1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa jumuia ya nchi za kiarabu wamalizika Doha

Oumilkher Hamidou31 Machi 2009

Viongozi wa nchi za kiarabu watanguliza mbele suluhu kati yao

https://p.dw.com/p/HNSv
Kiongozi wa Libya Muammar GaddafiPicha: AP

Viongozi wa jumuia ya nchi za kiarabu waliokutana jana mjini Doha nchini Qatar,wamemuunga mkono kiongozi mwenzao wa Sudan Omar Hassan al Bachir dhidi ya amri ya korti kuu ya kimataifa ya uhalifu ya kutaka akamatwe kwa tuhuma za kuhusika na uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya ubinaadam.


"Tunathibitisha mshikamano wetu pamoja na Sudan pamoja na kupinga hatua ya korti kuu ya kimataifa dhidi ya rais Bashir" wamesema hayo viongozi wa jumuia ya nchi za kiarabu katika taarifa yao ya mwisho iliyotangazwa jana usiku mjini Doha nchini Qatar.Mwenyewe rais Omar Hassan al Bashir aliyepuuza amri ya korti kuu ya kimataifa ya uhalifu wa vita kwa kufika ziarani nchini Misri,Eritrea na nchini Libya kabla ya kuhudhuria mkutano huu wa kilele wa Doha,amewashukuru viongozi wenzake na kusema

"Ndugu zangu wapendwa,tunathamini msaada wenu kwa Sudan.Msaada huu,Mungu akipenda,utaendelea.Mmepitisha uamuzi bayana na wa nguvu kwa kupinga nisikamatwe na kutaka amri hiyo ibatilishwe."


Hata kama Qatar imelifanya suala la suluhu likamate nafasi ya mbele katika ajenda ya mkutano,hata hivyo maajabu makubwa yalizuka, Tripoli na Ryadh zilipojongeleana.Kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi na mfalme Abdallah wa Saud Arabia wameamua kuwachilia mbali mvutano wao unaoendelea tangu miaka sita iliyopita.


Gaddafi alikatiza kikao cha ufunguzi na kutoa hotuba ambayo awali watu walifikiri imelengwa dhidi ya Saud Arabia.


Alimaliza hotuba hiyo hata hivyo kwa kushangiriwa aliposema anauangalia mvutano wao wa mwaka 2003 kua ni tukio lililopita.Mfalme Abdallah wa Saud Arabia na kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi walikutana baadae kwa zaidi ya nusu saa.


Na ikaamuliwa mkutano ujao wa kilele wa jumuia ya nchi za kiarabu utafanyika Libya.


Kuhusu ugonvi kati ya Israel na wapalastina,rais Bashar el Assad wa Syria amesema "amani kati ya Israel na nchi za kiarabu haitopatikana bila ya nia njema ya Israel."Rais huyo wa Syria anahisi hujuma za kijeshi za Israel dhidi ya Gaza,january mwaka huu zimeutia ila mpango wa amani wa mwaka 2002 ulioshauriwa na nchi za kiarabu .


Akipania kuimarisha mshikamano thabiti kati ya nchi za kiarabu,mfalme Abdallah wa Saud Arabia amefunga safari hadi Doha kuhudhuria mkutano huo wa kilele uliosusiwa lakini na rais Hosni Mubarak na viongozi wenzake wengine wanne.