1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano Mkuu wa chama cha Fatah

5 Agosti 2009

Chama cha Fatah cha Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas kinaendelea na siku ya pili ya mkutano wake mjini Bethlehem ambako kama wajumbe 2,000 wanajadili mkakati mpya wa chama kikubwa kabisa cha kisiasa cha Wapalestina.

https://p.dw.com/p/J4Fz
Palestinian President Mahmoud Abbas speaks during the Fatah conference in the West Bank town of Bethlehem, Tuesday, Aug. 4, 2009. The Palestinians' Fatah movement came together Tuesday for its first convention in 20 years, trying to rise from division and defeat with a pragmatic political program and new leaders, in what its supporters hope will be the final push toward Palestinian statehood. (AP Photo/Tara Todras-Whitehill)
Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas akizungumza katika mkutano mkuu wa chama cha Fatah.Picha: AP

Siku ya pili ya mkutano huo ambao ni wa kwanza kupata kufanywa tangu mwaka 1989, imeshuhudia marumbano makali,baada ya baadhi ya wajumbe kutaka uwajibikaji zaidi upande wa chama cha Fatah cha Rais Abbas. Lengo la mkutano huo ni kuwachagua viongozi wapya, kuondosha dosari za chama hicho na kukiwezesha kuwa changamoto kwa chama hasimu cha Hamas mbele ya Wapalestina.

Lakini mamia ya wajumbe mkutanoni leo hii wamekuwa wakilalamika kuwa wanachama wakongwe wa Fatah wanajaribu kuufanyia udanganyifu uchaguzi wa Kamati Kuu yenye wajumbe 21 na Baraza la Mapinduzi linalowakilishwa na wajumbe120-bodi mbili muhimu kabisa kuhusika na maamuzi ya chama cha Fatah. Mjumbe Hussam Khader amesema kuwa dai lake la kutaka kuelezwa jinsi fedha za chama zilivyotumiwa, limepingwa na Rais Abbas. Wajumbe mkutanoni wamesema kuwa wao hawakuridhika na maelezo ya kamati za Fatah kuwa hotuba ya ufunguzi wa mkutano, iliyotolewa na Rais Abbas siku ya Jumanne, ni sawa na ripoti ya uongozi wa chama cha Fatah kwa miaka 20 iliyopita.

Rais Abbas hakushiriki katika mijadala ya leo hii lakini, alipaswa kuitwa ili kusaidia kutuliza mabishano makali yaliyozuka mkutanoni. Alisema kuna makosa yaliyofanywa au hata madhambi, lakini hayo yote yanapaswa kujadiliwa katika mikutano ya kamati na sio kufanya ghasia. Lakini Abbas binafsi alikatizwa na vikosi vya usalama vililipaswa kuingilia kati kwa muda mfupi. Baadae Abbas akasema kuwa wamekutana ili waweze kukirekebisha chama cha Fatah na sio kulipiza kisasi.Mivutano ya ndani na madai ya ufisadi yamekidhoofisha kisiasa chama cha Fatah kilichokuwa kikiungwa mkono na Wapalestina wengi sana kabla ya kifo cha mwasisi wa chama hicho marehemu Yasser Arafat kilichotokea mwaka 2004.

Rais Mahmoud Abbas katika hotuba yake ya ufunguzi, alijaribu kuwaridhisha wanachama wenye misimamo ya wastani na wale wenye misimamo mikali likiwemo pia tawi la vijana wenye siasa kali na walio na wasiwasi na mchakato wa amani unaoyumba. Alisisitiza kuwa anaunga mkono majadiliano ya amani lakini Wapalestina pia wana haki ya kutoa upinzani. "Silaha" ni neno aliloepukana nalo .Abbas akawahimiza wajumbe kuutumia mkutano huo kama jukwaa la kufungua ukurasa mpya katika chama cha Fatah.

Wakati huo huo, wanachama wa Fatah kutoka Ukanda wa Gaza waliozuiliwa na chama hasimu cha Hamas kwenda mkutanoni mjini Bethlehem, wanataka kugaiwa sehemu yao ya vyeo katika kamati za uongozi zitakazochaguliwa. Mkutano huo umepangwa kumalizika siku ya Alkhamisi lakini kwa sababu ya mivutano iliyozuka kati ya wajumbe na viongozi kuhusu mada za kujadiliwa, huenda ukaendelea kwa siku moja au mbili zaidi.

Mwandishi:P.Martin/DPA/AFP

Mhariri: M.Abdul-Rahim