1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO na Urusi zinahitajiana

11 Julai 2016

Mkutano wa kilele wa jumuia ya NATO,hali nchini Marekani miaka minane baada ya kuingia madarakani rais Barack Obama na kumalizika fainali za kombe la mataifa barani Ulaya Euro 2016 ni miongoni mwa mada magazetini

https://p.dw.com/p/1JMtt
Rais Obama akihutubia mkutano wa kilele wa NATO mjini Warsaw,POlandPicha: Getty Images/AFP/M. Ngan

Tuanze lakini na mkutano wa kilele wa jumuia ya kujihami ya NATO mjini Warsaw nchini Poland. Gazeti la "Nordbayerischer Kurier" linazungumzia maazimio yaliyopitishwa na kuandika:"Maazimio yaliyopitishwa katika mkutano wa kilele wa jumuia ya kujihami ya NATO yanampekecha mtu matumbo. Jumuia ya NATO inataka kutuma wanajeshi katika eneo la Baltik na pia nchini Poland. Nini kitatokea ikiwa Putin ataendelea na uchokozi wake au pengine kuupalilia? Ndo kusema nchi za magharibi zitazidisha kwa upande wake shinikizo katika eneo la Baltik na Poland? Kitakachofuata hapo ni janga lisilokadirika."

Gazeti la "Der neue Tag" linahisi pande hizi mbili,NATO na Urusi, kila mmoja anamhitaji mwenzake. Gazeti hilo linaendelea kuandika: "Nchi za Magharibi zinaihitaji Urusi,kama nchi inayozipatia mali ghafi mfano wa mafuta, gesi au mbao na pia kama mshirika katika mapambano magumu na pengine ya muda mrefu dhidi ya magaidi wa itikadi kali. Lakini na Urusi pia inazihitaji nchi za magharibi kama nchi zinazoipatia teknolojia au wanunuzi wa kuaminika wa mali ghafi na pia kama washirika katika mapambano dhidi ya ugaidi. Kwasababu wafuasi wa itikadi kali hawatishwi na Urusi. Ndio maana vitisho na maneno makali havimsaidii yeyote.

Obama hajalifikia Lengo alilojiwekea

Rais wa Marekani Barack Obama amelazimika kufupisha ziara yake barani Ulaya na kurejea nyumbani kufuatia matumizi ya nguvu yanayozidi kuigubika nchi hiyo. Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linachambua hali namna ilivyo nchini Marekani na kuandika: "Miaka minane itakamilika hivi karibuni tangu rais Barack Obama alipoingia madarakani. Lakini majukumu mengine aliyojiwekea hayakutekelezwa. Na hasa mwisho wa mhula wake unapokurubia ndipo nchi hiyo inapozidi kujitokeza kama nchi iliyogawika kupita wakati wowote ule mwengine. Badala ya kupungua mwanya kati ya wazungu na wamarekani weusi,kati ya maskini na matajiri na kati ya wademokrat na warepublikan,hali inaonyesha imezidi kuingia sumu katika maeneo kadhaa ya nchi hiyo. Nafasi ya kupatikana ufumbuzi wa haraka si nzuri na kwa wakati huu wa pirika pirika za uchaguzi mkuu ndio kabisa."

Eti Dimba au Dama

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu dimba.Fainali za kombe la mataifa barani Ulaya Euro 2016 nchini Ufaransa zimeshamalizika,Ureno imetawazwa mabingwa wa Ulaya. Gazeti la "Emder Zeitung" linaandika:"Michuanao ya Euro 2016 imeshamalizika,mshindi ameshavikwa taji. Hata hivyo kimoja tayari kinajulikana : Miaka minne kutoka sasa michuano ya fainali za kombe la mataifa barani Ulaya itafanyika katika nchi 13. Kutokana na uzoefu ulioko,mtu anaweza ,au bora tuseme mtu anabidi kusema ni kichaa. Ndo kusema mashabiki watalazimika kusafiri toka nchi moja hadi nyengine ya Ulaya na kukabiliana na tofauti za masaa zilizoko katika nchi za Ulaya? Shangwe zitakuwa za aina gani wakati huo? Na wanasoka watakuwa na uwezo gani kukabiliana na mabadiliko kama hayo. Ulichotuletea Platini kinavuruga kila kitu.Hili si dimba tena ,limegeuka dama.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga