1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kundi la mataifa 20 wafanyika Bonn

Admin.WagnerD17 Februari 2017

Mawaziri wa mambo ya nje kutoka kundi la mataifa 20 duniani wamekuwa wikikutana katika mji mkuu wa zamani wa Ujerumani Bonn kujadili mizozo ilioko hivi sasa duniani na njia za kuzuwiya mizozo ya baadae

https://p.dw.com/p/2Xkoz
Deutschland G 20 Außenministertreffen in Bonn
Picha: DW/A. Freund

Mawaziri wa mambo ya nje kutoka katika mataifa 20 duniani yenye maendeleo makubwa ya kiuchumi na yale yanaoinukia wamekuwa wikikutana katika mji mkuu wa zamani wa Ujerumani Bonn tokea hapo jana kujadili mizozo ilioko hivi sasa duniani na njia za kuzuwiya mizozo ya baadae wakati huku kukiwa na hali ya mashaka miongoni mwa washirika na mahasimu juu ya mwelekeo wa sera ya kigeni ya Marekani.

Mwanadiplomasia mkuu wa Ujerumani ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo wa siku mbili mjini Bonn amedokeza kwamba kuchaguliwa kwa Rais Donald Trump kunapaswa kuwa wito wa kuizinduwa Ulaya iwapo bara hilo linataka kujiandaa kukabiliana na changamoto zinazokuja.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel ameliambia gazeti la Ujerumani la Frankfurter Allgemeine kwamba Umoja wa Ulaya unahitaji mageuzi iwapo inataka izingatiwe kwa umakini na mataifa yenye nguvu duniani kama vile Marekani,Urusi na China.

Gabriel amesema na " Kwa miaka mingi tumekuwa tukiamini kwamba maisha yetu yangelindwa vizuri zaidi na Wamarekani".Gabriel alikuwa akikusudia udhibiti wa serikali ya Marekani kwa mataifa ya magharibi kitamaduni, kidiplomasia na kijeshi baada ya kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Kutetea maadili

Deutschland G 20 Außenministertreffen in Bonn
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel.Picha: DW/A. Freund

Gabriel amedokeza kwamba wakati umefika kwa wananchi wa Ulaya kuachana na dhana ya kanda yao kuwa ya raha na kusimama kidete kutetea maadili yao ikibidi hata kwa nguvu za kijeshi bila ya kutegemea msaada wa Marekani.Amesema kufanya hivyo kutasaidia kushughulikia mashaka yanayozidi kuongezeka juu ya Umoja wa Ulaya kulikopelekea kufufuka kwa siasa za sera kali za mrengo wa kulia katika miaka ya hivi karibuni.

Mazungumzo rasmi miongoni mwa nchi hizo za kundi la mataifa 20 yenye maendeleo ya viwanda na zile zinazoinukia kiuchumi yanalenga kile kinachojulikana kama malengo ya maendeleo endelevu 17 ambayo jumuiya ya kimataifa iliyakubali yatimizwe kufikia mwaka 2030.

Suala la vita vya Syria vilivyodumu miaka sita linatazamiwa kuhodhi jukwaa Ijumaa (17.02.2017) na baadae mada ya namna ya kulisaidia bara la Afrika kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazokwamisha maendeleo yake itapewa kipaumbele.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/AFP

Mhariri : Gakuba Daniel