1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa jumuiya ya SADC wamalizika leo Windhoek

17 Agosti 2010

Kikao cha kilele cha marais wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya SADC kimeingia mkondo wa mwisho mjini Windhoek nchini Namibia

https://p.dw.com/p/Opg1
Waziri mkuu wa Zimbabwe, Morgan Tsvangirai, kushoto, na rais wa nchi hiyo, Robert MugabePicha: AP

Ajenda ya kikao hicho ilikuwa kuzijadili mbinu za kuuimarisha ushirikiano wa kiuchumi pamoja na masuala ya kisiasa yanayozitatiza nchi za Madagascar na Zimbabwe. Jumuiya ya SADC iliyo na nchi 15 wanachama iliasisiwa miaka 30 iliyopita.

Kikao hicho cha siku mbili kiliwaleta pamoja marais wa mataifa 15 wanachama wa Jumuiya ya SADC. Mada kuu zilizojadiliwa ni pamoja na masuala ya kuuimarisha uchumi wa kikanda na masuala tete ya siasa yanayozikabili nchi za Zimbabwe na Madagascar. Hii leo kikao hicho kililijadili suala la Zimbabwe ambayo imekataa kuyatimiza maagizo ya mahakama ya Jumuiya ya SADC. Mahakama hiyo iliamuru kuwa wakulima 78 wa kizungu wana haki ya kuendelea kuyamiliki mashamba yao kwani walipokonywa kwa misingi ya ubaguzi wa rangi. Itakumbukwa kuwa mwaka 2008, serikali ya Zimbabwe ilianzisha mfumo uliozua mitazamo tofauti wa kuwapokonya wakulima wa kizungu mashamba yao. Mabadiliko hayo ya sheria ya umiliki wa ardhi hayakuungwa mkono na wengi.  

Zimbabwe inakataa katakata kuuheshimu uamuzi huo wa mahakama ya SADC ijapokuwa imeuidhinisha mkataba ulikizindua chombo hicho cha sheria. Ifahamike kuwa mahakama hiyo ina mamlaka ya kuilazimisha nchi kuyatimiza maamuzi yake katika vikao vya Jumuiya hiyo ya SADC pekee. Kulingana na mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Chuo Kikuu cha Afrika Kusini, Dirk Kotze, hakuna uwezekano wowote wa kuiadhibu Zimbabwe kwa njia yoyote ile kwa mfano kuiwekea vikwazo. Hatua kali zaidi Jumuiya hiyo inayoweza kuchukua ni kueleza kuwa imevunjwa moyo na uamuzi wa kutoyatii maagizo ya mahakama hiyo ya kikanda. Suala la msingi katika hali hiyo ni kudumisha umoja katika serikali husika. 

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe aliye na umri wa miaka 86 na ambaye amekuwa madarakani kwa miongo mitatu aliunda serikali ya Umoja wa kitaifa mwaka uliopita akishirikiana na kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai wa chama  cha Movement For Democratic Change, MDC aliye Waziri Mkuu kwa sasa. Mwaka 2000, kiasi ya wakulima alfu 4 walilazimika kuyakimbia mashamba yao katika kampeni iliyokuwa na vurugu iliyoanzishwa na Rais Mugabe.

Kwa sasa kiasi ya wakulima 400 Wazungu bado wako Zimbabwe na hali ya kiuchumi ni mbaya baada ya mabadiliko hayo kukifanya kilimo kuvurugika jambo linaloifanya nchi hiyo kuitegemea misaada ya nje.   

Kwa upande wake Zimbabwe inashikilia kuwa makubaliano hayo ya kuianzisha mahakama ya SADC kamwe hayakuthibitishwa baada ya kuidhinishwa. Kulingana na wakosoaji, saini iliyoko kwenye mkataba huo inatosha. Viongozi hao wanatarajiwa kulijadili suala hilo katika kikao kijacho kilichopangwa kufanyika mwakani.

Mwandishi:Thelma mwadzaya-AFP

Mhariri:Josephat Charo