1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G20 wamalizika kwa maafikiano makubwa

5 Septemba 2016

Rais Xi Jinping wa China amesema Mkutano wa Kilele wa kumi na moja wa nchi za kundi la G20 umemalizika Jumattau (05.08.2016) nchini China kwa maafikiano juu ya masuala mbali mbali muhimu.

https://p.dw.com/p/1Jw8I
Picha: Reuters/D. Sagolj

Rais Xi Jinping wa China nchi iliyoandaa mkutano wa Kilele wa kundi la G20 akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo uliofanyika katika mji wa kihistoria wa Hangzhou ulioko mashariki mwa China.

Katika taarifa ya pamoja Rais Xi Jinping wa China na wenzake wa Marekani,Uingereza,Japani, Urusi na Ujerumani na nchi nyenginezo zenye maendeleo makubwa ya kiuchumi duniani halikadhalika zile zinazoinukia kiuchuni wameahidi kuimarisha ukuaji wa uchumi unaozorota duniani kwa kuendeleza ubunifu.

Xi amewaambia waansihi wa habari baada ya mkutano huo kwamba kufufuka kwa uchumi wa dunia kunakosa msukumo na kwamba wanahitaji kuchukuwa hatua zaidi kukwamuwa ukuaji wa uchumi wa kipindi cha wastani na kipindi cha muda mrefu.

Suala la hatua ya pamoja

Suala la kuuchochea uchumi huo wa dunia wala kuchukuliwa kwa hatua ya pamoja hayakutajwa ambapo hapo awali maafisa walisema hayatekelezeki kwa sababu hali za kiuchumi zinatafautiana sana kutoka nchi na nchi.

Rais Barack Obama wa Marekani na Rais Vladimir Putin wa Urusi mjini Hangzhou.
Rais Barack Obama wa Marekani na Rais Vladimir Putin wa Urusi mjini Hangzhou.Picha: picture-alliance/Russian Presidential Press and Information Office/Tass/A. Druzhinin

Katika juhudi za kuchochea uungaji mkono wa wananchi viongozi hao wameahidi ukuaji wa uchumi shirikishi ili kueneza matunda yake kwa wananchi walioachwa nyuma na mabadiliko makubwa.Hali hiyo inaonyesha kutambuliwa kwamba matatizo ya uchumi yanachochea mivutano ya kisiasa na shauku inayoongezeka ya kuweka vikwazo dhidi ya ushindani wa kigeni.

Taarifa yao hiyo imepinga aina zote za hatua za kuhami masoko katika biashara na uwekezaji.Serikali zimeahidi kuepuka kushusha thamani ya sarafu zao ili kuongeza usafirishaji nje wa bidhaa zao.Zimetowa wito wa kuwepo kwa ushirikiano wa kupunguza ukwepaji kodi na pia kuongeza misaada kwa ajili ya ongezeko la wakimbizi na nchi wanakotokea.

Hasira dhidi ya biashara huru

Viongozi hao wa kundi la G20 pia wameazimia kupambana na ghadhabu za wanaharakati wanaopinga biashara ya dunia kwa kunadi faida za biashara hiyo ikiwemo ya kuwatowa katika umaskini mamilioni ya watu.

Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Christine Lagarde.
Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Christine Lagarde.Picha: picture-alliance/AP Photo/R. Abd

Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa Christine Lagarde akifafanuwa suala hilo katika mkutano wake na waandishi wa habari amesema"Kulikuwa na muafaka juu ya mambo mawili kwamba lazima kuwepo na ukuaji zaidi wa uchumi na ukuaji huo lazima uwe shirikishi.Pia kulikuwa na azma ya kutambuwa vizuri zaidi faida za biashara hiyo na zipi ni chanya ili kujibu ghadhabu za wanaharakati wanaopinga ukuaji huo wa uchumi na utandawazi."

Viongozi wa China wanataraji mkutano huo wa siku mbili utaongeza ushawishi wa nchi hiyo katika suala la kusimamia uchumi wa dunia.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/dpa

Mhariri : Josephat Charo