1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele kuhusu vyoo wafanyika New Delhi

Josephat Charo1 Novemba 2007

Wajumbe kutoka nchi 40 duniani kote wanahudhuria mkutano wa kilele kuhusu vyoo mjini New Delhi nchini India. Mada mbiu ya mkutano huo ni ´Vyoo kwa Wote´.

https://p.dw.com/p/C7rT
Mwanamke akisafisha vyoo
Mwanamke akisafisha vyooPicha: dpa

Wanasiasa na wataalamu wanakutana kwa siku nne mjini New Delhi India kujadiliana kuhusu njia za kuboresha usafi kwa kutumia vyoo. Kwa mujibu wa shirika la afya duniani, WHO, watu takriban bilioni 2.6 au thuluthi moja ya idadi ya wakaazi wote dunaini, hawana vyoo. Wataalamu wanasema zaidi ya nusu ya idadi hiyo wanaishi nchini India au China, huku India ikiwa na watu takriban milioni 700 katika idadi hiyo.

Dr Nath kutoka India anasema uhaba wa vyoo ni tatizo la dunia nzima.

´Ni tatizo kubwa duniani kote na pia katika nchi zinazoendelea kwa sababu njia salama ya kutupa kinyesi cha binadamu itakuokoa kutokana na magonjwa mengi yakiwemo ungonjwa wa kupooza, kipindupindu, maumivu ya tumbo yanayotokana na minyoo na hata kifo.´

Daktari Nath ni mwanachama wa shirika la kimataifa la Sulabh, shirika la kihindi lililouandaa mkutano wa mjini New Delhi. Yeye amekuwa akijishughulisha na vyoo vya kitamaduni nchini India vinavyouzwa kwa bei ya kuanzia dola 18, mifumo ya kusafisha maji ya kunywa na usafi katika maeneo ya mashambani.

Damodar Bhartia mshauri katika shirika la Sulabh anasema tatizo la vyoo ni la kuzingatiwa kwa makini. Amesema, ´Maafisa wa serikali na wataalamu walio madarakani wameamua kuyamaliza matatizo ya vyoo. Kwa miongo mitatu sasa hawana tena matatizo ya vyoo.´

Bhartia anasema watu wanazunguzia maji, chakula kupambana na baa la njaa, lakini hata vyoo ni jambo dogo lililo muhimu kwa ukuaji wa kiuchumi. Kandoni mwa mkutano wa mjini New Delhi watengenezaji wa vyoo wanaonyesha bidhaa zao.

´Choo hiki ni cha mtu wa kawaida. Kimewekewa dawa ya kuua bakteria wanaosababisha homa ya mafua, SARS na magonjwa mengine yanayosababishwa na virusi.´

Mfanyabiashara mwingine wa India, Rajeev Kher, anapongeza ushirikiano kati ya India na Ujerumani katika utengenezaji wa vyoo.

´Kwa karibu miaka minne au mitano nimekuwa nikifanya kazi na bwana Peter Fliegenschmidt. Yeye ni fundi wa kutengeneza vyoo kutoka eneo la Sachsen – Anhalt nchini Ujerumani.´

India inalenga kuangamiza tabia ya watu kwenda haja kubwa katika misuti au maeneo mengine mbali na vyoo kufikia mwaka wa 2012 kwa kujenga vyoo kwa mamilioni ya raia wake wake wanaokabiliwa na umaskini uliokithiri na ambao hawana nyumba za kulala.

Waziri wa maendeleo ya maeneo ya mashambani wa India, Raghuvansh Prasad, amesema India itakuwa huru kutokana na tabia hiyo kufikia mwaka wa 2012 na itatimiza majukumu yake ya kimataifa kuhusiana na swala hilo. Waziri huyo ameyasema hayo jana kwenye mkutano wa kimataifa kuhusu vyoo unaoendelea mjini New Delhi.

Wataalamu wa afya na usafi kutoka nchi 40 duniani wanahudhuria mkutano mjini New Delhi kutafuta njia za kusambaza vyoo kwa kila mtu na kujadili maswala mengine kuhusu usafi. Waziri Prasad amesema India imetenga takriban dola milioni 255 kugharamia miradi ya usafi katika maeneo ya mashambani mwaka huu. Kiwango hicho cha fedha kimeongezeka kwa asilimia 43 ikilinganishwa na kiwango kilichotumika mwaka jana.

Wataalamu wanasema watu takriban nusu milioni nchini India husafisha vyoo na kubeba kinyesi cha binadamu kutumia vichwa au mikokoteni kwenda kukitupa kwenye majaa ya takataka. Tabia hiyo imepigwa marufuku lakini imeenea sana kutokana na ukosefu wa nafasi nyingine za ajira na mifumo ya kupitishia maji taka.