1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano juu ya mazingira.

Abdu Said Mtullya17 Septemba 2009

Wachafuzi wakubwa wa mazingira wakutana Washington.

https://p.dw.com/p/Jipv
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- Moon katika kampeni ya kusisitiza ulazima wa kulinda mazingira.Picha: AP PHoto/Mark Garten/UN

Wajumbe kutoka nchi 17 zinazoongoza kwa uchafuzi wa mazingira duniani wanakutana Washington kujadili tishio la mabadiliko ya hali ya hewa.

Lengo la mkutano huo ni kujaribu kuondoa tofauti baina ya nchi hizo 17 kabla ya mkutano wa Umoja wa Mataifa juu ya mabadiliko ya hali ya hewa utakaofanyika mjini Copenhagen katika mwezi wa desemba.

Wajumbe hao kwanza wanakutana kwa muda wa siku mbili kwenye wizara ya mambo ya nje ya Marekani kabla ya kuhamia New York wiki ijayo.

Wajumbe hao wanajadili njia za kuendeleza harakati za matayarisho ya mkutano huo wa mjini Copenhagen unaotarajiwa kupitisha mkataba kamambe juu ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Mkutano huo unafanyika wakati ambapo Marekani inajaribu kurudi tena katika dhima ya kuongoza juhudi za kupamabana na tishio la mabadiliko ya hali ya hewa na wakati ambapo katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameonya dhidi ya sera na nyendo zinazoweza kuwatosa binadamu katika maafa makubwa.

Katibu Mkuu Ban Ki Moon amesema kuwa mguu wa mwanadamu bado umekanyaga pedeli ya sera nyendo hizo.

Katibu Mkuu huyo ameliambia gazeti la Guardian la Uingereza kuwa ana wasiwasi mkubwa kutokana na kutosonga mbele kwa mazungumzo juu ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Amesema ni muhimu sana kwa viongozi kuonyesha dhamira ya kisiasa na kutoa mwongozo kwa wawakilshi wao kwenye mazungumzo.

Mkutano wa mjini Washington unahudhuriwa pia na wajumbe kutoka Umoja wa Ulaya, Ufaransa, Italia, Ujerumani na Uingereza.

Kuna habari kwamba nchi za Ulaya zimekwaruzana na Marekani juu ya viwango vya kupunguza gesi zinazoharibu mazingira na jinsi ya kukabiliana na tishio la kuongezeka kwa joto duniani.

Kufanyika kwa mkutano huo kwenye wizara ya mambo ya nje ya Marekani kunadhihirisha mabadiliko katika msimamo wa Marekani juu ya suala la ulinzi wa mazingira tokea rais Barack Obama aingie madarakani.

Mapema mwezi machi rais Obama alizindua baraza la nchi zenye nguvu kubwa za kiuchumi ili kushughulikia masuala ya nishati na ya hali ya hewa.

Rais wa hapo awali G. W. Bush alikataa kuidhinisha rasimu ya Kyoto juu ya ulinzi wa mazingira.

Mwandishi: Abdul Mtullya /Reuters

Mhariri:M.Abdul-Rahman