1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa NATO waanza

Admin.Lilian Mtono8 Julai 2016

Viongozi wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, wameanza mkutano maalumu wa kilele mjini Warsaw ambapo katibu mkuu, Jens Stoltenberg amesema utaleta mabadiliko makubwa ndani ya ushirika huo ili kuhakikisha usalama wa raia wake.

https://p.dw.com/p/1JLzq
NATO Gipfel in Gruppenbild
Picha: Reuters/J. Ernst

Stoltenberg amesema maamuzi yatakayofikiwa na rais wa Marekani Barack Obama na viongozi wengine wa NATO katika mkutano huu yataijenga NATO mpya na itakayodumu kwa muda mrefu.

Ufunguzi huo rasmi ulianza kwa shughuli ya kuwakumbuka askari wa vikosi vya NATO waliopoteza maisha wakiwa katika operesheni za Jumuiya hiyo na washirika wake.

Awali, Jumuiya hiyo ya kujihami pamoja na Umoja wa Ulaya, EU zimetiliana saini makubaliano yaliyoitwa kuwa ni ya kihistoria, yanayolenga kuimarisha ushirikiano katika masuala ya ulinzi dhidi ya changamoto mpya. Makubaliano hayo yamesainiwa leo katika mkutano huo.

Makubaliano hayo yalifikiwa muda mfupi kabla ya mkutano huo kudhihirisha wazi kitisho dhidi ya jumuiya hiyo ya nchi za Magharibi, kutoka Mashariki na Kusini. Makubaliano hayo yamesainiwa na Katibu mkuu wa NATO, Jens Stolteberg na Rais wa baraza la Umoja wa Ulaya, Donald Tusk na rais wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Junker.

Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg na Rais wa baraza la EU, Donald Tusk waliposaini makubaliano
Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg na Rais wa baraza la EU, Donald Tusk waliposaini makubalianoPicha: Reuters/K. Pempel

Stoltenberg amesema, ni makubaliano hayo ya kihistoria, yanayotoa mwelekeo mpya wa kiushirikiano kati ya EU na NATO katika kupambana na uhalifu wa kimtandao na ongezeko la wimbi la biashara haramu ya binaadamu.

Katika kuonyesha utayari wao, tayari Rais Barack Obama amesema Marekani itapeleka vikosi vya wanajeshi 1000 na kuweka makao makuu mapya ya brigade ya vikosi hivyo nchini Poland, wakati ambapo NATO inatanua shughuli zake za kiulinzi katika eneo la Mashariki mwa Ulaya.

Vikosi hivyo vya Marekani ni sehemu ya mpango mkubwa wa NATO, utakaohusisha batalioni tatu za kijeshi, zitakazoongozwa na Canada, Ujerumani na Uingereza, zitakazopelekwa katika mataifa matatu ya Baltiki, ili kuwezesha mataifa hayo ya Mashariki ambayo pia ni washirika wao katika kukabiliana na Urusi.

Rais wa Poland, Andrzej Duda amemshukuru rais Obama kwa kuona umuhimu wa kuimarisha usalama katika eneo la Mashariki mwa Ulaya kwa kuongeza majeshi.

Rais wa Barack Obama akiwa na katibu mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg na Rais wa Poland Andrzej Duda
Rais wa Barack Obama akiwa na katibu mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg na Rais wa Poland Andrzej DudaPicha: Reuters/Agencja Gazeta/S. Kaminski

Hata hivyo katika hatua nyingine, Rais Obama ameelezea wasiwasi wake dhidi ya kile kinachoelezwa kuwa ni marekebisho tata ya mahakama ya juu ya Poland yanayofanywa na serikali yake ya mrengo wa kulia, ambayo wachambuzi wanasema umeendelea kudumaza chombo hicho.

Suala la Uingereza ambaye ni miongoni mwa wanachama muhimu wa NATO kujiengua kutoka umoja wa Ulaya, limechukua nafasi kubwa katika mkutano huo. Hata hivyo Waziri mkuu David Cameron amesema Uingereza itaendelea kutekeleza kikamilifu majukumu yake, hata baada ya kuondoka ndani ya EU.

Urusi kwa upande wake imeishutumu Jumuiya ya kujihami ya NATO kwa kuwa na mtizamo hafifu na dhana tofauti dhidi yake kuhusiana na nchi hiyo kuchukuliwa kama kitisho, ikiwa ni saa chache kabla ya NATO kupitisha uamuzi wa kupeleka vikosi vya majeshi, ya takribani askari 4000, katika mataifa ya Baltiki na Poland. Lakini imesema ipo tayari kwa mazungumzo.

Mwandishi: Lilian Mtono/APE/AFPE/Reuters.

Mhariri: Mohammed Khelef