1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika wahamishiwa Addis Ababa

Mohamed Abdulrahman21 Juni 2012
https://p.dw.com/p/15He1

Umoja wa Afrika umeuhamishia mkutano wake wa kilele mwezi Julai katika mji mkuu wa Ethiopia baada ya Malawi kuzuwia kushiriki kwa Rais wa Sudan Omar Hassan al-Bashir, anayetakiwa na  mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC.

Mwezi uliopita, Malawi iliuomba Umoja wa Afrika kumzuwia  rais Bashir asishiriki, ikisema  hilo litaathiri uchumi wake unaotegemea msaada  kutoka nje.

Mwaka jana Malawi iliwakasirisha wafadhili wake wa kimataifa ambao wamekuwa wakifidia 40 asili mia ya bajeti ya nchi hiyo ilipomkaribisha Rais Bashir, wakati wa utawala wa Rais wa zamani, Bingu Wa Mutharika, aliyefariki dunia mwezi Aprili.

Taarifa ya Umoja wa Afrika imesema sasa mkutano huo wa  kilele wa 19 utafanyika kwenye makao makuu ya Umoja huo mjini Addis Ababa. Rais Bashir anatuhumiwa kupanga mauaji na maovu mengine dhidi ya binaadamu katika jimbo la Darfur. 

Mwaka 2009, viongozi wa nchi za Afrika walilikataa ombi la mahakama ya kimataifa kumkamata  kiongozi huyo wa Sudan, wakisema hatua hiyo itahujumu juhudi za kusuluhisha migogoro kadhaa ya ndani ya Sudan. Pia waliilaumu mahakama hiyo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuwaandama waafrika pekee.