1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano mkuu wa chama cha Republican waanza

28 Agosti 2012

Baada ya kimbunga cha "Isaac" kuwalazimisha wanachama wa Republican kuahirisha mkutano wao wa kumteua Mitt Romney kuwa mgombea rasmi wa urais, hatimaye mkutano huo umeanza mjini Tampa.

https://p.dw.com/p/15yB4
Mkutano wa Republican waanza
Mkutano wa Republican waanzaPicha: picture-alliance/dpa

Miaka minne iliyopita, kimbunga "Gustav" kilizuka wakati ambapo wanachama wa Republican walikuwa katika mkutano wao mkuu wa kumteua mgombea wa urais John McCain. Ingawa kimbunga "Isaac" hakitafika katika mji wa Tampa ambapo mkutano wa chama unafanyika mwaka huu, kimbunga hicho kitasababisha mvua nzito kunyesha . Kwa sababu hiyo, mkutano uliokuwa umepangwa kuanza jana unaanza hii leo na utaendelea hadi Alhamisi. Mwenyekiti wa chama, Reince Priebus, jana aliufungua mkutano na kisha kueleza kwamba umeahirishwa.

Kutokana na kuahirishwa huko, wanachama wa Republican sasa wamebakiwa na siku tatu tu badala ya nne, kwa ajili ya kumtambulisha rasmi mgombea wao wa urais. Kwa mujibu wa taasisi ya utafiti wa maoni ya wapiga kura iliyopo Marekani, lengo kuu la mkutano wa wanachama wa Republican ni kumtambulisha Mitt Romney kwa wale wasiomfahamu na kumtambulisha upya kwa wale wasiompenda. "Jambo la muhimu ni kuuonyesha ubinadamu wake," alisema Peter Brown kutoka taasisi hiyo ya utafiti na kutabiri kwamba washirika wa Romney wataelezea mafanikio ya mwanasiasa huyo pamoja na kuutambulisha mpango wake wa uchumi wenye lengo la kuuboresha uchumi wa Marekani.

Wanasiasa maarufu kuzungumza

Mpaka sasa inaonekana kwamba raitba ya mkutano wa chama cha Republican haujaathirika sana na kusogezwa mbele kwa tarehe ya ufunguzi. Sehemu kubwa ya watu waliotakiwa kutoa hotuba zao jana watapewa nafasi siku nyingine. Mke wa Romney, aliyepaswa kuzungumza mbele ya umati hapo jana atafanya hivyo leo. Waalikwa wengine watakaouhutubia mkutano mkuu ni aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Bi Condolezza Rice na Seneta John McCain aliyegombea urais mwaka 2008. Watakuwepo pia baadhi ya wanasiasa walioshindwa na Romney katika kinyang'anyiro cha kumtafuta mgombea wa Republican. Miongoni mwao ni Newt Gingrich na Rick Santorum. Watoa hotuba wa muhimu zaidi watakuwa Romney mwenyewe pamoja na Paul Ryan ambaye ni mgombea wake mwenza.

John McCain ni miongoni mwa wale watakaotoa hotuba
John McCain ni miongoni mwa wale watakaotoa hotubaPicha: REUTERS

Kwa mujibu wa maoni ya wapiga kura, rais Barack Obama kwa asilimia chache anapewa uwezekano mkubwa zaidi wa kushinda uchaguzi. Hii ni kwa sababu Obama tayari anafahamika na wengi wameshafikia uamuzi wao. Kwa sababu hiyo, Obama ametumia muda mwingi sana kuwahimiza wafuasi wake kwenda kupiga kura ifikapo siku ya uchaguzi mwezi Novemba.

Kimbunga cha Isaac kinaweza kuwa tatizo kwa Romney iwapo vyombo vya habari vitaelekeza macho kwa kimbunga hicho badala ya kuuzungumzia mkutano mkuu wa chama cha Republican.

Mwandishi: Christina Bergmann

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Josephat Charo