1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa mabadiliko ya Tabianchi waanza Bonn

Bruce Amani
9 Mei 2017

Wajumbe wa mazungumzo ya mabadiliko ya Tabianchi wamerejea mjini Bonn; Ujerumani chini ya wingu la vitisho vya Donald Trump kuiondoa Marekani katika Makubaliano ya Paris yaliyopiganiwa kwa nguvu

https://p.dw.com/p/2ce2H
Bonn UN Klimakonferenz
Picha: picture-alliance/dpa/M. Hitij

Baada ya miezi ya kutokuwa na uhakika, Rais wa Marekani alionekana kuukaribia uamuzi kuhusu kama ananuia kuitimiza ahadi ya kampeni ya kuiondoa Marekani kutoka kwa mkataba huo wa kuokoa hali ya hewa, ambao utekelezaji wake unajadiliwa katika mazungumzo ya Umoja wa Mataifa mjini Bonn. Trump na wasaidizi wake wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi na kiuchumi wanaanza mazungumzo leo nchini Marekani. Jumla ya nchi 196 sasa zimesaini mkataba huo wa tabianchi, uliofikiwa 2015 baada ya miaka ya mazungumzo makali na mabishano, na Trump akatishia kuubatilisha.

Mkutano wa Bonn ulioanza leo tarehe 8 na utamalizika tarehe 18 mwezi huu, ni wa kuanza kuandika muongozo kwa nchi wanachama kuutekeleza mkataba huo, ambao unalenga kudhibiti ongezeko la joto duniani kwa kupunguza uzalishaji wa gesi chafu inayotokana na nishati ya mafuta. David Burns ni Meneja wa Misitu ya Kitropiki/Kiasili na Kilimo katika Shirikisho la Kitaifa la Wanyamapori nchini Marekani "Kwa sasa tunapaswa kuunda mkakati wa namna serikali zitakavyowajibikia uzalishaji wao wa gesi chafu na mkakati wa pili wa uwazi wa namna mashirika ya kiraia kote duniani yanavyofahamu kama ahadi hizi zinatekelezwa au la.

Bonn UN Klimakonferenz
Wajumbe wanajadili mkakati wa utekelezaji wa mktaba wa TabianchiPicha: picture-alliance/dpa/M. Hitij

Lakini mazungumzo hayo yanakabiliwa na kitisho kutokana na wasiwasi kuwa taifa hilo pili kwa ukubwa duniani linalozalisha gesi chafu litajiondoa na kuuweka mkataba huo katika matatizo. Lakini Burns amejaribu kuondoa hofu "Sidhani kuna mitazamo hafifu, mataifa mengine ya dunia kuanzia Ufaransa yaliweka wazi kuwa tuko pamoja katika hili na tutaepusha madhara makubwa kwa hiyo kama Marekani inajiondoa au la, majimbo na miji imejitolea kusonga mbele hata bila ya serikali kuu.

Marekani imeutuma ujumbe katika mazungumzo hayo, ukiongozwa na mjumbe Trigg Talley aliyehudumu katika enzi ya Obama. Wazungumzaji katika kikao cha mjadala hapo jana walisisitiza kuwa makubaliano hayawezi "kujadiliwa upya” – ikiwa ni pendekezo la Waziri wa Nishati katika serikali ya Trump Rick Perry.

Baada ya kusifiwa kote kama nafasi ya mwisho ya kuepusha madhara makubwa ya ongezeko la joto duniani, Makubaliano ya Paris yalikosolewa na Trump wakati wa kampeni, aliyeyaita mabadiliko ya tabianchi kuwa ni "utapeli” unaofanywa na China. Trump anasema atafanya uamuzi wake kabla ya mkutano ujao wa G7 mnamo Mei 27 hadi 28 mjini Sicily, Italia.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Josephat Charo