1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kimataifa wa uchumi barani Afrika Magazetini

Oumilkheir Hamidou
5 Mei 2017

Kongamano la kimataifa la uchumi barani Afrika mjini Durban , ndoto ya matumaini mema yatoweka Sudan Kusini na Umoja wa ulaya kujenga vituo vya wakimbizi nchini Libya ni miongoni mwa mada za Afrika magazetini wiki hii

https://p.dw.com/p/2cR6k
Südafrika Weltwirtschaftsforum in Durban Wofgang Schäuble
Picha: Reuters/R. Ward

 

Tunaanzia Afrika Kusini ambako kongamano la siku tatu la kimataifa kuhusu haali ya uchumi barani Afrika lilifanyika katika mji wa mwambao wa Afrika Kusini-Durban, lengo likiwa kusaka njia za kuinua uchumi wa bara hilo. Magazeti mengi mashuhuri ya Ujerumani yamemulika kongamano hilo na kuchambua hali ya kiuchujmi namna ilivyo barani Afrika. Gazeti la Frankfurter Allgemeine limezungumzia mada hiyo katika uchambuzi uliopewa kichwa cha maneno" Bara lasaka njia inayofaa", lile la mjini Berlin die Tageszeitung linasema "Mambo kwenda kombo, ni jambo linalowezekana daima", Kölner Stadt Anzeiger linasema uchumi wa Afrika unadorora huku die Zeit likimulika zaidi mpango wa serikali kuu ya Ujerumani wa kuhimiza maendeleo barani Afrika Marshallplan.Tarakimu zinabainisha ukuaji wa kiuchumi wa hadi asili mia nane ulioshuhudiwa kati ya mwaka 2004 na 2014 unasalia kuwa ndoto. Fuko la fedha la kimataifa IMF linaashiria ukuaji finyu wa kiuchumi  wa asili mia moja nukta sita-kiwango ambacho hakilingani na kile cha kuzidi idadi ya wakaazi wa bara hilo kinachofikia asili mia 2.5.

Nchi za magharibi zinabidi ziitumie fursa iliyojitokeza

Stadt Anzeiger linahisi hali hiyo imesababishwa zaidi na ile hali kwamba Afrika iliviwekea matumaini makubwa vitega uchumi vya moja kwa moja kutoka jamhuri ya China. Vitega uchumi hivyo lakini vimepungua kwa karibu asili mia 40 tangu mwaka 2015. Hali hiyo inazifungulia fursa nzuri nchi za magharibi linaandika gazeti hilo la mjini Cologne linalozungumzia mipango inayopangwa kuanzishwa na Ujerumani barani Afrika. Serikali kuu ya Ujerumani imewakilishwa  mjini Durban na waziri wa fedha Wolfgang Schäuble, na waziri wa uchumi bibi Brigitte Zypries huku waziri wa mambo ya nchi za nje Sigmar Gabriel akiwa ziarani nchini Ethiopia kutetea sera ya pamoja ya Umoja wa Ulaya kuelekea Afrika. Juhudi zote hizo lengo lake ni moja tu linaandika gazeti la Stadt Anzeiger linaloashiria kuporomoka uchumi wa Afrika itamaanisha kuzidi kuongezeka idadi ya wakimbizi wanaoelekea Ulaya.

Gazeti laq Taz-die Tageszeitung linamnukuu mkuu wa shirika la misaada ya kiutu la Oxfam, Byanyima akihimiza ibuniwe njia mpya Afrika. Ukosefu wa usawa unaendelea na mamilioni ya waafrika hawakufaidika na ukuaji wa kiuchumi wa miaka ya nyuma anasema bibi Byanyima.

Matumaini ya amani Sudan Kusini yatoweka

"Ndoto imetoweka" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la Berliner Zeitung kuhusu hali namna ilivyo Sudan Kusini. Gazeti linazungumzia matumaini makubwa yaliyochomoza mwaka wa 2000 ulipowadia, baada ya miongo 40 ya vita na ukandamizaji, amani ikaonekana kukurubia Sudan kusini na baadae matumaini ya uhuru. Berliner Zeitung linawataja wengi walivovunjika moyo kuona matumaini waliyokuwa wamejiiwekea yakitoweka na wanaharakati miongoni mwa wale waliokuwa wakipigania mageuzi hayo, kuuliwa mfano wa mwandishi habari Isaac Vuni. Mtindo wa kuwafumba midomo daima wapinzani unafuatwa na pande zote, serikali na upinzani, linaandika gazeti la Berloiner Zeitung.

 Vituo vya kuwapokea wakimbizi kujengwa Libya

Mada yetu ya mwisho katika ukurasa huu wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii inajikita katika suala la wakimbizi. Lilikuwa pia gazeti la mjini Berlin-Taz, die tageszeitung lililoloandika kuhusu mpango wa Umoja wa ulaya wa kuwarejesha  wakimbizi nchini Libya."Wanarejeshwa kule kule kwenye vurugu ndio kichwa cha maneno cha gazeti hilo linalozungumzia azma ya Umoja wa Ulaya kuunda "vituo halali" watakakokusanywa wakimbizi hao. Gazeti hilo linasema mpango huo umejadiliwa katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya ndani na wale wa sheria  wa Umoja wa ulaya uliofanyika hivi karibuni mjini Brussels.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/ARD PresseArchiv

Mhariri: Iddi Ssessanga