu hajapewa nafasi.

´´Nadhani kuna dhamira kwa pande zote mbili ya kuimarisha uhusiano na ushirikianao wao, lakini ili kuendeleza nia hiyo ni lazima pia ujiulize maswali magumu. Mkutano huu umechagua mada ambazo haziwezi kumkera mtu yoyote.Lakini huwezi kuzungumzia amani na usalama, bila ya kugusia masuala ya utawala bora, sheria na haki za binaadamu.Unaweza kuwekeza kiasi chochote cha fedha katika nchi kama vile , Guinea ya Ikweta, au Angola, au Chad, lakini fedha hizo zinapofika katika mikono ya watawala, basi tutakuwa hatujafanya chochote cha maendeleo kwa waafrika´´

Kiasi ya viongozi kutoka mataifa 38 barani Afrika wameudhuria mkutano huo, wenye nia ya kuimarisha uhusiano kati ya Ufaransa na bara la Afrika.

Mwandishi:Renate Krieger(HF-Portugiesich)Aboubakary Liongo

Mhariri:Mohamed Abdulrahman