1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Afrika waanza Kigali

17 Julai 2016

Kuibuka upya kwa mapigano Sudan Kusini kulikogharimu maisha ya watu 300 kumehodhi majadiliano katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Afrika uliofunguliwa katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali

https://p.dw.com/p/1JQTR
Picha: DW/G. Tedla

Usitishaji tete wa mapigano umekuwa ukiendelea kufanya kazi tokea Jumatatu kufuatia mapigano hayo ambayo yalidumu kwa siku nne mjini Juba na kusababisha mamia kupoteza maisha na wengine 40,000 kukimbia makaazi yao.

Ghasia hizo katika mji mkuu wa Sudan Kusini zinakumbushia mapigano yaliyochochea vita vya wenyewe kwa wenyewe na kutowa pigo kwa makubaliano ya mwaka jana kukomesha mzozo huo mbaya ambao ulianza baada ya Rais Salva Kiir kumshutumu muasi wa zamani na hivi sasa makamo wake wa rais kwa kupanga njama ya mapinduzi.


Machafuko hayo pia yameutumbukiza katika mashaka mpango wa amani uliofikiwa hapo mwezi wa Agusti mwaka 2015 kati ya pande hizo mbili.

Kwa pamoja viongozi wa nchi za Umoja wa Afrika wamekemea mauaji ya Sudan Kusini na Burundi. Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Rais wa Chad Iddris Deby amesema bila ya kupoteza muda wanamtaka Rais Salva Kiir na makamu wake Riek Machar kuwahurumia raia wasiokuwa na hatia na kurejesha amani nchini humo.

Wito wa Ban waungwa mkono

Baada ya kukutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa hapo Jumamosi usiku viongozi wa jumuiya ya maendeleo ya kanda IGAD waliunga mkono wito wa Ban wa kutaka Sudan Kusini kuwekewa vikwazo vya silaha, vikwazo kuwalenga watu binafsi na kuimarisha shughuli za kulinda amani nchini humo pamoja na kuwekwa kwa kikosi cha kulinda raia kuyatenganisha makundi hayo yanayohasimiana.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moonPicha: DW/G. Tedla

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini- Zuma ameipongeza IGAD kwa kuchukuwa hatua haraka ya kuitisha mkutano juu ya mzozo wa Sudan Kusini. Akizungumza katika kikao cha ufunguzi wa mkutano huo amesema "hatutopuuza na tutachukuwa hatua kwa kuamini kwamba wakati nguvu ya mapenzi kwa ndugu zetu wa Afrika inaposhinda mapenzi ya madaraka kutakuwa na amani mikononi mwetu"

Sudan Kusini ni mojawapo ya mzozo uliobuka tena hivi karibuni katika bara hilo ambao viongozi wa Afrika wataujadili katika mkutano huo wa kilele.

Umoja wa Afrika pia utatafuta nji za kupata usuluhishi kwa mzozo ulioikumbwa Burundi ambapo mfululizo wa mauaji umekuwa ukiikumba nchi hiyo tokea Rais Piere Nkurunziza kutangaza hapo mwezi wa Aprili mwaka 2015 kwamba angeliwania tena muhula wa tatu.

Viongozi hao wa Afrika wamekemea mauaji ya nchini humo wakisema kwamba sasa inatosha.

Sula jengine lilioko kwenye agenda ni mapambano yanayoendelea dhidi ya kundi la Boko Haram ambalo asili yake ni kaskazini mwa Nigeria lakini limekuwa likifanya mashambulizi katika kanda zima ya Ziwa Chad.

Masuala mengine yanayotarajiwa kujitokeza katika agenda hiyo ni matukio ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Mtu wa kuchukuwa nafasi ya Dlamini Zuma

Hata hivyo juhudi za kufanikisha amani Sudan Kusini na kwengineko yumkini zikakorofishwa kutokana na mgawanyiko uliopo juu ya mtu anayepaswa kuchukuwa nafasi ya Dlamini-Zuma mke wa zamani wa Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini kuwa mwenyekiti mpya wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika.

Mwenyekiti wa Halmshauri ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini-Zuma.
Mwenyekiti wa Halmshauri ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini-Zuma.Picha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Nchi kadhaa barani humo zimedokeza kwamba hazimuungi mkono mgombea yoyote kwa wadhifa huo kutokana na kukosa hadhi ya wadhifa huo.

Inaonekana kwamba wagombea wote watatu wakuu yumkini wakashindwa kupata kura za kutosha kutoka nchi wanachama 54 wa umoja huo.

Mwenyeji wa mkutano huo Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema kutoungana kwa nchi za Afrika kunatoa mwanya kwa wageni walio na maslahi binafsi kuendelea kuwagawa. Viongozi hao wamezindua rasmi pasi ya pamoja ya kusafiria barani Afrika ambapo watu wa kwanza kunufaika watakuwa ni marais, mawaziri wa mambo ya nje na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao makao makuu ya Umoja wa Afrika nchini Ethiopia.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Sylvia Mwehozi