1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kundi la mataifa ya G4 wavunjika.

Sekione Kitojo22 Juni 2007

Mataifa makuu manne yenye nguvu za kibiashara yanayofanya kile kinachojulikana kama G4, Brazil, umoja wa Ulaya , India na Marekani yameurejesha tena mpira upande wa shirika la biashara la dunia WTO wakati yalipotangaza jana Alhamis mjini Potsdam nchini Ujerumani kuwa majadiliano yaliyokuwa na lengo la kupatikana kwa makubaliano ambayo yangefufua duru ya majadiliano ya kimataifa ya biashara ya Doha yamevunjika.

https://p.dw.com/p/CHCO

Mkurugenzi mkuu wa WTO Pascal Lamy, ambapo kama idadi kubwa ya mataifa yanayoendelea hakuwa akipendelea sana majadiliano sambamba ya kundi hili la G4, haraka alichukua hatua ya kuitisha kikao kisicho rasmi leo Ijumaa cha kamati ya majadiliano ya kibiashara, kamati ambayo inahusika na uongozaji wa majadiliano ya Doha, iliyozinduliwa mwaka 2001 katika mji mkuu wa Qatar , Doha.

Lakini wakati wajumbe wa kundi la G4 walikuwa wakilaumiana wao kwa wao kwa kushindwa kwa mkutano ambao ungechukua siku nne lakini ukamalizika baada ya siku chini ya tatu, mataifa mengi yanayoendelea , yakiwa na hofu juu ya usiri unaozunguka majadiliano hayo, wamepaza sauti zao mjini Geneva kwa kulalamika kuwa malalamiko yao makubwa yamepuuzwa.

Hatua za majadiliano za hivi karibuni za WTO hazijakuwa za uwazi na ushiriki, yamelalamika mataifa ya kundi la Afrika , Caribik na Pacifik, ACP, kundi la mataifa ya Afrika na mataifa masikini zaidi duniani LDC, ambayo kwa pamoja yanafanya kundi la mataifa 90 linalojulikana kama kundi la mataifa yanayoendelea la G90, ambalo limejitokeza wakati wa mkutano wa tano wa ngazi ya mawaziri wa WTO uliofanyika mjini Cancun , Mexico mwaka 2003.

Taarifa iliyotolewa na kundi hilo la mataifa ya G90 inadai kuwa pamoja na kwamba mataifa mawili ya wanachama wa kundi hilo la G4, Brazil na India ni nchi zinazoendelea, mataifa hayo hayawezi kutarajiwa kubeba dhamana ya kuwakilisha mawazo ya mataifa yote yanayoendelea.

Kundi hilo la G90 kwa hivyo lilijiweka mbali kutoka uwakilishi wa Brazil na India muda mfupi baada ya kushindwa kwa mkutano huo wa Potsdam kulipojulikana hadharani, licha ya kuwa katika muda wa wiki chache zilizopita, vyombo vya habari vinavyotoa habari za biashara viliripoti maelezo muhimu juu ya jukumu la mataifa hayo mawili katika kundi hilo la G4.

Mazungumzo hayo yamekwazwa na tofauti baina ya mataifa tajiri na masikini katika suala la kuvunjwa kwa mfumo wa utoaji wa ruzuku za kilimo kwa mataifa yenye viwanda ya kaskazini na kutumiwa kwa masoko ya nchi zinazoendelea kwa bidhaa ambazo hazitokani na kilimo, ili mataifa yanayoendelea yaweze kulinda haki yao ya kuhami viwanda vyao.

Aileen Kwa , wa taasisi ya Focus on Global South yenye makao yake makuu nchini Thailand, ameliambia shirika la habari la IPS, kuwa nafikiri hali ya baadaye ya WTO iko mashakani. Jinsi shirika hili limekuwa likifanya kazi zake hadi sasa halifanyi hivyo tena.