1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kitaifa waanza Madagascar

Admin.WagnerD13 Septemba 2010

Mazungumzo ya kuutatua mzozo wa kisiasa Madagascar yaanza hii leo.

https://p.dw.com/p/PB3m
Andry Rajoelina akiwahutubia wananchi katika mji mkuu wa Madagascar - Antananarivo.Picha: AP

Mkutano wa kitaifa  wa wiki moja kuutatua mzozo wa kisiasa nchini Madagascar umefunguliwa  hii leo asubuhi nje ya mji mkuu  Antananarivo huku wawakilishi  wa viongozi wakuu wa kisiasa wakiususia mkutano huo.

Mjadala huo unaotarajiwa kudumu muda wa wiki nzima untarajiwa kugusia masuala ya serikali ya mpito,katiba mpya,maandalizi ya uchaguzi unaokuja pamoja na uwiano wa kitaifa.

Takriban wanachama 4000 wa mashirika ya kijamii na wanasiasa wa vyama mbali mbali wanaotoka miji yote nchini humo walikuwepo katika mkutano huo unaofanyika nje ya mji mkuu wa Antananarivo.

Washirikishi wa viongozi wakuu wa kisiasa,akiwemo rais aliyepinduliwa Marc Ravalomanana,aliyemtangulia Didier Ratsiraka na Albert Zafy, wameususia mkutano huo wakisema kuwa hawataki kuidhinisha jitihada hizi ambazo wanaona hazitafaulu. Habari zinasema hata  kiongozi wa sasa  Andry Rajoelina hakushiriki.

Viongozi hao watatu wa  zamani wanasisitiza juu ya kuandaliwa mazingira muwafaka ya kurejea  kutoka uhamishoni kwa Ravalomanana na Ratsiraka pamoja na kuvunjwa kwa serikali ya sasa ya mpito. Tangu alipoangushwa na Rajoelina kwa msaada wa wanajeshi, Ravalomanana anaishi Afrika kusini na Ratsiraka  anaishi uhamishoni nchini Ufaransa.

Marc Ravalomanana Präsident Madagaskar
Rais aliyepinduliwa madarakani Marc Ravalomanana.Picha: AP

Tarehe 13  mwezi uliopita wa Agosti, vyama  kiasi ya 150 vya kisiasa kisiwani Madaagascar wakiwemo wanasiasa  wanaojitegemea binafsi na waliokaribu na  Bw Ravalomanana, vilisaini mkataba wa kisiasa vikiwa na shabaha ya kujaribu kufungua ukurasa mpya wa maelewano, ili kuutatua mgogoro huo wa kisiasa. Mkataba huo ukatoa wito wa kuitishwa mkutano wa kitaifa, kuzungumzia mustakbali wa kisiasa wa taifa hilo.

Madagascar Imetumbukia  katika mgogoro mkubwa wa kisiasa tangu mwishoni mwa 2008 na hali ikazidi kuwa mbaya baada ya kuangushwa Ravalomanana  tarehe 17 Machi 2009,mapinduzi ambayo hayakutambuliwa na jamii ya kimataifa.

Bado inasubiriwa kura ya maoni mwezi Novemba kama ilivyosisitizwa katika makubaliano yaliofikiwa, na kura hiyo  kufuatiwa na  uchaguzi wa bunge Machi mwaka ujao na ule wa rais mwezi wa Mei.

Hata hivyo bado kuna  utata juu ya ratiba hiyo,kutokana na vikwazo vinavyomkabili rais wa zamani Ravalomanana, baada ya kuhukumiwa hivi karibuni, kwa makosa ya ubadhirifu wa mali ya umma na mauaji yaliofanywa na walinzi wake, wakati wa maandamano ya wapinzani, yaliokuwa chanzo cha vuguvugu  la kumuondoa madarakani.Wapi inaelekea Madagasacar ni suala litakaloweza kujibiwa zaidi  na matokeo ya mkutano huo wa kitaifa .

Mwandishi:Maryam Abdulla/AFP

Mpitiaji:Mohammed Abdul-Rahman