1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Doha juu ya kuisaidia Darfur

8 Aprili 2013

Wawakilishi wa nchi wahisani na mashirika ya misaada wanakutana leo mjini Doha, Qatar ili kuunga mpango wa kuchangisha fedha kwa ajili ya kulijenga upya jimbo la Darfur.

https://p.dw.com/p/18BDs
Kambi ya Kalma ya wakimbizi wa ndani, Darfur
Kambi ya Kalma ya wakimbizi wa ndani, DarfurPicha: picture-alliance/dpa

Kiongozi wa ujumbe wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa, Jorg kuhnel amesema mkutano huo ni fursa ya kipekee kwa Sudan ya kuweza kuibadilisha hatma ya jimbo hilo lililokumbwa na migogoro.

Mkutano huo wa siku mbili, unaohudhuriwa na wajumbe 400, unafanyika kwa mujibu wa mkataba wa amani wa Julai mwaka 2011, uliotiwa saini mjini Doha baina ya Sudan na mfungamano wa makundi ya waasi.

Mkutano huo unafanyika miaka kumi baada ya waasi katika jimbo hilo la  magharibi mwa Sudan kuanzisha harakati za kukomesha walichoita udhibiti wa mamlaka na mali, wa viongozi wa kiarabu nchini Sudan.

Uhalifu wa Janjaweed :

Ili kuwakabili waasi ,wanamgambo  wa Janjaweed waliokuwa  wanaungwa mkono na serikali ya Sudan walitenda unyama dhidi ya raia,ulioishtua dunia na kuifanya Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague itoe hati ya kisheria ya kuwezesha kumkamata Rais wa Sudan Omar al-Bashir kwa tuhuma  za kutenda uhalifu wa kivita,uhalifu dhidi ya ubinadamu na mauaji halaiki.

Rais wa Sudan, Omar Hassan al-Bashir
Rais wa Sudan, Omar Hassan al-BashirPicha: picture-alliance/dpa

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia maendeleo Bwana  Kuhnel ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, baada ya miaka kumi ya kutegemea misaada ya  dharura,wakati sasa umefika wa  kuanza kuzijenga upya jamii za  Darfur na kuwawezesha watu wa  jimbo hilo kujihudumia wenyewe.

Uingereza yaahidi Pauni milioni 11 kwa mwaka:

Katika hatua ya kwanza,Uingereza imetoa ahadi ya kuchangia Pauni  Milioni 11 kila mwaka kwa ajili ya jimbo la Darfur kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.Fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kilimo cha mazao ya chakula na kwa ajili ya mafunzo yatakayowawezesha watu kupata ajira. Waziri wa Uingereza anaeshughulikia misaada ya maendeleo ya kimataifa Lynne Featherstone amesema haitoshi tu ,kutoa ruzuku zaidi. Waziri Featherstone ameeleza kuwa fedha hizo zitawasaidia masikini kupata nyenzo wanazohitaji ili kuweza kujisimamia wenyewe na hivyo  kuzikabili vizuri zaidi hali za migogoro zinapozuka.

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron
Waziri Mkuu wa Uingereza, David CameronPicha: AFP/Getty Images

Maendeleo ya kilimo:

Mpango utakaofadhiliwa na wahisani na mashirika ya kimataifa ni pamoja na kuboresha kilimo, kuwawezesha watu kupata misaada ya fedha na kuchukua hatua ili kuwasaidia watu wa Darfur kujisimamia wenyewe chini ya uongozi wa mfumo wa serikali ya jimbo hilo ,unaofanyakazi kwa ufanisi zaidi. Mkakati wa maendeleo ya jimbo la Darfur,unasisitiza kwamba wakati wa kuchukua hatua ni sasa, kwani kuchelewa kutasababisha mchakato huo uwe mgumu.

Hata hivyo wakati mikasa mibaya ya umwagikaji wa damu imeshapita, waasi na wanajeshi wa serikali wanaendelea kupambana,sambamba na mapambano baina ya jamii za kiarabu.

Wakati mgumu lakini hapana kushika tama

 Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia maendeleo,UNDP Bwana Kuhnel amekiri kwamba hizi ni nyakati ngumu duniani kukusanya fedha.Lakini amesema litakuwa kosa kubwa kutoitumia fursa iliyopo duniani. Ameeleza kuwa, siyo lazima fedha zote zinazohitajika zipatikane mara moja. Ameeleza kwamba kinachohitajika ni kuanza juhudi na kupata kiasi cha fedha kitakachojenga imani ya mkakati unaokusudiwa kutekelezwa.

Nembo ya UNDP
Nembo ya UNDPPicha: APGraphics

Usalama kwanza nyumbani:

Wakati huo huo wakimbizi wa ndani  katika jimbo la Darfur,katika kambi  kadhaa, walifanya maandamano kabla ya mkutano wa Doha kuanza kusisitiza ulazima wa kulipa kipaumbele suala la usalama.Watu  hao wamesema kuwa hawatarejea kwenye vijiji vyao kabla ya amani kurejea.

Justice and Equality Movement:

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alisema mapema  mwaka huu kwamba kukataa kwa makundi muhimu kuutia saini mkataba wa Doha kumepunguza hatua za utekelezaji wa mkataba huo.

Kundi moja lililojitenga na chama cha "Justice and Equality" hapo jana(Jumamosi) lilikuwa kundi la pili  kujiunga na mkataba wa Doha. Lilitiliana saini mjini Doha "makubaliano ya mwisho" na serikali  ya Sudan.

Mwandishi:Mtullya  Abdu/afpe,rtre
Mhariri: Grace Patricia Kabogo