1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa hali ya hewa duniani mjini Copenhagen

Miraji Othman16 Novemba 2009

Tamaa ni ndogo kwa mafanikio ya mkutano wa kilele wa Copenhagen

https://p.dw.com/p/KYPF
Makamo wa rais wa zamani wa Marekani na mshindi wa zawadi ya amani ya Nobel, Al Gore, akiuhutubia mkutano wa Umoja wa Mataifa juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa Duniani mwaka 2007 huko Nusa Dua, Bali, IndonesiaPicha: AP

Mawaziri wa mazingira kutoka nchi muhimu 44 walikutana leo kwa ajili ya mkutano wa faragha wa siku mbili kwa lengo la kuzuwia aibu ya kutofaulu mkutano wa mwezi ujao wa Umoja wa Mataifa kuhusu ujoto duniani. Wajumbe wa mkutano huo ni pamoja na wale wa kutoka nchi zenye kutoa uchafuzi mkubwa wa hali ya hewa kutokana na moshi wa magari na viwanda vyao, zikiweko China, Marekani, India na Brazil, pamoja na mataifa kadhaa ya visiwa na nchi za Kiafrika ambazo ni miongoni mwa zile zilizo maskini kabisa duniani na wepesi wa kuadhirika na mabadiliko ya hali ya hewa duniani.

Mkutano wa Disemba saba hadi nane unakusudia kufikia makubalinao yatakayoanza kufanya kazi baada ya mwaka 2012 na yatakayotaka kupunguza moshi na athari za uwezekano wa kutokea ukame, mafuriko na vima vya maji baharini kupanda juu- yote yanasababishwa na mpagaranyiko wa mifumo ya hali ya hewa. Lakini baada ya miaka miwili ya mabishano, nchi wanachama 192 zilizotia saini Mkataba wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa duniani hazijafikia muwafaka. Waziri wa hali ya hewa wa Denmark, Connie Hedegarrd, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba watazungumzia masuala magumu yaliobaki, kama vile kugharimia miradi na yale malengo yakufikiwa. Alisema mkutano huo ni nafasi ya kwenda kwenye moyo wa mazungumzo hayo, ikiwa ni pamoja na masuala magumu, kwa vile hawana wakati mwingi uliobaki.

Lakini haikataliki kwamba, ikiwa wiki tatu kabla ya kufanyika mkutano huo wa kilele wa hali ya hewa duniani, sura yaonesha si ya kutia moyo. Rais Barack Obama wa Marekani na viongozi walioshiriki katika jukwaa la kilele la nchi za Amerika na zile zinazopakana na bahari ya Pasifik walisema hakuna lengo la kufikia mkataba wa lazima wa mapambano ya dunia dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa. Waziri mkuu wa New Zealand, John Key,alisema:

" Sasa kunatambuliwa hakutakuweko mkataba unaolazimisha, kisheria, na utakaotiwa saini Copenhagen. Haitafanyika, kabisa.... ukiwacha mbali baadhi ya miujiza. Na hamna mtu anayestabiri kutokea muujiza wa aina hiyo."

Nchi zinazoendelea zimezitaka nchi zenye uchumi tajiri kupunguza moshi zinazoingiza hewani kwa asilimia 40 ifikapo mwaka 2020, ukilinganisha na viwango vya mwaka 1990, na kutoa karibu moja asilimia ya ya mapato yao ya mwaka, karibu dola bilioni 400, kugharimia jambo hilo. Hadi sasa hamna nchi tajiri iliojitolea kulikaribia takwa kama hilo.

Kwa hivyo, nchi tajiri zinazishawishi nchi kubwa kama vile China, India na Brazil kushikilia ahadi zao za kushughulikia suala la moshi unaotoka kwenye viwanda na magari ya nchi zao.

Kwa mujibu wa duru za kibalozi ni kwamba waziri wa hali ya hewa wa Denmark atawasilisha pendekezo la kuweko maafikiano ya kisiasa ya lazima- mswada wa hati ya kurasa tano unataja ahadi ambazo sitasisitizwa hapo mwaka 2010, na zitafafanuliwa njia za kugawana mzigo wa kupunguza hewa hizo chafu. Nchi tajiri zitatambua ahadi zao za kupunguza moshi kwa kipindi cha muda wa wastani, ikimaanisha hadi mwaka 2020, nazo nchi zinazoendelea pia zitahimizwa kutaja hatua zitakazochukuwa kukabiliana na tatizo la kuigizwa moshi hewani. Ijumaa iliopita, Brazili ilikuwa ni nchi ya kwanza kubwa inayoendelea ambayo ilitoa ahadi kama hiyo isio ya lazima, ikisema itajitolea yenyewe kupunguza moshi wake unaoingia hewani kwa baina ya asilimia 36 hadi 39, ifikapo mwaka 2030

Mkataba huo mpya utakuwa na mfuko wa kuzisaidia nchi maskini zibadilike na kuwa na uchumi wa viwanda venye kutoa moshi mdogo hewani na pia ziweze kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Naye katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon aliuwambia mkutano wa kilele wa chakula mjini Roma kwamba mapatano juu ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani ni muhimu sana katika kupambana na njaa duniani, kwa vile mabadiliko ya hali ya hewa yanaharibu uzalishaji wa vyakula mashambani katika nchi maskini.

Wakuu wa serekali na nchi 40 wamedokeza nia yao ya kuhudhuria mkutano wa Copenhagen juu hasli ya hewa, akiwemo kansela Angela Merkel wa Ujerumani.

Mwandishi.Othman Miraji/AFP

Mhariri:M.Abdul-Rahman