1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa kwanza wa viongozi wa BRIC.

Abdu Said Mtullya16 Juni 2009

Viongozi wa nchi zinazoinukia kiuchumi wanakutana mjini Yakaterinburg nchini Urusi.

https://p.dw.com/p/IAdf
Mwenyeji wa mkutano rais Medvedev wa Urusi.Picha: AP


Viongozi wa mataifa yanayoinukia kiuchumi leo wanafanya mkutano wao wa kilele kwa mara ya kwanza, katika mji wa Yakaterinburg nchini Urusi.

Pamoja na masuala mengine viongozi hao wanatarajiwa kusisitiza umuhimu wa kuleta mageuzi katika mfumo wa fedha duniani.

Mkutano huo unawaleta pamoja viongozi wa nchi zinazochangia asilimia 15 ya uchumi wa dunia yaani Brazil,Urusi,India na China. Fungu la fedha linalotokana na uchumi wa nchi hizo ni kiasi cha dola TRILLIONI 60.7

Viongozi wa nchi hizo pamoja na mwenyeji rais Dmitry Medvedev wataanza mkutano wao baadae leo katika mji wa Yakaterinburg mashariki ya mji mkuu wa Urusi,Mosko

Viogozi hao watajadili njia za kuleta mageuzi katika mfumo wa fedha wa dunia kufuatia mgogoro mkubwa wa uchumi ulioikumba dunia.

Msemaji wa serikali ya Urusi amefahamisha kwamba rais Dmitry Medvedev atawasilisha suala la akiba ya fedha za kigeni kwenye mkutano huo.

Msemaji huyo bwana Arkady Dvorkovich ameeleza kwamba katika nyakati hizi,hakuna nchi inayotaka kuona vurumai nyingine katika mfumo wa fedha duniani. Amesema hakuna anaetaka kuiteketeza dola.

Russland China Hu Jintao bei Wladimir Putin in Moskau
Rais Hu jintao wa China na waziri mkuu wa Urusi Putin.Picha: AP

Hapo awali kulikuwa na miito kutoka sehemu mbalimbali juu ya kutumia sarafu nyingine katika miamala ya kimataifa badala ya dola ya kimarekani.

Hatahivyo kabla ya mkutano huo rais Medvedev wa Urusi alishauri kwa viongozi wanaokutana leo juu ya kutumia fedha za nchi zao katika biashara baina yao.

Nchi hizo kwa pamoja zinamiliki dola trilioni karibu tatu katika akiba ya fedha za kigeni.

Rais wa Urusi amesema nchi zinazoinukia kiuchumi zinapaswa kuuimarisha mfumo wa fedha wa kimataifa siyo tu kwa kuiimarisha dola bali pia kwa kuanzisha sarafu nyingine ya akiba ya kigeni ; sarafu nyingine kwa ajili ya malipo, itakayokuwa juu ya fedha nyingine zote.

Wachunguzi wanaamini kwamba nchi zinazoinukia kiuchumi zinalenga shabaha ya kuighubika dola ya kimarekani katika miamala ya biashara baina yao.

Wachunguzi pia wanasema viongozi wa nchi zinazojulikana kama BRIC wanadhamiria kushirikiana kwa undani zaidi ili kuweza kukabiliana na athari za mgogoro wa uchumi- BRIC ni kifupi cha Brazil,Russia,India na China.

Hatahivyo wataalamu wanahoji kwamba umuhimu wa mkutano wa viongozi hao wa BRIC utakaochukua muda wa saa mbili utakuwa wa kisiasa zaidi kuliko kuwa wa kiuchumi.

Mkutano wa mjini Yakaterinburg unahudhuriwa na marais Hu jintao wa China, Luiz Lula da Silva wa Brazil,waziri mkuu wa India Manmohan Singh na mwenyeji rais Dmitry Medvedev wa Urusi.


Mwandishi:A.Mtullya /RTR

Mhariri:M.Abdul-Rahman

AFPE/RTRE/AFA.






Mkutano huo muhimu unazileta pamoja nchi zinazochangia asilimia 15 ya uchumi wa dunia.