1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

230409 Energiegipfel Russland

Charo Josephat23 Aprili 2009

Urusi kupigania nafasi yake kama msafirishaji mkubwa wa gesi

https://p.dw.com/p/HcjE
Waziri mkuu wa Bulgaria, Sergei StanishevPicha: AP

Mkutano kuhusu maswala ya nishati unaanza leo mjini Sofia nchini Bulgaria, ambapo tofauti ya maoni kati ya Umoja wa Ulaya na Urusi itajadiliwa upya. Mkutano huo unafanyika baada ya mikutano mingine miwili kuhusu nishati kuanza jana nchini Urusi na Turkimenistan. Tangu mzozo wa gesi kati ya Urusi na Ukraine mwezi Januari mwaka huu, Umoja wa Ulaya unataka uhuru wake kutokana na kuitegemea gesi ya Urusi. Serikali ya mjini Moscow kwa upande wake haitaki kuachilia.

Waziri mkuu wa Urusi, Vladamir Putin, hatohudhuria mkutano kuhusu nishati unaofanyika mjini Sofia nchini Bulgaria licha ya kwamba kuhudhuria kwake kulikuwa kumethibitishwa. Waziri wa mashauri ya kigeni wa Bugaria, Ivaylo Kalfin, amesema Putin hatohudhuria mkutano huo kwa sababu ya mzozo kuhusiana na mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirishia gesi kupitia chini ya bahari ya Black Sea.

Mradi huo unasimamiwa na kampuni ya Urusi ya Gazprom na kampuni ya ENI ya Italia na unalenga kuisafirisha gesi ya Urusi kupitia bahari ya Black Sea kwenda nchini Bulgaria na baadaye nchini Austria, Ugiriki na hatimaye Italia.

Bulgaria ambayo tayari inasafirisha gesi ya Urusi kwenda nchini Ugiriki, Serbia na Macedonia kupitia mfumo wake wa usafirishaji wa gesi, haitaki mabomba yake yatumiwe kwenye mradi huo mpya. Badala yake inasisitiza kwamba mfumo mwingine wa mabomba ujengwe kwa ajili ya mradi huo.

Lakini Urusi kwa upande wake inashinikiza mabomba ya gesi yaliyopo yatumiwe kwa mradi huo. Swala hilo huenda lijadiliwe kwenye mkutano kati ya waziri mkuu wa Bulgaria, Sergey Stanishev, atakapozuru Moscow kati ya Aprili 26 na 28.

Ausschnitt Der russische Präsident Wladimir Putin
Waziri mkuu wa Urusi Vladamir PutinPicha: picture-alliance/dpa

Putin amekasirika

Waziri mkuu wa Urusi, Vladamir Putin, bado amekasirika kutokana na hatua ya Umoja wa Ulaya na Ukraine kusaini mkataba unaoiwezesha Ukraine kuwa na mfumo wake huru wa usafirishaji wa gesi, bila kuifahamisha Urusi ambayo ndiyo nchi inayomiliki gesi hiyo.

Pia kuna mkataba wa muda mrefu kuhusu ushirikiano katika maswala ya nishati kati ya Turkmenistan na kampuni ya RWE. Waziri mkuu Vladamir Putin alimuonya meneja wake muhimu wa kampuni ya Gazprom, Alexei Miller na naibu waziri mkuu Igor Sechin kuzuia mkataba huo na kudhibiti hali ya mambo.

Ikiwa Urusi inataka katika siku za usoni kuendelea kuwa na ushawishi mkubwa, mkuu wa jumuiya ya kampuni za gesi nchini Urusi, Valerij Jazew, anasema wataalam wa nishati nchini Urusi wanalazimika kujishughulisha zaidi.

"Naitolea wito kampuni ya Gazprom, kuinunua gesi yote kutoka nchi za katikati mwa bara la Asia."

Umoja wa Ulaya na Marekani kuwakilishwa

Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barosso, na viongozi wa serikali na marais kutoka mataifa saba ya eneo la Balkan, Georgia na Qatar, watahuhuria mkutano huo wa siku mbili mjini Sofia hii leo. Urusi itawakilishwa na waziri wake wa nishati, Sergey Shmatko huku Marekani ikiwakilishwa na mjumbe wake maalum wa nishati barani Ulaya na Asia, Richard Morningstar. Ufaransa, Ujerumani na Austria zitawakilishwa na wataalam.

Kama utawala wa Kremlin mjini Moscow, Jazew anayashuku mataifa ya Ulaya kwa kuwa na njama ya kuiondoa Urusi kutoka soko la nishati la kimataifa. Ana uhakika kuwa lazima kuwe na swala lengine la siri mbali na kutaka kuipanua biashara ya nishati.

"Tuanzie na mkataba uliosainiwa na Ukraine na Umoja wa Ulaya. Mkataba huo ulikuwa kilele cha mlima wa tatizo hili. Hayo ni matokeo ya kazi ya Umoja wa Ulaya, ili kuiondoa Urusi na kampuni ya Gazprom kutoka barani Ulaya."

Marais wa nchi muhimu zinazosafirisha gesi, Kazakhstan na Turkmenistan, watatuma wajumbe wao maalum kwenye mkutano wa mjini Sofia utakaowaleta pamoja watumiaji kutoka nchi za Umoja wa Ulaya na wasambazaji kutoka eneo la Caspian, Asia ya Kati na Mashariki ya Kati.

Mwandishi: Christina Nagel/Josephat Charo

Mhariri: Abdul-Rahman