1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano kuhusu kuenea kwa majangwa duniani

Maja Dreyer3 Septemba 2007

Mjini Madrid, Spain, kumeanza mkutano wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ambao unalenga kutafuta mbinu wa kusitisha kutambaa kwa majangwa duniani. Katika kufungua mkutano, wajumbe wa mkutano huo walitoa mwito kwamba kuenea kwa majangwa ni changamoto kubwa inayowakabili binadamu na inapita mipaka ya kisiasa.

https://p.dw.com/p/CHjS
Maeneo makavu yanatambaa nchini Kenya
Maeneo makavu yanatambaa nchini KenyaPicha: Maja Dreyer

Huu ni mkutano wa nane tangu nchi 191 zilizotia saini mapatano ya kupiga vita kuenea kwa majangwa mnamo mwaka 1994. Safari hii wajumbe wanatajariwa kuafikiana juu ya mpango ambao unatakiwa kuweka mkakati kwa muda wa miaka kumi ijayo wa kupambana na tatizo hili pamoja na kuweka malengo ya pamoja.

Waziri Cristina Narbona wa mambo ya ulinzi wa Spain, nchi ambayo pia inakabiliwa na majangwa kutambaa, analaumu kuwa katika miaka kumi iliyopita mapatano haya hayakutekelezwa vya kutosha. Amesema: “Haitoshi kuwa na mapatano lakini kutekeleza miradi michache tu kwa kutumia fedha kidogo. Inabidi kujitahidi zaidi katika kupiga vita pia majangwa kuenea. Hilo si tatizo tu la nchi maskini, kama wengi walivyoamini.”

Ulimwenguni kote theluthi moja ya ardhi ni maeneo makavu na kwa hivyo yanaweza kukauka zaidi na kuwa majangwa. Mabara yanayokabiliwa hasa ni Afrika, Asia, Amerika Kusini na vilevile Ulaya. Juu ya hayo, idadi ya watu wanaoishi kwenye maeneo haya makavu inazidi kuongezeka, kama anavyoeleza Gregoire de Kalbermatten, katibu mkuu wa mkutano huu wa Madrid: “Katika kipindi cha miaka kumi hivi, idadi ya watu wanaoishi katika maeneo makavu imekua mara nne na leo watu takriban Billioni mbili. Ikiwa hali ya ardhi inazidi kuwa ni ngumu barani Afrika, huenda robo tatu ya watu hao watategemea misaada ya chakula hadi mwaka 2025.”

Katibu mkuu Kalbermatten pia anatoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa kushughulikia tatizo hilo kwa haraka, la sivyo litawakabili wote. Spain ni moja kati ya nchi ambazo tayari zinawahi kuona matokeo ya kuenea kwa majangwa, kwani kila wiki Waafrika wengi hufika kwenya pwani ya nchi hiyo Kusini mwa bara la Ulaya wakikimbia kutoka hali ngumu ya maisha kule makwao.

Kulingana na uchunguzi ulifanywa na Umoja wa Mataifa, sababu mkubwa ya kuenea kwa majangwa ni matumizi mabaya ya ardhi na maji katika maeneo makavu, mfano kukata miti au kufuga wanyama wengi wanaoamaliza majani yote pale wanapolishwa. Sababu nyingine ni ongezeko la wakaazi na mabadiliko ya hali ya hewa. Ili kutafuta suluhisho ni muhimu kuzingatia hali ya kijamii na ya kiuchumi ya wakaazi wa maeneo haya. Kwa sababu hiyo, mashirika mengi yasiyo ya kiserikali pia yanahudhuria mkutano wa Madrid.

Waziri Narbona wa Spain anataka wajumbe wa mkutano wa Madrid kusogeza mbele kutoka kufanya uchunguzi kuelekea kuchukua hatua. Pia anataka miradi ya kupambana na ukame igharamiwe zaidi kwa kutumia sehemu ya bajeti ya miradi mingine ya Umoja wa Mataifa, mfano mradi wa kulinga hali ya hewa. Bi Narbona ametoa hoja kwamba kwa kuzuia ardhi isikauke ni hatua ya kuzuia mabadiliko ya hali ya hewa, kwani kukata miti kunazidisha ongezeko la hali ya hewa na pia kunasababisha mafuriko wakati wa mvua nyingi.