1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa jumuiya ya kiarabu wamalizika

Charo, Josephat31 Machi 2008

Suluhisho la mzozo wa Lebanon halikupatikana

https://p.dw.com/p/DXb7
Rais wa Syria Bashar al Assad (kushoto) na kiongozi wa Libya Muammar GaddafiPicha: picture-alliance/ dpa

Mkutano wa jumuiya ya nchi za kiarabu ulimalizika jana mjini Damascus nchini Syria. Maswala yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo ni mzozo nchini Lebanon, mdahalo na maridhaino nchini Irak na katika maeneo ya Wapalestina pamoja na pendekezo la amani kwa Israel.

Mgogoro nchini Lebanon uliamua mkondo wa mkutano wa mjini Damascus tangia mwanzo. Mzozo huo ulitakiwa kuwa mada ya mkutano wa siku mbili wa jumuiya ya nchi za kiarabu na ilikuwa hivyo licha ya viongozi wengi wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo kuugomea mkutano wa mjini Damascus kwa sababu ya mgogoro huo wa Lebanon na badala yake kuwatuma wanadiplomasia kuwawakilisha kwenye mkutano huo.

Mkutano wagomewa

Viongozi wa Jordan, Misri na Saudi Arabia hawakuhudhiria mkutano wa Damascus wakiilaumu Syria kwa kuingilia siasa za ndani za Lebanon na kuzuia uchaguzi wa rais mpya wa taifa hilo na kutaka kuanzisha tena mamlaka yake nchini humo.

Nusu ya viongozi wa jumuiya ya nchi za kiarabu yenye wanachama 22, wakiwemo viongozi wa Saudi Arabia, Misri na Jordan, waliugomea mkutano wa mjini Damascus,wakiilaumu Syria kwa kuusababisha mzozo wa Lebanon. Marekani iliwahimiza washirika wake wafikirie mara mbili kabla kuhudhuria mkutano huo huku ikiilumu Syria kwa kuzuia uchaguzi wa rais nchini Lebanon.

Lakini rais wa Syria, Bashar al Assad, amekanusha madai ya kuingilia mambo ya ndani ya Lebanon katika hotuba yake ya ufunguzi Jumamosi iliyopita.

"Sisi hapa Syria tuko tayari kujitolea kwa dhati na kikamilifu katika mipango ya kiarabu na isiyo ya kiarabu kwa sharti kwamba kila mpango unazingatia maslahi ya Lebanon. Lengo letu kubwa ni uthabiti."

Rais wa Libya, Muammar Gaddafi amesema, "Hakuna kipya cha kutangaza katika mkutano huu wa kilele. Ni kama mikutano mingine iliyopita ya jumuiya ya nchi za kiarabu," Aidha kiongozi huyo amesema la muhimu zaidi lililojitokeza kwenye mkutano wa Damascus ni kutambuliwa kwa kiwango fulani migawanyiko, matatizo na chuki kati ya nchi za kiarabu.

Taarifa ya pamoja

Taarifa ya mkutano wa Damascus iliyosomwa na kiongozi wa jumuiya ya nchi za kiarabu, Amr Mussa, mwishoni mwa mkutano huo, imeitolea mwito Lebanon ichague rais na iidhinishe tena mpango wa amani na Israel.

Viongozi wa kiarabu pia wameishawishi Irak kuyavunja makundi yote ya wapiganaji pasipo kubakisha hata moja na iharakishe kuundwa na kupewa mafunzo vikosi vya jeshi na usalama ili kujiandaa kwa kuondoka kwa wanajeshi wa kigeni kutoka Irak.

Viongozi pia wamezitaka nchi za kiarabu kuongeza uwakilishi wao wa kidiplomasia nchini Irak kwa kufungua balozi katika nchi hiyo inayokabiliwa na vita.

Kuhusu mgogoro wa Lebanon, viongozi wa kiarabu wamesisitiza kujitolea kwao kwa mpango wa amani wa waarabu kuutanzua mgogoro huo na kuwatolea mwito viongozi wa Lebanon wamchague jenerali Michel Sleiman kuwa rais wakati utakaokubalika.

Pia wametaka uhusiano kati ya Lebanon na Syria, ambao umekuwa ukiyumba, uboreshwe. Wanasiasa wanaohasimiana wa Lebanon wanatakiwa waamue juu ya msingi wa kuunda baraza la mawaziri la umoja wa taifa, kwa mujibu wa mpango wa amani wa jumuiya ya kiarabu unaolenga kumaliza mzozo mbaya wa kisiasa kuwahi kutokea nchini Lebanon tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka wa 1975 na 1990.

Amr Mussa anasema ipo haja ya pande zote kuungana nchini Lebanon. "Pande zote husika nchini Lebanon zinatakiwa zihimizwe ziungane ili mgororo huu utatuliwe na usalama, uthabiti na utawala vilindwe."

Libanon Wahlen Präsident Ministerpräsident Saniora und Moussa
Katibu mkuu wa jumuiya ya nchi za kiarabu Amr Moussa (kulia) akizungumza na rais wa zamani wa Lebanon Emile LahoudPicha: AP

Lebanon imekuwa bila rais tangu mwezi Novemba mwaka jana wakati rais Emile Lahoud aliyeegemea Syria, alipomaliza awamu yake kukiwa na mkwamo kati ya serikali inayoungwa mkono na nchi za magharibi na upinzani unaoongozwa na Hezbollah unaoungwa mkono na Syria na Iran.

Kiongozi wa ujumbe wa Saudi Arabia katika mkutano wa mjini Damascus, Ahmed Qattan, ameushutumu upinzani nchini Lebanon kwa kutaka kudhibiti taasisi zote za taifa. "Hakuna anayeweza kushuku jukumu la Saudi Arabia nchini Lebanon kujaribu kudumisha uthabiti na kuulinda uhuru wake," amesema kiongozi huyo.

Mpango wa amani na Israel

Viongozi wa jumuiya ya kiarabu wameidhinisha upya pendekezo kwa Israel kurejesha mahusiano ya kawaida kwa mabadilishano ya kuondoka maeneo yote iliyoyakalia wakati wa vita vya Mashariki ya Kati vya mwaka wa 1967.

Mkutano wa Damascus umesisitiza kutumiwa kwa mpango wa amani wa waarabu unaoweka misingi ya kumaliza tofauti mbalimbali za mzozo baina ya warabu na waisraeli. Mpango huo wa amani ulianzishwa kwenye mkutano wa kilele wa mjini Beirut mnamo mwaka wa 2002 na ukazinduliwa upya mjini Riyadh Saudi Arabia mnamo mwaka jana.

Kiongozi wa jumuiya ya kiarabu, Amr Mussa, anasema kufaulu kwa mpango huo kutategemea ikiwa Israel itayatimiza majukumu yake ya amani. "Kufaulu kwa jumuiya ya kiarabu kuhusu mpango wake wa amani kumefungamanishwa na Israel kutimiza majukumu yake inayotakiwa kulingana na maazimio ya kimataifa kuhusu amani katika eneo hilo."

Mkutano wa Damascus uliangazia kuongezeka kwa mkingamo kati ya Syria na washirika wa Marekani kama vile Misri na Saudi Arabia. Waziri wa mashauri ya kigeni wa Saudia, mwanamfalme Saud al Faisal, ameitaka Syria ichukue hatua za maana kuumaliza mkwamo nchini Lebanon.

Rais wa Misri, Hosni Mubarak, katika ujumbe wake amesema uliwengu wa nchi za kiarabu ulitumai kabla mkutano wa Damascus kwamba suluhisho la mzozo wa Lebanon lingepatikana.

Syria ikiuandaa mkutano wa jumuiya ya nchi za kiarabu kwa mara ya kwanza, ilisema kutokuhudhuria kwa washirika wa Marekani ni ushindi dhidi ya ushawishi wa serikali ya mjini Washington.

Syrien Außenminister Walid al-Muallim in Damasus zu Frankreich
Waziri wa mambo ya kigeni wa Syria Walid al-MuallemPicha: AP

Waziri wa mambo ya kigeni wa Syria, Walid al Mualem, amesema Syria itakuwa tayari wakati Marekani itakapoichukulia hatua ya kijeshi. "Mtu mwenye busara hujiandaa vizuri, hususan tukijua tunalazimika kupambanana na utawala unaojua kuvamia lakini usiojua jinsi ya kuondoka."