1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano mkuu juu ya kuwasaidia watu wa Darfur

Miraji Othman5 Mei 2008

Mkutano wa kuwasaidia watu wa Darfur unaanza leo mjini Oslo.

https://p.dw.com/p/Dtjd
Kaburi la watu wengi huko DarfurPicha: AP


Pale nchi fadhili hii leo zinaposhauriana mjini Oslo, mji mkuu wa Norway, kuhusu namna ya kuwasaidia watu wa Mkoa wa Sudan wa Darfur ulio katika mzozo, bila ya shaka msaada huo hivi sasa unahitajika zaidi kuliko wakati wowote mwengine, licha ya kwamba imepita miaka mitano tangu kuanza mapigano katika eneo hilo. Mazungumzo ya amani yaliofanyika katika miaka iliopita hayajaleta tija, na uwezekano wa kupatikana suluhisho kutokana na mashauriano umezidi kupotea. Sababu hasa ni kusambaratika kwa makundi mbali mbali ya waasi. Mamilioni ya watu inawabidi wabakie katika hali tete ya usalama kwenye makambi, na hawawezi kurejea katika vijiji vyao.


Shirika la Mpango wa Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa, WFP, limepeleka tani 423,000 za vyakula hadi Darfur. Jumuiya ndogo za kutoa misaada, kama ile ya Kupambana na Njaa Duniani, pia zinawasaidia malaki ya watu katika eneo hilo la Darfur. Kiasi cha watu milioni tatu katika eneo hilo wanahitaji misaada. Na licha ya kwamba mzozo huo umedumu sasa miaka mitano, hali za watu huko zinazidi kuwa mbaya. Ubaya zaidi ni kwamba bei za vyakula duniani zimepanda, na huko Sudan ughali huo umeongezeka kwa asilimia 500. Halafu kunaengezeka suala la njia za hatari za kuvisafirisha vyakula hivyo kutoka Bandari ya Port Sudan hadi Darfur kwenyewe, masafa ya kilomita 1000, na baada ya hapo hadi katika maeneo ambako vyakula hivyo vinahitajika sana.


Corine Fleischer, mratibu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, anasema suala la kusafirisha bidhaa za misaada hadi kuwafikia walengwa huko Darfur kwake yeye ni kama jinamizi. Mara nyingi malori yanayobeba misaada hiyo pamoja na madereva wao hutekwa nyara.


Hadi mwanzoni mwa mwezi huu, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, limebidi lipunguze resheni za vyakula zinazotolewa kwa watu kwa asilimia 40 ili vyakula hivyo viweze kufika hadi mwisho wa mwaka huu. Na hali hiyo inafanyika licha ya kwamba hivi sasa inahitajika misaada mingi ipelekwe ili ijalizie wakati wa mvuwa, pale njia nyingi zinakuwa hazipitiki. Wakimbizi hivi sasa wanapatiwa tu kalorie 1242 kwa siku kwa kila mmoja wao, na kima hicho ni chini ya mahitaji ya mtoto mwenye umri wa miaka mitano. Mabingwa wanahofia kwamba katika miezi ijayo kutatokea balaa la njaa ambalo litawaathiri zaidi vijana wanaotapia mlo. Hivi sasa ni tani 900 tu za vyakula kwa siku zinazofika huko Darfur. Lakini Salih Osman, wakili anayeshughulikia harakati za kupigania haki za binadamu na pia ni mbunge wa kutokea Darfur, ana hamu ya kuona jambo tu, nalo ni usalama:


O.Ton Salih:


+Nyinyi mnatuma fedha na badae mnahisi raha kwa vile mnatubakisha kuwa hai. Lakini tunahitaji ulinzi, tunahitaji kurejea majumbani kwetu, tunaweza kuzalisha vyakula kwa ajili yetu wenyewe, si ni wachapaji kazi sana. Ni vizuri, tunaishukuru jamii ya kimataifa kwamba imewazesha watu milioni 5 kubakia kuwa hai hadi leo, lakini tunahitaji zaidi, tunahitaji kurejea majumbani kwetu."


Si wanajeshi wa serekali wala makundi ya waasi yaliosambaratika sana yanayoweza kuleta amani. Na hadi sasa ni asilimia 40 tu ya wanajeshi wa usalama 26,000 wa Umoja wa Afrika, AU, na Umoja wa Mataifa, waliopangwa kuweko Darfur, ambao wamewasili huko. Na wanajeshi hao wanakosa hasa fedha. Inatajwa kwamba idadi kamili ya wanajeshi hao wa kuweka amani haitafikiwa kabla ya mwaka 2009.


Ni siku chache tu zilizopita, pale wanajeshi wa Umoja wa Mataifa na wale wa Umoja wa Afrika, AU, ilibidi wavihamishe vijiji vya kaskazini ya Darfur ambavyo vilikuwa katikati wakati wa mapigano baina ya waasi na majeshi ya serekali. Inasemakana idadi ya wakimbizi wa kutokea Darfur sasa inafikia milioni 2.5, huku watu laki mbili sasa wanaaminiwa wameuwawa tangu mapigano yaanze mwanzoni mwa mwaka 2003. Na idadi ya waliokufa inaweza kuwa kubwa zaidi hadi kufikia laki tatu, ukitilia maanani watu waliokufa kutokana na magonjwa na maambukizi yalioenea katika kambi za wakimbizi. Wiki chache zilizopita, zahanati ya Shirika la Madaktari Wasiojali Mipaka ambayo iliwapa hifadhi mamia ya watu waliokuwa wanayakimbia mapigano pia ilishambuliwa.