1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Iraq na majirani zake

9 Machi 2007

Kuna siri kubwa inayozunguka mkutano wa wa kimataifa juu ya Iraq ambao unaanza leo mjini Baghdad, na hiyo inadhihirisha ukubwa wa mzozo ambao watakaoshiriki kwenye mkutano huo wanatakiwa wautanzuwe.

https://p.dw.com/p/CB5L
Waziri wa mambo ya kigeni wa Iraq, Hoschajar Zebari , akihojiwa na Radio Deutsche Welle, mjini Berlin, Ujerumani.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Iraq, Hoschajar Zebari , akihojiwa na Radio Deutsche Welle, mjini Berlin, Ujerumani.Picha: DW

Viongozi wa Iraq wamenyamaa kimpya wapi mkutano huo utafanyika na wakati gani utaanza ili kuepusha kutokea mashambulio. Pia maslahi ya nchi zinazoshiriki yanatafautiana kabisa, kwa hivyo hakutazamiwi kutakuweko makubaliano zaidi ya tu kusema kwamba michafuko izuiliwe kutokea.

Kumekuweko na tetesi za hapa na pale kama wanadiplomasia wa Iran na Marekani watakuwa na mazungumzo ya ana kwa ana pembezoni mwa mkutano huo ulio na lengo la kuzifanya nchi zilizo jirani na Iraq zijishughulishe zaidi kuleta utulivu katika nchi hiyo ilivurugika kwa michafuko.

Ikiwa ni badiliko la msimamo, maafisa wa Kimarekani walisema jana kwamba wako tayari kufanya mazungumzo na Iran na pia na Syria, hasimu mwengine wa Marekani katika eneo hilo la Mashariki ya Kati. Marekani inazituhumu Iran na Syria kwamba zinachangia katika michafuko inayoendelea sasa huko Iraq. Mratibu katika wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, David Satterfield, alisema ikiwa wataalikwa na Wa-Syria au Wa-Irani wanywe maji ya matunda pamoja na kuzungumzia masuala yanayoihusu Iraq, basi wao hawatakataa. Lakini alisema harakati za Iran za kujipatia nishati ya kinyukliya hazitakuwemo katika ajenda ya mazungumzo hayo.

Iran imesisitiza kwamba haitazamiwi kuweko mazungumzo baina yake na Marekani, na imemtuma makamo wa waziri wa mambo ya kigeni, Abbas Araqchi, katika mkutano huo. Bwana Araqchi alisema mkutano wa Baghdad utakuwa ni mtihani wa kuzipima siasa za Marekani na kuona kama Wamarekani kweli wanataka kutafuta suluhisho au wanataka kuendelea na siasa zao za ubabe. Mara kadhaa Iran imeyakana madai ya Marekani kwamba inajiingiza katika mambo ya ndani ya Iraq, ikiwa ni pamoja na madai ya Rais Bush kwamba jamhuri hiyo ya Kiislamu inawapa silaha waasi wa Kishia wapambane na majeshi ya Kimarekani. Iran inadai kwamba Marekani na Uengereza zinafanya njama za kuleta mtafaruku baina ya Waislamu wa madhehebu ya Sunni na Shia huko Iraq ili kusaidia kuiimarisha Israel. Wa-Irani wanasema wako tayari kushirikiana na Marekani katika kuyatuliza mambo nchini Iraq, pindi, lakini, Marekani, nayo iondoshe majeshi yake kutoka Iraq.

Wanadiplomasia kutoka nchi zilizo jirani na Iraq, Misri na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanatazamiwa kuhudhuria mkutano wa leo wa Baghdad. Mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi hizo watakutana mwezi ujao wa April nje ya Iraq.

Ilivokuwa ule muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani unasambaratika huko Iraq, watawala wa Washington wanatafuta washirika zaidi kusaidia kuidhibiti Iraq ili majeshi ya Kimarekani yaweze kurejea nyumbani. Iran na Syria zinataka kujikosha na yale madai kwamba kwa kuyaunga mkono makundi yenye siasa kali, nchi hizo zinachangia katika michafuko na mauaji inayofanyika katika nchi jirani ya Iraq. Serekali ya Iraq, ambayo inadhibitiwa sana na Washia na Wa-Kurd, inatarajiwa kupatiwa misaada ya kifedha na kufutiliwa mbali madeni yake. Jambo zaidi linaloleta mashaka ni kwamba muungano wa Kishia wa waziri mkuu Nuri al-Maliki unayategemea majeshi ya Kimarekani na mafungamano yake na Iran ili kubakia madarakani.

Vyama vya Kisunni na washirika wao huko Saudi Arabia, Misri na Jordan vinauuangalia mkutano huu uweze kuengeza mbinyo juu ya Washia ili wazuwie mauaji yanayofanywa na wanamgambo wa Kishia dhidi ya Wasunni walio wachache.

Wakati huo huo, kamanda wa majeshi ya Kimarekani katika Iraq, Jenerali David Petraeus, amesema kwamba operesheni za kaijeshi peke yake dhidi ya michafuko ya kimadhehebu katika Iraq hazitoshi. Alisema harakati za kijeshi ni za lazima kusaidia kuboresha usalama. Kwa mujibu wake yeye, maendeleo ya kisiasa yatahitaji kuweko mazungumzo na maafikiano na wale wanaohisi kwamba Iraq mpya haina nafasi kwa ajili yao.

Pia jana wajumbe wa Chama cha Democratic katika Baraza la wawakilishi la Bunge la Iraq walitaka majeshi ya Kimarekani yaondoke Iraq kuanzia Mwezi Machi mwakani. Ikulu ya Marekani ilisema Rais Bush ataupinga mswaada wowote wa sheria unatoaka majeshi ya Marekani yaondoke kwa haraka Iraq na iliwatuhumu viongozi wa Chamna cha Democratic katika bungekwamba wanajiingiza katika mkakati wa kijeshi ili kujipatia faida za kisiasa.