1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano mkuu wa chama tawala nchini Korea ya kaskazini pengine ukamteuwa mrithi wa "kiongozi mpendwa" ambae hali yake si nzuri

Oumilkher Hamidou27 Septemba 2010

Kim Jong Il aitisha mkutano mkuu wa chama cha wafanyakazi miaka 30 baada ya yeye binafsi kuingia madarakani-jee anataka kumtangaza mwanawe wa kiume kuwa mrithi wake?

https://p.dw.com/p/PNuY
Kiongozi wa Korea ya kaskazini Kim Jong Il na mwanawe Kim Jong UnPicha: picture-alliance/dpa

Chama tawala cha Korea ya kaskazini kinaitisha mkutano wake mkuu kwa mara ya kwanza hii leo baada ya kupita miaka 30.Wadadisi wanahisi mtawala wa nchi hiyo Kim Jong Il anapanga kutangaza watakaokabidhiwa nyadhifa muhimu chamani na kumtangaza mwanawe wa kiume,Kim Jong Un kama mrithi wake madarakani.Yeye mwenyewe amekuja madarakani kufuatia mkutano mkuu wa chama mnamo mwaka 1980.

Uvumi kuhusu nani atakabidhiwa uongozi wa Korea ya kaskazini umeanza kuenea tangu "kiongozi mpenzi" kama Kim Jong Il" anavyoitwa nchini humo,alipopigwa na kiharusi mnamo mwaka 2008.Kwamba mkutano mkuu wa chama unaitishwa hivi sasa,bila ya shaka sababu inatokana na hali mbaya ya afya ya Kim Jong Il,anasema mtaalam wa masuala ya Korea ya kaskazini kutoka chuo kikuu huru cha Berlin-Werner Pfenning

"Ni dhahir kwa sababu,kwa muda sasa watu wanaona picha ambazo si za kuvutia za kiongozi huyo.Anaonyesha mgonjwa na dhaifu.Pengine wanaonyesha makusudi ili watu watambue kwamba "kiongozi mpendwa" hatoishi milele.Na ndio maana anajitahidi kupata jibu la haraka kuhusu suala la nani atashika nafasi yake."

Nje ya nchi hiyo inayojikuta katika hali ya upweke,hakuna anaemjua mteule huyo kim Jong Un.Anakadiriwa kuwa na umri wa chini ya miaka 30.Kuna picha yake moja alipokua na umri wa miaka 11 na ambayo anaonekana kushabihiana sana na babaake.Kijana huyo anasemekana amesomea katika shule moja ya Uswisi na anazungumza vizuri kijerumani,kiengereza na kifaransa pia.

Kim Jong Un anasemekana ni mcheshi,hapendi ugomvi.Hata hivyo wadadisi wanahisi sifa hizo sio zitakazoamua kama atakubaliwa na uongozi ,wanajeshi na taasisi za chama tawala cha wafanyakazi.

"Ni muhimu kusafisha njia kwaajili ya kizazi kipya",alisisitiza Kim Jong Il wakati wa ziara yake ya hivi karibuni katika jamhuri ya umma wa China.Alifuatana na mwanawe katika ziara hiyo na kuyatembelea maeneo mashuhuri ambayo yaliwahi kutembelewa na marehemu babaake ,muasisi,"rais wa kudumu" Kim Il Sung.

Wadadisi wanaamini kwamba Kim Jong Il anataka kutoa ishara na kuhalalisha kwamba mrithi wake,ambae ni mwanawe mwenyewe atashika nafasi yake hivi karibuni.Wadadisi wanahisi hiyo pia ndio sababu ya kuitishwa mkutano huu wa dharura wa chama tawala cha wafanyakazi.Wajumbe hawatowaidhinisha peke yao viongozi wepya,bali pia watamteuwa Kim Jong Un kama mrithi wa babaake madarakani.

Kwanza pengine Kim Jong Un atakabidhiwa wadhifa wa wastani katika uongozi wa chama ili baadae aweze kupanda katika daraja ya kupitisha uamuzi.

Wadadisi wanaamini wanachama wakongwe watapata shida kumuunga mkono kijana kama huyo ambae hana maarifa yoyote ya kisiasa.Hata jeshi linaweza kumtia kishindo.

Hata hivyo wachunguzi wa kigeni wanataraji kijana Kim,kutokana na maarifa aliyojikusanyia alipokua shule nchi za nje,atakuwa na moyo wa kutaka ushirikiano zaidi wa kimataifa kuliko babaake.

Mwandishi:Lehmann,Ana (DW Asien)/Hamidou Oummilkheir

Mpitiaji:Abdul-Rahman