1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano kuhusu hatima ya Kosovo wamalizika

P.Martin31 Agosti 2007

Matokeo muhimu ya majadiliano mapya yaliyofanywa mjini Vienna na tume ya upatanishi ya pande tatu yaani Umoja wa Ulaya,Marekani na Urusi pamoja na wajumbe wa serikali za Belgrade na Pristina ni kwamba Waserbia na Waalbania wa Kosovo watakutana uso kwa uso upesi iwezekanavyo.

https://p.dw.com/p/CH8h
Wolfgang Ischinger akizungumza na waandishi wa habari mjini Vienna baada ya mkutano wa tume ya pande tatu-Troika
Wolfgang Ischinger akizungumza na waandishi wa habari mjini Vienna baada ya mkutano wa tume ya pande tatu-TroikaPicha: AP

Mjerumani,Wolfgang Ischinger ambae ni mjumbe wa Umoja wa Ulaya katika tume ya upatanisho ya pande tatu au Troika amesema,wajumbe wa Kosovo na Serbia wamekubali kukutana tena pamoja na tume hiyo katikati ya mwezi wa Septemba na mwishoni mwa mwezi huo,ukingoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.

Kwa upande mwingine Waziri wa Masuala ya Nje wa Uholanzi,Maxime Verhagen alipokutana na viongozi wa Serbia mapema juma hili mjini Belgrade alishauri kulitenga jimbo la Kosovo.Lakini siku ya Alkhamisi,Ischinger alisema:

“Suala la kuitenga Kosovo wala halikuwepo katika ajenda ya leo na hakuna hata mjumbe mmoja alielizusha suala hilo mkutanoni.Tume ya pande tatu (Troika) inabakia na mwongozo wake unaopinga kuitenga Kosovo.“

Kwa mujibu wa Ischinger,pande zote mbili zimehakikisha kuwa hazitotamka wala hazitochukua hatua itakayoweza kutafsiriwa kuwa ni uchochezi. Mapema siku ya Alkhamisi,Waziri Mkuu wa Serbia Vojislav Kostunica aliionya jumuiya ya kimataifa kutowaruhusu Waalbania wa Kosovo kujitangazia uhuru wao.Kwa maoni ya Serbia,hatua hiyo ni uchochezi.

Serbia,ikiungwa mkono na Urusi,inapinga kabisa pendekezo lililotolewa na mjumbe wa Umoja wa Mataifa,Martti Ahtisaari kuwa Kosovo ipewe uhuru wa aina fulani utakaosimamiwa.Mradi huo lakini unaungwa mkono na Marekani na vile vile Umoja wa Ulaya.

Waziri Mkuu wa Kosovo Agim Ceku,siku ya Alkhamisi alisema,huo ni mradi ulio bora kabisa,kuunda taifa lililo imara na linalofanya kazi.

Ifikapo tarehe 10 mwezi wa Desemba,tume ya pande tatu,inatazamiwa kuwasilisha kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Ban Ki Moon ripoti ya majadiliano yaliofanywa kuhusu Kosovo.

Jimbo la Kosovo,linaongozwa na Umoja wa Mataifa tangu mwaka 1999,baada ya kampeni ya mashambulizi ya Shirika la Kujihami la Magharibi-NATO- kuvitmua vikosi vya Serbia.Kikosi cha wanajeshi 16,000 wa NATO kimebakia Kosovo.