1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano mkuu wa dharura wa chama cha upinzani cha Social Democratic-SPD mjini Berlin

Oumilkher Hamidou27 Septemba 2010

Wana Social Democratic wanajiandaa kwa chaguzi za majimbo sita ya Ujerumani mwakani katika wakati ambapo utafiti wa maoni ya umma uinaonyesha chama hicho kinazidi kujivunia imani ya wapiga kura

https://p.dw.com/p/PNVO
Wajumbe katika mkutano mkuu maalum wa SPD mjini BerlinPicha: picture-alliance/dpa

Chama cha upinzani cha Social Democratic nchini Ujerumani-SPD kilikua na mkutano mkuu maalum mjini Berlin jana ambapo viongozi wameonyesha jinsi walivyopania kurejesha upya imani ya wafuasi wao na kufaidika wakati huo huo na hali ya kudhoofika serikali ya muungano ya kansela Angela Merkel.

Mkutano huo maalum ulilengwa kudhihirisha jinsi chama cha SPD kinavyoanza kuja juu,mwaka mmoja baada ya pigo kubwa kuwahi kushuhudiwa katika historia ya chama hicho kikongwe cha kisiasa nchini Ujerumani,pale SPD kilipoondoka na asili mia 23 ya kura ya matokeo jumla ya uchaguzi mkuu.

Uchaguzi huo ulihitimisha serikali ya muungano wa vyama vikuu-SPD,na vyama ndugu vya CDU/CSU na kufungua njia ya kuingia madarakani serikali ya muungano wa CDU/CSU na waliberali wa FDP mjini Berlin.

"Pigo hilo liliuma kweli kweli"-amekiri matibu mkuu mwenza wa SPD bibi Andrea Nahles.

Jana jumapili SPD wamejitokeza wameshikamana kinyume na jinsi taasisi za maoni ya umma zilivyoashiria mwaka mmoja uliopita.

Utafiti wa maoni ya umma unaashiria asili mia 30 ya kura kwa SPD-kikipitwa kwa asili mia moja tuu na vyama ndugu vya CDU/CSU.

Wakiitumia mivutano isiyokwisha katika serikali ya muungano ya CDU/CSU na waliberali wa FDP, na jinsi wajerumani walivyokasirishwa na uamuzi wa serikali ya kansela Angela Merkel wa kurefusha muda wa matumizi ya nishati ya kinuklea,SPD wameutumia mkutano maalum wa jana kujiandaa kwa kampeni za uchaguzi katika majimbo sita ya shirikisho hapo mwakani.

Deutschland SPD Parteitag Sigmar Gabriel in Berlin
Mwenyekiti wa SPD,Sigmar GabrielPicha: AP

Mwenyekiti wa chama cha Social Democratic,Sigmar Gabriel ameahidi SPD itapigania zaidi usawa katika jamii na uhuru.Wengi wa wajumbe 500 waliohudhuria mkutano huo maalum mjini Berlin wameunga mkono mageuzi katika sekta ya kodi ya mapato,ajira na malipo ya uzeeni.

Sigmar Gabriel ameitumia fursa hiyo kumkosoa kansela Angela Merkel na kusema:

Angela Merkel hakutoa mchango wowote wa maana.Fikra zilikuwa zetu sisi.Bila ya shaka alikua kansela bora kwa wakati wote ule ambao wana Social Democrat tulikuwa tukimlinda."

SPD imejaribu pia kujitenganisha na walinzi wa mazingira walioshirikiana nao serikalini kati ya mwaka 1998 hadi 2005.

Hata hivyo mwenyekiti wa SPD Sigmar Gabriel amesema wazi lengo lao baada ya uchaguzi mkuu ujao mwaka 2013 ni kuunda tena serikali ya muungano pamoja na walinzi wa mazingira.

Mwandishi:Hamidou /dpa/afp

Imepitiwa:Abdul-Rahman