1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Davos waanza Uswisi

John Juma
17 Januari 2017

Rais wa China Xi Jinping kufungua mkutano huo ambapo hotuba yake italenga kutetea utandawazi na biashara huru kati ya mataifa

https://p.dw.com/p/2VuIj
Weltwirtschaftsforum in Davos
Picha: World Economic Forum/Benedikt von Loebell

 

Mkutano wa kimataifa wa kiuchumi unaofanyika kila mwaka katika mji wa mapumziko wa Davos nchini Uswisi, unaanza leo. Mkutano huo unaowaleta pamoja zaidi ya wakuu 100 wa mashirika makuu duniani unafunguliwa rasmi na Rais wa China Xi Jinping.

Hotuba ya Rais Xi Jinping katika ufunguzi wa kikao cha leo inatizamwa kuwa kilele cha mkutano huo na kwa nchi za Ulaya na Uswisi. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa rais wa nchi ya pili kwa ukubwa kiuchumi baada ya Marekani kuhudhuria mkutano huo wa kila mwaka unaowaleta pamoja viongozi wa nchi na wakurugenzi wakuu wa mashirika.

Hotuba ya Xi itakayolenga kuimarisha amani ulimwenguni, kukuza maendeleo kwa pamoja na mfumo wa biashara iliyo wazi kwa wote ulimwenguni, inajiri wakati kukiwa na hofu kuwa rais ajaye wa Marekani Donald Trump huenda akaweka mikakati ya kukuza biashara za kibinafsi badala ya biashara huru na mataifa mengine. Akizungumza na wanahabari nchini Uswisi kabla ya mkutano, Xi alisema atatetea utawala ulio sawa na mwelekeo mwema duniani. Klaus Schwab ambaye ni mwanzilishi na mwenyekiti wa Jukwaa hilo la kiuchumi amesema ana matumaini mkutano utapata suluhisho kwa baadhi ya matatizo."Tunakutana wakati kuna mkanganyiko tele na maswali mengi sana. Tunayopaswa kuyafanya hapa ni kushughulikia vyanzo vya wasiwasi. Ninatarajia mjadala wenye ari unaolenga kupata suluhisho kwa pamoja."

Klaus Schwab
Klaus SchwabPicha: Reuters/P. Albouy

Mwakilishi pekee wa Donald Trump Anthony Scaramucci ambaye ni mshauri wake mkuu anatarajiwa kuelezea mkutano huo vipaumbele vya utawala wa Trump. Mkutano wa Davos unajiri wakati wanademokrasia katika nchi za magharibi wanakabiliana na kuibuka kwa ushawishi wa kizalendo, ikiwemo uliomsaidia Donald Trump kutwaa mamlaka. Kauli mbiu ya mkutano wa mwaka huu ni Uongozi wa uwajibikaji.

Eneo linakofanywa mkutano wa Davos
Eneo linakofanywa mkutano wa DavosPicha: World Economic Forum/Benedikt von Loebell

China ilitizamiwa kuwa mstari wa mbele kuunga mkono Jukwaa la Kimataifa la Kiuchumi WEF, baada ya Trump kusema ataondoa Marekani katika jumuiya ya kibiashara ya nchi kumi na mbili wanachama wa biashara ya Pasifik iliyoanzishwa na Rais Barrack Obama.

Urusi pia itawakilishwa na manaibu wawili wa waziri mkuu na wakuu wengine wa kibiashara. Washiriki 3,000 miongoni mwao wanasiasa, wakuu wa biashara, wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, wasomi na wanaharakati, wanatarajiwa kujadili masuala ya kiulimwengu yanayoweza kukabiliana na siasa za umaarufu, ukosefu wa usawa katika maendeleo ya teknolojia na kupungua kwa nafasi za ajira.

Mwandishi: John Juma/DPAE/RTRE/APE

Mhariri: Josephat Charo