1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G8 leo.

Halima Nyanza25 Juni 2010

Viongozi wa mataifa duniani katika kundi la nchi za G8 wanakutana leo kuzungumzia masuala ya usalama duniani na maendeleo, pamoja na kujadili namna ya kuupiga jeki uchumi unaolega lega.

https://p.dw.com/p/O2u8
Mkutano wa viongozi wa nchi za G-8 na G-20, unaanza leo, nchini Canada.Picha: picture-alliance/dpa

Chini ya ulinzi mkali, viongozi kutoka katika kundi la mataifa manane tajiri duniani wanakutana leo katika mji wa Muskoka ulioko kilomita 220 kaskazini mwa Toronto.

Awali akizungumzia katika mkutano huo wa leo, Waziri Mkuu wa Canada Stephen Harper alisema viongozi wa mataifa hayo manane tajiri wataungana pamoja katika mkutano huo kuchukua hatua dhidi ya baadhi ya matatizo makubwa yanayoikabili dunia na hatimaye kupata matokeo.

Mkutano huo utaanza kwa viongozi kuanza kukutana katika mkutano wa ndani, kujadiliana masuala ya uchumi duniani.

Kauli mbiu ya mkutano huo wa leo ni ''kukua kwa uchumi na kuwa na imani na jambo hilko.

Kulingana na kauli mbiu hiyo, Waziri wa Fedha wa Marekani  Tim Geithner amesema kazi yao ni kuhakikisha kwamba wanakutana pamoja kuelekeza juhudi kukabiliana na suala la kukua kwa uchuni na kuwa na imani katika hilo kwa sababu kukua kwa uchumi na kujiamini ni mambo yaliyo muhimu kabisa.

Kwa upande wake, akizungumza kabla ya kuanza kwa mkutano huo, unaoangalia pia utekelezwaji wa ahadi zilizotolewa katika vikao vilivyopita, kansela wa Ujerumani ana mtazamo mwingine ameonesha kutoridhishwa na hali baada ya ahadi zilizotolewa.

Amesema bado hawajaridhika na hali ilivyo tangu mkutano wa kwanza wa G 20 ulipofanyika. na kwamba wanahisi kwamba marekerbisho yanapaswa kuharakishwa.

Katika mkutano wa leo, viongozi wa mataifa sita ya Afrika wanaungana na wakuu wa nchi za  kundi la G8 katika mazungumzo yatakayolenga kulisaidia bara la Afrika kupambana na ugaidi pamoja na kufanikisha kutimiza malengo ya milenia ya kupambana na umasikini.

Akizungumzia kuhusiana na ushiriki wa viongozi hao, Rais wa Umoja wa Ulaya, Herman Van Rompuy, amesema uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika ni kipaumbele chao na kwamba wanasisitiza zaidi juu ya ahadi ya Umoja wa Ulaya  katika masuala ya amani na usalama barani Afrika.

Mkutano huo wa leo unafanyika pia wakati ambapo nchi za Umoja wa Ulaya ziko katika shinikizo la kupunguza bajeti zake, tangu kutokea kwa mzozo wa madeni wa Ugiriki, kutokana na kwamba athari za tatizo kama hilo zinaweza pia kutokea katika nchi nyingine za Ulaya zinazotumia sarafu ya Euro.

Katika mkutano huo itakuwa pia ni mara ya kwanza kwa Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, kuhudhuria katika mkutano mkubwa kama huo tangu aliposhika madaraka mwezi uliopita.

Baada ya mkutano wa leo, siku ya kesho na kesho kutwa  kundi jiingine la mataifa yaliyoendelea na yanayoinukia kiuchumi -G20- yataungana pia katika mkutano huo, huku kukiwa na ulinzi mkali ambapo takriban polisi 20,000 wametawanywa katika eneo hilo

Kundi la G8 linaundwa na nchi za Ujerumani, Marekani, Uingereza Ufaransa, Japan, Italy, Canada na Urusi.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp)

Mhariri: Miraji Othman