1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G-20 wagubikwa na tofauti za maoni

P.Martin/afpe27 Juni 2010

Viongozi wa kundi la nchi zilizoendelea kiviwanda na zile zinazoinukia kiuchumi G-20,leo jioni watashauriana njia za kuimarisha uchumi duniani.

https://p.dw.com/p/O4K9
Chancellor Angela Merkel of Germany arrives in advance of the G8 and G20 Summit at Pearson International Airport in Toronto, Thursday, June 24, 2010. (AP Photo/Gerry Broome)
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel akiwasili Toronto Kanada kuhudhuria mikutano ya kilele ya G-8 na G-20.Picha: AP

Viongozi hao,kwenye mkutano huo uliogubikwa na tofauti za maoni, wanatazamia kukubaliana kuhusu hatua za kuchukuliwa kufuatia mzozo wa fedha uliotokea duniani.Wakati Marekani ikishinikiza kuongeza matumizi ili kunyanyua uchumi, nchi za Ulaya zinataka kudhibiti matumizi yake.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesisitiza kuwa hatua barabara za kupunguza matumizi, hazitokwamisha ukuaji wa kiuchumi. Tofauti zingine za maoni katika mkutano huo wa Toronto, zinahusika na pendekezo la Ujerumani na nchi zingine za Umoja wa Ulaya, kuzitaka benki kuweka akiba maalum ili katika siku zijazo, ziwe na uwezo wa kuhimili mzozo mwengine wa fedha.Merkel amesema, haamini kuwa kutapatikana makubaliano ya kimataifa kuhusu pendekezo hilo. Vile vile amesema haitokuwa rahisi kuafikiana kuanzisha kodi maalum kwa kila biashara ya ulanguzi inayofanywa na taasisi za fedha.

Kwa upande mwingine,machafuko yalizuka katika maandamano ya amani ya wanaharakati wa mazingira na wa kupiga vita umasikini. Zaidi ya wanaharakati 10,000 waliandamana, baada ya mkutano wa viongozi wa kundi la nchi nane tajiri zilizoendelea kiviwanda G-8 kumalizika mjini Toronto, bila ya kutekelezwa ahadi zilizotolewa hapo awali.

An activist runs past a burning police car in Toronto's financial district during the G20 Summit Saturday, June 26, 2010. (AP Photo/The Canadian Press, Darren Calabrese
Gari la polisi lililotiwa moto na wapinzani wa utandawazi.Picha: AP

Wapinzani wa utandawazi walichoma moto magari ya polisi na walifanya uharibifu katika maduka. Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchini humo zaidi ya watu 100 wamekamatwa.