1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G20 wakaribia muafaka kuhusu biashara

Daniel Gakuba
8 Julai 2017

Mnamo siku ya pili na ya mwisho, mkutano wa G20 mjini Hamburg unakaribia kupata muafaka juu ya biashara duniani, lakini suala la ulinzi wa mazingira bado linasababisha mpasuko mkubwa.

https://p.dw.com/p/2gBnn
G20 Hamburg Trump Merkel Tusk
Muafaka unakaribia kupatikana kuhusu biashara huria duniani, suala la mazingira labakia kuwa tetePicha: Reuters/I.Langsdon

Viongozi katika mkutano huo unaofanyika katika mji wa Hamburg Kaskazini mwa Ujerumani, wanajaribu kupata muafaka juu ya masuala muhimu kama biashara huria, kupambana na mabadiliko ya tabianchi, na vita dhidi ya ugaidi. Tangu mwanzo wake, mkutano huo umeghubikwa na maandamano ya kupinga utandawazi, ambayo mara nyingine yameishia katika vurugu.

Mada muhimu ya mkutano huu wa kilele wa G20 ni ushirikiano kati ya nchi zinazounda kundi hilo na bara la Afrika, katika masuala ya uhamiaji na afya. Agenda nyingine kwenye meza ya viongozi hao ni pamoja na kuendeleza mfumo wa digitali, kuwaongezea uwezo wanawake na kuunda nafasi za ajira.

Maafisa wahaha kutafuta muafaka

G20 Gruppenbild (picture alliance/dpa)
Viongozi wa nchi za G20: Ujerumani inataka kuendeleza utamaduni wa maamuzi yanayoafikiwa na wotePicha: picture-alliance/dpa

Jambo la kipaumbele ni namna viongozi wa kundi hilo la nchi zilizoendelea kiviwanda na zinazoinukia kiuchumi watakavyoweza kuweka msimamo wa pamoja juu ya biashara ulimwenguni na hatua za kukabiliana na ongezeko la joto duniani. Baada ya siku ya kwanza ya mazungumzo, mwenyeji na mwenyekiti wa mkutano huo, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema majadiliano kuhusu biashara hayakuwa rahisi.

''Kuhusu suala la biashara, karibu kila mmoja wetu anaamini kuwa tunahitaji biashara huru, lakini pia ya kunufaisha wadau wote'', amesema Kansela Merkel, na kuongeza, ''Lakini naweza kutabili kuwa maafisa watatoka jasho katika kukubaliana juu ya tangazo la mwisho. Sitaki kuzungukazunguka, mazungumzo yalikuwa magumu sana.''

Duru  zimeeleza muda mfupi uliopita kuwa muafaka unakaribia kupatikana kuhusu suala hilo gumu la biashara duniani, ambapo imeafikiwa kuondoa vizuizi vya kibiashara, huku lakini nchi zikiachiwa haki ya kulinda masoko yao.

Sera ya Trump yaweka kiunzi katika mazungumzo

Ujerumani imeazimia kuendelea utamaduni wa kundi la G20 wa kuchua maamuzi yanayoafikiwa na wote, lakini muafaka kuhusiana na biashara ya kimataifa unakuwa vigumu kupatikana, kutokana hasa na mtazamo wa Rais Donald Trump wa Marekani, na kauli mbiu ya utawala wake ya 'Marekani kwanza'. Hali kadhalika hatua ya utawala wake kuiondoa Marekani katika mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, imesababisha wasiwasi mkubwa kuhusu mafanikio ya mkataba huo uliosainiwa na nchi 195 mwishoni mwa mwaka 2015.

Hamburg G20 Gipfel - Proteste Schanzenviertel
Mkutano wa Hamburg umekumbwa na maandamano yenye ghasiaPicha: picture-alliance/dpa/C. Gateau

Wanachama wa kundi la G20 nia Argentina, Australia, Brazil, China, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, India, Indonesia na Italia. Nyingine ni Japan, Canada, Korea Kusini, Mexico, Urusi, Saudi Arabia, Afrika Kusini, Uturuki, Marekani, na Umoja wa Ulaya. Katika mkutano huu wa Hamburg zilialikwa pia Uholanzi, Norway, Uhispania, Guinea, Senegal, Singapore na Vietnam.

Papa Francis aiponda G20

Jana Kansela Merkel alizungumzia umuhimu wa viongozi wanaokutana mjini Hamburg kuzingatia maslahi ya wakazi wa nchi zisizoshiriki katika mazungumzo haya, kwa sababu maamuzi yanayochukuliwa yanaathiri maisha ya wakazi wa sehemu kubwa ya dunia.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ameelezea hofu kubwa kuhusu nguvu waliyonayo viongozi wa G20, akiliita kundi hilo ''Muungano wa hatari dhidi ya wanyonge duniani''. Papa Francis amenukuliwa na gazeti la Repubblica la nchini Italia, akisema maamuzi ya viongozi hao yanaathiri wahamiaji katika nchi ambazo zinaunda nusu nzima ya dunia, na kwamba kitisho cha muungano huo kinazidi kukua kadri siku zinavyosonga mbele.

Kikao cha leo Jumamosi kinafuatia usiku wa ghasia mjini Hamburg, ambako waandamanaji wanaopinga utandawazi wamefanya ghasia mitaani, wakiwasha moto barabarani na kupora maduka makubwa ya kibiashara. Waandamanji hao pia wamewavamia polisi na kuwarushia mabomu ya petroli. Mamia ya polisi waliingia katika kitongoji cha Schanzenviertel kuwakamata wafanyafujo. Polisi wapatao 160 walijeruhiwa katika ghasia hizo jana Ijumaa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape,rtre,afpe

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman