1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kimataifa kuhusu Afghanistan wafanyika Bonn

5 Desemba 2011

Ujerumani ni mwenyeji wa mkutano wa kimataifa kuhusu mustakabali wa Afghanistan unaofanyika leo mjini Bonn. Ni miaka kumi tangu mkutano wa kwanza wa kimataifa kuhusu Afghanistan kuanza katika eneo la Bonn la Petersburg.

https://p.dw.com/p/13MjC
Rais wa Afghanistan, Hamid Karzai na mwenyeji wake kansela wa Ujerumani, Angela Merkel
Rais wa Afghanistan, Hamid Karzai na mwenyeji wake kansela wa Ujerumani, Angela MerkelPicha: dapd

Imesalia miaka mitatu kabla Afghanistan kuchukua majukumu kamili ya kusimamia kikamilifu masuala ya usalama na kuendesha masuala yake ya ndani. Hayo ni kwa mujibu wa mpango wa jumuiya ya kimatiafa, na ndivyo serikali ya Afghanistan inavyotumai. Kwenye mkutano wa Bonn mchakato mzima wa kufanikisha azma hiyo utajadaliwa na kukamilishwa, mpango ambao nchi za magharibi umeuita "Kukabidhi Majukumu". Waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Thomas de Maziére, wa chama  cha Christian Democratic, CDU, anasema:

"Tumekubaliana kuhusu mkakati wa kisiasa na kijeshi ambao kufikia mwishoni mwa mwaka 2014 shughuli zote za kijeshi nchini Afghansitan zinatakiwa kukamilishwa. Huo ni ujumbe pia kwa Waafghanistan kwamba baadaye watatakiwa kubeba jukumu la kulinda usalama wa nchi yao."

Maafisa 130,000 wa polisi na wanajeshi 175,00 wa Afghanistan wamepata mafunzo kutoka nchi za kigeni kupitia msaada wa kimataifa. Vikosi vya jumuiya ya kujihami ya NATO tayari vimeanza kuondoka Afghansitan, hasa wanajeshi wa Marekani. Pia jeshi la Ujerumani, Bundeswehr, lenye wanajeshi 5,000 nchini Afghansitan itapunguza maafisa wake mwaka ujao. Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujermani, Guido Westerwelle, anasema:

"Tumekuwa Afghanistan miaka kumi na haiwezekani kuendelea kubakia kwa miaka mingine kumi. Ndio maana ni lengo la serikali ya Ujerumani na lengo langu pia kwamba kufikia mwaka 2014 vikosi vyote vya mapambano viwe vimeondoka Afghanistan."

Wataalamu waonya kuhusu kuondoka Afghanistan

Kwa kipindi kitakachofuata baada ya mwaka 2014 serikali ya Ujerumani inapanga kuwa na wanajeshi Afghnistan watakaokuwa na kibarua cha kutoa mafunzo. Mtaalamu wa jeshi la Ujerumani, Marco Seliger, anauona mpango mzima wa kuondoka Afghansitan ni wa kutilia shaka. Amesema wapinzani wanajua ni wakati gani wanajeshi wa kimataifa watakapoondoka nchini humo kwa hiyo wanasubiri ufike. Wana muda mwingi wa kijiimarisha kabla kufikia wakati huo.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, kulia, na mwenzake wa Afghanistan, Salmai Rasul
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, kulia, na mwenzake wa Afghanistan, Salmai RasulPicha: dapd

Seliger ameonya kwamba polisi ya Afghanistan pamoja na jeshi linaweza kuwa dhaifu bila ushirikiano kutoka kwa vikosi vya kimataifa. Miaka kumi tangu kuangushwa kwa utawala wa Taliban nchini Afghansitan, katika siku za nyuma jumuiya ya kimataifa imekuwa ikiweka matumaini makubwa mno. Waziri wa zamani wa ulinzi wa Ujerumani, Peter Struck, amesema miaka kumi tangu kuanza operesheni nchini Aghnaistan, Ujerumani imepata uzoefu mkubwa. "Tuliamini tungeweza kujenga taasisi za kidemokrasia nchini humo, lakini kwa sasa tunafahamu kwamba bado tuko mbali kulifikia lengo hilo" amesema bwana Struck.

Akiufungua mkutano wa Bonn, waziri wa mambo ya kigeni Guido Westerwelle ameahidi kuwa jumuiya ya kimataifa haitoiacha mkono Afghanistan baada ya majeshi ya jumuiya ya NATO kuondoka mwaka 2014.

Mwandishi: Werkhäuser, Nina/Josephat Charo

Mhariri: Yusuf Saumu