1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano kutafuta njia za kukabiliana na Uharamia waanza Mjini Naiorbi, Kenya

Eric Kalume Ponda11 Desemba 2008

Mkutano wa kimataifa kujadilia tatizo la uharamia katika pwani ya Somalia umeanza hii leo katika mji mkuu wa Kenya Nairobi. Mkutano huo wa siku moja unahudhuri na waakilishi kutoka jumla ya mataifa 40 .

https://p.dw.com/p/GDdp
Baadhi ya meli zinazozuiliwa na maharamia katika pwani ya Somalia. Zaidi ya meli 100 zimetekwa nyara na maharamia mwaka huu.Picha: AP



Mkutano huo unafanyika huku baraza la mawaziri nchini Ujerumani likiridhia kupeleka kikosi cha wanajeshi 1,400 katika eneo la ghuba ya Eden.


Miongoni mwa ajenda kuu zinazotarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na mapendekezo yaliyotayarishwa na Umoja wa mataifa kuhusu njia za kuisaidia Somalia kuwa na serikali dhabiti, ambayo itasaidia katika vita dhidi ya Uharamia katika pwani yake.


Wajumbe wanaohudhuria mkutano huo pia wanatarajiwa kutoa mapendekezo yatakayowezesha kukamatwa na kushtakiwa kwa maharamia, pamoja na mchango wa jamii ya kimataifa kupeleka vikosi vya usalama katika eneo hilo ambalo sasa linatajwa kuwa hatari zaidi.


Tayari baraza la mawaziri nchini Ujerumani limeridhia kupelekwa kwa kikosi cha wanajeshi 1,400 na manuari katika eneo la upembe mwa Africa na ghuba ya Aden kama sehemu ya mchango wa oparesheni za vikosi vya mataifa ya Umoja wa Ulaya kukabiliana na visa vya uharamia katika pwani hiyo ya Somalia.


Hii ni mara ya kwanza kwa vikosi vya jumuiya ya Ulaya kushiriki zoezi la kupambana na vita dhid ya uharamia kwa kutumia manuari na ndege za kivita kudumisha usalama dhidi ya uharamia katika eneo la Ghuba ya Eden, mbali na kutoa usalama kwa misafara ya mashirika ya kutoa misaada kwa raia wengi wanaohitaji misaada nchini Somalia.


Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Frank Josef Jung, amesema kuwa kuweko kwa manuari za nchi za Umoja wa Ulaya katika eneo hilo kutawatisha maharamia na ikiwa dharura vikosi hivyo vitalazimika kutumia silaha.


Serikali ya Ujerumani ambayo ni miongoni mwa mataifa makubwa ulimwenguni yanayouza na kuagiza bidhaa zake kwa wingi katika nchi za nje, hutumia sana usafiri wa kutumia vyombo vya baharini, na hivyo basi ipo haja ya kwa taifa hilo kushiriki katika oparesheni ya kudumishwa kwa usalama huo. Bunge la Ujerumani linatarajiwa kuidhinisha mpango huo mnamo tarehe 19 mwezi huu.


Kwa upande wake mesmaji wa serikali ya Ujerumani Ulirich Wilhem,alisema kuwa biashara inayotokana na misafara ya baharini inaendelea kuongezeka, hivyo basi ni muhimu kwa Ujerumani kushiriki katika oparesheni hiyo.


Visa vya uharamia vimeongezeka katika siku za hivi majuzi katika pwani hiyo ya Somalia ambapo zaidi ya Meli 100 zimeshambuliwa na kutekwa nyara mwaka huu, na kisa cha hivi punde zaidi ikiwa ni kutekwa nyara kwa ile meli ya Mafuta ya Saudia. Maharamia hao bado wanaizuliwa meli hiyo iliyo na shehena na mafuta ya thamani ya dola milioni 100. Mbali na hayo maharamia hao pia bado wanazuilia meli zaidi ya melin 15 wafanyi kazi wasiopungua 300 wa meli hizo.