1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Jumuiya ya Madola kufanyika leo

Kabogo Grace Patricia27 Novemba 2009

Mkutano huo utajadili masuala yanayohusu hali ya hewa kabla ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa utakaofanyika Copenhagen, Denmark, mwezi ujao.

https://p.dw.com/p/KhYH
Malkia Elizabeth II wa Uingereza, ambaye pia ni mkuu wa Jumuiya ya Madola.Picha: AP

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa leo wanatarajia kuzungumzia mjadala juu ya hali ya hewa wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola, unaofanyika Trinidad na Tobago, kabla ya mkutano wa kilele wa hali ya hewa utakaofanyika Copenhagen, Denmark mwezi ujao. Viongozi wa mataifa 53 wanachama wa Jumuiya ya Madola wamewapa viongozi hao wawili ambao sio wanachama wa jumuiya hiyo fursa ya kipekee na adimu kuhutubia katika mkutano huo unaofanyika kwenye mji mkuu wa Trinidad na Tobago wa Port-of-Spain, kabla ya mkutano wa Umoja wa Mataifa wa hali ya hewa uliopangwa kufanyika kuanzia tarehe 7 hadi 18 Desemba mjini Copenhagen. Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza, mkuu wa Jumuiya ya Madola, anatarajiwa kufungua rasmi mkutano huo wa siku tatu kabla ya Bwana Ban, Rais Sarkozy na mjumbe mwingine ambaye sio mwanachama wa umoja huo, Waziri Mkuu wa Denmark, Lars Loekke Rasmussen, hawajazungumza.

Jumuiya hiyo na mataifa yanayoendelea

Jumuiya hiyo inawawakilisha watu bilioni mbili, robo ya idadi yote ya watu duniani na inafanya kazi kama mwakilishi katika kuzungumzia misimamo tofauti baina ya mataifa yaliyoendelea na yale yanayoendelea kuwakilishwa katika mkutano wa Copenhagen. Mataifa yaliyoendelea kiviwanda na kisiasa kama vile Uingereza, India, Australia, Afrika Kusini na Canada yatakuwa pamoja na mataifa kama vile Vanuatu, Tuvalu na Lesotho, ambayo mawazo yao mara nyingi yamekuwa yakipuuzwa katika ngazi ya kimataifa, lakini yamekuwa yakiathiriwa kutokana na ongezeko la ujoto duniani. Msemaji wa Jumuiya ya Madola, Eduardo del Buey, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa jumuiya hiyo inaziruhusu nchi ndogo duniani kuwa na sauti. Waziri Mkuu wa Trinidad na Tobago, Patrick Manning jana alisema kuwa Bwana Ban, Rais Sarkozy na Rasmussen wamealikwa kuhudhuria mkutano huo huku kukiwa na wasi wasi kuhusu jinsi majadiliano yanavyoendelea kabla ya mkutano wa Copenhagen. Manning amesema kulikuwa pia na mpango wa kumualika Rais Barack Obama, lakini suala hilo halikufikia popote.

Umuhimu wa mkutano wa Copenhagen

Wiki chache zilizopita mkutano wa Copenhagen umeonakana kuwa muhimu kutokana na kufikiwa kwa mkataba mpya wa kupunguza matumizi ya gesi zinazochafua mazingira utakaochukua nafasi ya Mkataba wa Kyoto. Lakini wiki hii Rais Obama alitangaza atahudhuria mkutano wa Copenhagen na kuahidi kupunguza matumizi ya gesi zinazoharibu mazingira kwa asilimia 17 ifikapo mwaka 2020. China nayo imeahidi itapunguza kwa asilimia 40 hadi 45 ifikapo mwaka 2020. China na Marekani ni mataifa yanayoongoza kwa kutumia gesi zinazoharibu mazingira hivyo taarifa hizo zinaonekana kuwa muhimu katika kufikiwa kwa mkataba wa Kyoto. Rais Sarkozy na Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil, wamesema watayashinikiza nchi tajiri kuzilipa nchi zinazoendelea ili kulinda mazingira yao na kuyainua kiuchumi kutokana na athari zilizotokana na matumizi ya gesi hizo. Brazil nayo imeahidi kupunguza matumizi ya gesi zinazoharibu mazingira kwa asilimia 36 hadi 39 ifikapo mwaka 2020.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)

Mhariri: Aboubakary Liongo