1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya hali ya hewa unaendelea jijini Nairobi, Kenya

14 Novemba 2006

Jamii za wafugaji na wavuvi zinatoa kilio chao jinsi maisha yao yanavyo athirika kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa

https://p.dw.com/p/CHm9
Profesa Wangari Maathai mwanamazingira na mshindi wa Tuzo ya Nobel ya umoja wa mataifa
Profesa Wangari Maathai mwanamazingira na mshindi wa Tuzo ya Nobel ya umoja wa mataifaPicha: AP

Jamii zilizotengwa ambazo pia zinawakilishwa katika mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya hali ya hewa unaofanyika mjini Nairobi nchini Kenya, zimeeleza jinsi hali yao ya maisha inavyozidi kuharibika kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Hatuwezi tena kuwinda wala kuvua kama ilivyokuwa hapo zamani kwa sababu maji katika maziwa na mito yanazidi kupungua kila kukicha na kwingine mito imekauka kabisa hakuna maji hata kidogo. Hivi sasa tumebakia kuwa wakimbizi wa mabadiliko ya hali ya hewa.

Hayo ni maneno yake Anna Pinto mjumbe katika mkutano wa umoja wa mataifa unaojadili juu ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani kutoka India ambae alieleza alipozungumza na waandishi wa habari jijini Nairobi.

Kwa mujibu wa Hussein Abdullahi anetoka kwa jamii ya wafugaji katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Kenya, mabadiliko katika hali ya hewa yemefikia kiwango cha kutotabirika na kusababisha mfumo wa kienyeji wa kuitabiri hali ya anga na misimu mbali mbali kutoweza kutumika kabisa siku hizi.

Hapo kale wafugaji walitegemea sana ujuzi wao wa kienyeji kubashiri msimu fulani anasema mimi kama mfugaji sikutegemea habari kutoka watalaam wa hali ya anga hata siku moja eti wanieleze mvua zitaanza lini.

Kwa kawaida tulitegemea kuwasikia vyura wakilia na hapo tungeweza kutabiri kitakachofuata au hata ndege wakiimba tungeweza kubashiri sauti za ndege hao zilimaanisha kuwa mvua ziko karibu na hapo mara moja tunaanza kutayarisha akiba ya chakula kwa mifugo yetu, lakini yote hayo sasa yamekuwa historia.

Kwa kuwa katika eneo la kaskazini mashariki mwa Kenya kuna matatizo mengi, wenyeji wa maeneo hayo hulazimika kutembea kwa siku kadhaa ili kuweza kupata huduma kama vile ya maji safi na hali hiyo imesababisha mifugo yao kufa kwa kiwango cha asilimia 50, hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya umoja wa mataifa ambayo hali ya hewa eneo hilo limekumbwa na ukame mkubwa katika miaka ya hivi karibuni.

Hussein Abdillahi anasema kwa ajili ya ukame jamii ya wafugaji katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Kenya imelazimika kuitelekeza mifugo yao na kuhamia mijini.

Idadi kubwa ya watu wa eneo hilo wanaishi kwa kutegemea misaada ya chakula na wengine wamefariki dunia kutokana na hali mbaya ya ukame.

Mkutano huo wa kimataifa unao jadili juu ya mabadiliko ya hali ya hewa kwa muda wa wiki mbili umewajumuisha takriban wajumbe 6000 kutoka sehemu zote ulimwenguni.

Nchi masikini ambazo hazina mikakati ya kuziwezesha kukabili mabadiliko ya hali ya hewa zitaathiriwa zaidi na hali hii pamoja na kuwepo kwa hali mbaya ya ukame inayoendelea.

Mabadiliko ya hali ya hewa ndio hasa chanzo cha mafuriko na hali ya juu ya joto inayosababisha wasiwasi mkubwa katika uzalishaji wa chakula na pia kupatikana maji ya kutosha.

Ripoti ya umoja wa mataifa iliyotolewa mwanzoni mwa mkutano huo inaonyesha barani Afrika, zaidi ya watu milioni 136 wameathirika na hata kufa kutokana na majanga yanayohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa katika kipindi cha mwaka 1993 na 2002.

Mkutano wa kimataifa unaofanyika mjini Nairobi, Kenya ni wa kumi na mbili wa aina yake kufanyika miongoni mwa nchi wanachama 189 zilzotia saini azimio la umoja wa mataifa la mwaka 1992 juu ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Hadi sasa ni nchi 165 pekee ndio zilizofungamana na mswaada wa Kyoto unaozitaka nchi kubwa kiviwanda kupunguza utoaji wa gesi zinazochafua mazingira.

Mshindi wa tuzo ya Nobel kutoka Kenya Profesa Wangari Maathai anazihimiza jamii kushirki katika upanzi wa miti ili kuokoa mazingira.

Jamii masikini barani Afrika inatumia miti kama njia moja ya nishati na biashara lakini haipandi miti kama vile inavyoikata.

Bibi Maathai ameanzisha kampeni ya kupanda miti yenye lengo la kupanda miti bilioni moja kufikia mwaka 2007.