1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Kamati Kuu ya ZANU-PF wafanyika bila Mugabe

Florence Majani15 Desemba 2017

Kamati Kuu ya chama cha Zanu-PF  nchini Zimbabwe  leo inakutana kwa mara ya kwanza tangu Rais wa zamani Robert Mugabe aondoke madarakani. Rais mpya Emmerson Mnangagwa atahutubia katika mkutano unaofanyika Harare.

https://p.dw.com/p/2pQRY
Simbabwe  Emmerson Mnangagwa
Rais mpya wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa akizungumza na wananchi katika ofisi za ZANU-PF Novemba 22 mwaka huu.Picha: Getty Images/M.Longari

Rais mpya wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa anatarajia kuhutubia mkutano huo wa siku moja  na wa kipekee,  mjini Harare leo.Pamoja na mambo mengine, anatarajia kutumia mkutano huo wa chama tawala cha ZANU-PF, kuimarisha nguvu zake madarakani, baada ya Mugabe, kuondolewa  mwezi uliopita.

 Tayari Mnangagwa ameshaapishwa kama rais mpya wa Zimbabwe, na kiongozi mkuu wa chama hicho tawala akichukua nafasi ya Mugabe, ambaye ameongoza chama hicho tangua mwaka 1975 na kuongoza nchi hiyo tangu ipate uhuru mwaka 1980.

Mkutano Mkuu wa Zanu-PF ni hatua ya mwisho  ya Mugabe kupoteza umashuhuri wake baada ya jeshi kumuweka kizuizini nyumbani kwake. Wakati huo, mamia kwa maelfu ya wananchi waliandamana barabarani  huku watunga sheria wakijiandaa kumuondoa madarakani.

Robert Mugabe und Grace Mugabe
Mugabe na mke wake Grace Mugabe wakati wa utawala wake. Picha: Getty Images/J.Njikizana

Mugabe aliondoka madarakani akiwa na miaka 93

Kutokana na shinikizo kubwa, Mugabe, mwenye umri wa miaka 93, na aliyeapa  kutawala katika maisha yake yote, hatimaye alijiuzulu.Wakati akiapishwa, Mnangagwa, alimuelezea Mugabe kama baba, komredi katika jeshi na kiongozi.

Akizungumza jana katika vikao vya awali vya mkutano huo, Mnangagwa aliyaomba mataifa ya magharibi kuondoa vizuizi ilivyoiwekea nchi hiyo  ili kurahisisha uwekezaji wa nje.  Pia aliahidi kulifanya taifa hilo  kuwa sehemu ambayo rasilimali zipo salama.

"Ili kusonga mbele tunaomba kuondolewa kwa vizuizi visivyo na masharti vya kiuchumi na kisiasa, ambayo vimezorotesha maendeleo ya taifa.  Tumegundua kuwa kutengwa si kuzuri wala si uhai kwa sababu kuna mengi ya kunufaika kutokana na mshikamano na manufaa ya ushirkiano ambao utatusaidia kujua maslah yetu ya kipekee ya taifa."alisema Mnangagwa

Msemaji wa chama  cha ZANU-PF Simon Khaya Moyo, amesema uamuzi wa kumuondoa Mugabe kama kiongozi wa chama ulifanywa na kamati kuu, na  ni uamuzi ambao wajumbe watauidhinisha leo.

Moyo amesema  katika mkutano huo, ZANU-PF pia inatarajiwa kumuidhinisha Mnangagwa kuwa kiongozi wa chama hicho na mgombea halali wa urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Anatarajia pia kutumia mkutano huo kuteua wasaidizi wake wawili lakini Moyo amesema  anaweza asitangaze uteuzi huo huo leo. Amesema  ni hiari ya Rais  kutangaza uteuzi wa wasaidizi wake katika mkutano mkuu au asitangaze.

Kadhalika Moyo amesema chama kina  mfumo mpya na kimsingi jambo kubwa katika ajenda hiyo ni kuwa Rais mpya  ataidhinishwa kuwa rais wa chama na mgombea wa urais katika uchaguzi wa 2018.

Mugabe hatakuwepo katika mkutano huo. Inaelezwa kuwa amekwenda Malaysia na Singapore, mapema wiki hii, kuitembelea familia yake na kupata matibabu. Hii ni safari yake ya kwanza ya nje ya nchi, tangu tukio la kujiuzulu kwake mwezi uliopita.

 Mwandishi: Florence Majani(Afp, Ap)

Mhariri: Yusuf Saumu