1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kuhamasisha Urasilmalishaji mali za maskini wafanyika Dar es salaam.

Christopher Buke4 Desemba 2006

Wahudhuriwa na Bi Madeleine Albright

https://p.dw.com/p/CHm0

Mkutano wa kimataifa wenye lengo la kuwawezesha maskini kisheria kwa kurasilmalisha rasilmali zao ulifanyika hivi majuzi Dar es salaam nchini Tanzania na ukionyesha mafanikio.

Mkutano huo ambao ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka mataifa mbalimbali, mabalozi wa nchi mbalimbali Tanzania, uliendeshwa chini ya uenyekiti wa Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani, Bi Madeleine Albright ambaye kwa sasa lakini ni mwenyekiti mwenza wa Tume ya Kimataifa ya kuwajengea uwezo Masikini.

Akizungumza mbele za wajumbe wa mkutano huo Bibi Albright aliainisha lengo kubwa la tume yake kuwa ni kupambana na ufukara uliokithiri.

Anasema “ Tunatafuta suluhisho la kitaifa na kimataifa, maendeleo duni ni tatizo linaloziathiri kila bara. Kila mmoja katika chumba hiki anafahamu changamoto zilizopo kwa hiyo sitakaa au kusalia katika kutoa takwimu” alisema Bi Albright huku akiwaasa wajumbe wa mkutano huo umuhimu wa kuinua hali za maisha za watu wa kawaida.

Anasema hata nyumba hujengwa kwa kuanzia chini, na haijengwi kwa kuanzia kuezeka asilani.

Mpango huu kwa hakika unafanana sana na ule uliotambulishwa nchini Tanzania na rais wa awamu ya tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Benjamin William Mkapa uliojulikana kama Mpango wa Kitaifa wa Kurasilmalisha Rasilmali na Biashara za wanyonge Tanzania, kwa ufupi MKURABITA.

Lakini pia Benjamin Mkapa mwenyewe anashiriki katika tume hii ya kimataifa. Alihudhuria mkutano wa Dar es salaam na aliwaambia washiriki wa semina hiyo kuwa.

“ Katika sehemu mbalimbali ulimwenguni, suala la ajira mpya, iwe ni ajira binafsi au kazi ya kulipwa mshahara ndizo zapatikana kwa urahisi katika sekta binafsi. Tuliliona hili kama la muhimu la kiutawala. Na kwa hiyo tukafikia wazo la jumla kuwa upungufu wa haki, na unapelekea watu kuwa wahanga na bila ya usawa na hii inaonyesha kanuni duni za utawala husika”.

Rais wa sasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete ndiye alifungua mkutano huo huku akiwashawishi mashirika, taasisi na wananchi kwa ujumla kuiunga mkono serikali yake katika kuhakikisha inaboresha maisha ya watu wa chini.

Suala la umaskini na ufukara hasa linazigubika nchi nyingi za kiafrika licha ya kuwa nchi hizo zina rasilmali za kutosha. Wengi wa wananchi wanaishi kwa kipato cha chini ya dola moja kwa siku.

Hali hii ya ufukara uliopinudikia ulitajwa na Bi Albright kama gereza lililowakamata wengi.

“ Umaskini uliokithiri ni gereza. Gereza ambalo wengi wamenaswa, gereza lillilo na msongamano na lisilokuwa na haki” alisisitiza Waziri wa mambo ya nje wa Marekani wa zamani.

Lakini licha ya hivyo Bi Albright aliisifia Tanzania kuwa inafanya vizuri kiuchumi huku akihamasisha kuwa juhudi hizo lazima ziendelezwe.

Hivi sasa uchumi wa Tanzania unakua kwa hadi asilimia 7 katika wakati ambapo uongozi wa serikali ya awamu ya nne ukiahidi kuongeza kasi hiyo.

Lakini wakati ikijadiliwa namna ya kuwarasilmalisha wananchi wa maisha duni, majuma kadha wa kadha yaliyopita Wafanya biashara ndogo ndogo wakijulikana kwa jina la machinga kwenye mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania Dar es salaam walishudia maburudoza yakibomoa vibanda vyao vya biashara na baadhi mali zao zikiteketezwa ndani ya vibanda hivyo na hivyo kurudi nyuma kimaendeleo.

Serikali kwa upande wake ilidai hatua hiyo ililenga kusafisha jiji lakini pia kuwaweka wafanya biashara hao kwenye nafasi nzuri kwa lengo la kuwapatia elimu nzuri ya biashara na maeneo yanayokubalika.

Tume hii ya Kimataifa inayoongozwa na bi Albright inalengo hasa la kukusanya maoni kutoka nchi mbalimbali ulimwenguni hasa zile zenye hali mbaya kiuchumi.

Tayari tume hii imekusanya maoni katika nchi za Brazil, Ukraine, na Indonesia na inategemea kufanya vivyo hivyo katika nchi za Kenya, Uganda Ethiopia Sri Lanka, Bangladesh, Mexico na Guatemala.

Hii ni mara ya tatu kwa Bi Albright kuja Tanzania.

Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1998 baada ya kulipuliwa Ubalozi wa Marekani Tanzania na Kenya, na mwaka 1999 wakati wa mazishi Mwasisi wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mwisho.