1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa amani Syria utaandaliwa lini?

21 Oktoba 2013

Hali ya sintofahamu inaonekana kuunzunguka mkutano wa kimataida wenye lengo la kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, kufuatia kauli zinazokinzana juu ya mkutano huo.

https://p.dw.com/p/1A33X
Kiongozi wa Jumuiya ya Kiarabu Nabil al-Arab na Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Lakhdar Brahimi
Kiongozi wa Jumuiya ya Kiarabu Nabil al-Arab na Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Lakhdar BrahimiPicha: Reuters

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ilitangaza jana kuwa mazungumzo yatafanyika mwezi ujao jijini Geneva, Lakini mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Lakhdar Brahimi amekanusha kuwepo kwa tarehe iliyopangwa kwa ajili ya mazungumzo hayo. Wakati huo huo, nchini Syria kwenyewe watu 43 wameuawa katika shambulizi lililofanywa na mlipuaji wa kujitoa mhanga.

Mkanganyiko huo wa kidiplomasia ambao ni wa kushangaza, baina ya mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Nabil al-Arabi na Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Lakhdar Brahimi, katika kikao cha pamoja cha waandishi wa habari mjini Cairo, unaendeleza mashaka juu ya uwezekano wa kuandaliwa kongamano hilo la amani.

Al-Arabi alisimama na kutoa matamshi haya mbele ya waandishi wa habari "Nimejadili suala la Syria na Lakhdar Brahimi na ikaamuliwa kuwa mkutano wa Geneva utafanyika Novemba 23 na maandalizi yanaendelea kwa ajili ya kongamano hilo. Yapo matayarisho mengi yakufanywa na vizuizi vingi ambavyo lazima viondolewe kabla ya kuyafanyikisha mazungumzo hayo".

Mabaki ya gari baada ya shambulizi la bomu la kujitoa mhanga mjini Hama, Syria
Mabaki ya gari baada ya shambulizi la bomu la kujitoa mhanga mjini Hama, SyriaPicha: Reuters

Kisha ulipowadia muda wa Brahimi kuzungumza, akasema "Kuna makubaliano ya kujaribu kuandaa kongamano la pili la Geneva mwezi Novemba kakini tarehe bado haijatangazwa rasmi".

Brahimi alionya kuwa mazungumzo hayo ya Geneva yataendelea tu ikiwa patakuwepo kile alichokiita “upinzani halali unaoiwakilisha sehemu kubwa ya wananchi wa Syria” ambao wanampinga Rais Assad. Alisema kuna makubaliano ya kuandaliwa mkutano wa awamu ya pili jijini Gevena maarufu kama Geneva 2, lakini akaongeza kuwa tarehe itatangazwa baadaye. Brahimi yuko katika mkondo wa kwanza wa ziara yake katika Mashariki ya Kati inayolenga kutafuta uungaji mkono kwa mpango huo wa amani. Amesema atazuru Qatar, Uturuki, Iran, Syria na kisha Geneva ili kufanya mazungumzo na wawakilishi wa Urusi na Marekani, zikiwa ni nchi mbili zilizoanzisha mpango huo.

Uamuzi kama kweli mazungumzo hayo yaliyosubiriwa kwa hamu yatafanyika au la, huenda ukatokana na mkutano wa upinzani nchini Syria mwezi ujao, ambao utajadili kama utakaa kwenye meza moja na utawala wa Rais wa Bashar al-Assad. Nchini Syria kwenyewe, gari lililokuwa na mabomu limelipuliwa na mlipuaji wa kujitoa mhanga katika kituo kimoja cha kijeshi mjini Hama. Takribani watu 43 waliuawa ikiwa ni pamoja na raia 32 huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika shambulizi hilo.

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Syria limesema wapiganaji wa kundi la Jabhat al-Nusra ambalo lina mahusiano na mtandao wa al-Qaeda lilifanya shambulizi hilo ambalo ni la pili kufanywa dhidi ya serikali katika siku mbili. Siku ya Jumamosi, wapiganaji waasi wa al-Nusra walilipua bomu jingine wakati wakikishambulia kituo kimoja cha serikali karibu na mji mkuu Damscus, na kuwauwa wanajeshi 16.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Daniel Gakuba