1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano kati ya rais Mubarak na Peres

23 Oktoba 2008

Wakati Misri imeahidi kuhimiza kubadilishana wafungwa,Israel yakaribisha mpango wa amani wa waarabu.

https://p.dw.com/p/FfUS
Shimon PeresPicha: AP

Rais Hosni Mubarak wa Misri ameahidi hii leo kuimarisha upya juhudi za nchi yake za kupatanisha kubadilishana wafungwa kati ya Israel na Hamas.Hii inafuatia mazungumzo yake na mgeni wake huko Sharm el-Sheikh, rais Shimon Peres wa Israel.

Rais Peres akiwa amekaribishwa kwa shangwe na shamra shamra huko Sharm el-Sheikh - mwambao wa bahari ya Sham,ameungamkono ule mpango wa amani wa nchi za kiarabu uliotungwa na Saudi Arabia akiueleza ni fursa nzuri inayoweza kuleta amani Mashariki ya Kati.

Rais wa Israel alisema hayo wakati wa mkutano pamoja na rais Mubarak na waandishi habari .Peres alionya hatahivyo, kwamba haungimkono mapendekezo yote yaliomo katika mpango wa Saudi Arabia,lakini moyo wa mapendekezo yake anaukaribisha. Mpango wa Saudia wa mwaka 2002 unazitaka nchi za kiarabu kuitambua Israel ili Israel nayo ihame ardhi zote za waarabu ilizoziteka 1967.

Jumuiya ya nchi za kiarabu-Arab League yenye wanachama 22 imeuidhinisha mpango huo.Peres ambae wadhifa wsake hauna madaraka ya utendaji kinyume na rais Mubarak, alimtaka mfalme Abdullah wa Saudi Arabia mwezi uliopita kuuendeleza mpango wake na tangu wakati huo, ameiendeleza fikra hiyo kwa waisraeli,waarabu na maafisa wa nchi za magharibi.

Bw.Peres alikaribisha pia ahadi ya rais wa Misri kuongeza kasi juhudi zake za kuachwa huru kwa mwanajeshi wa Israel Gilad Shalit -hatua ambayo haitanufaisha ukoo wake bali umma mzima wa Mashariki ya Kati-alisema rais Peres.Rais Mubarak alithibitisha juhudi inazofanya misri kuziba mwanya kati ya msimamo wa israel na ule wa chama cha Haamas kinachotawala Gaza juu ya kuachwa huruz kwa wafungwa wa pande hizi mbili:

HAMAS kinadai kuachwa huru kwa wafungwa wake 1.400 waliopo katika magereza ya Israel wakati Israsel haiko tayari kuridhia kuacha huru wafungwa wengi namna hiyo.Rais Mubarak anakanusha lakini kuwa , mpango wa kubadilishana wafungwa kati ya pande hizo mbili umevunjika kabisa.

Juni mwaka huu, Israel na Hamas , ziliafikiana kusimamisha mapigano kwa muda wa miezi 6 tangu Gaza na vitongoji vyake na hivyo, kumaliza mapigano yaliodumu miezi kadhaa.

Licha ya maafikiano hayo, upande wa kubadilishana wafungwa hakuna maendeleo makubwa yaliofikiwa.

Rais Hosni Mubarak na Shimon Peres walizungumza pia juu ya mazungumzo ya amani yaliosita kati ya Israel na wapalestina. Mazungumzo haya yalikwama baada ya kutangaza kujiuzulu kwa waziri mkuu Ehud Olmert wa Israel.Wakati huu alieongoza mazungumzo hayo waziri wa nje Livni, anaongoza juhudi za kuanda serikali mpya ya muungano .

Rais Mubarak amesema mazungumzo ya leo yalihusika pia na kuhimiza mazungumzo ya amani baina ya Israel na wapalestina pamoja na kuimarisha utulivu mwambao wa gaza pamoja na kuwaondolea hatua za kuwazingira wakaazi wa Gaza.

Gazeti la HAARETZ la hapo jana liliarifu kwamba,rais Peres angependekeza mapatano yaliotungwa na afisi yake pamoja na ya waziri wa mambo ya nje Bibi Livni ,kujadiliana na waakilishi wa kila nchi ya kiarabu juu ya mpango wa amani wa Saudi Arabia ulioidhinishwa na Jumuiya ya kiarabu 2002."Livni anaelewa kila kitu nilichozungumza na rais Mubarak" alinukuliwa rais Peres kusema leo kabla kuondoka kurejea nyumbani.