1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUmoja wa Falme za Kiarabu

Mkutano wa mabadiliko ya tabianchi wamalizika Abu Dhabi

Amina Mjahid
5 Novemba 2023

Majadiliano yenye utata yamefanyika kwenye mkutano wa mwisho kabla ya Mkutano wa kilele wa marais na viongozi wa serikali kuhusu mabadiliko ya tabianchi COP 28.

https://p.dw.com/p/4YQJO
Mkutano huo uliomalizika jana Jumamosi mjini Abu Dhabi ulijadili kuhusu hazina ya hasara na uharibifu unaohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa
Mkutano huo uliomalizika jana Jumamosi mjini Abu Dhabi ulijadili kuhusu hazina ya hasara na uharibifu unaohusiana na mabadiliko ya hali ya hewaPicha: Amr Alfiky/REUTERS

Majadiliano yenye utata yamefanyika kwenye mkutano wa mwisho kabla ya Mkutano wa kilele wa marais na viongozi wa serikali kuhusu mabadiliko ya tabianchi COP 28. Mkutano huo uliomalizika jana Jumamosi mjini Abu Dhabi ulijadili kuhusu hazina ya hasara na uharibifu unaohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa nchi masikini zilizoathirika sana na ongezeko la joto duniani.

Aidha, washirika wamekubaliana kuwa Benki ya Dunia iwe mwenyeji wa mfuko huo wa kusaidia nchi masikini kwa muda wa miaka minne ijayo.

Marekani na nchi kadhaa zinazoendelea zilieleza kutoridhishwa na rasimu ya makubaliano hayo, ambayo itawasilishwa kwa viongozi katika mkutano wa hali ya hewa wa COP28, ambao utafanyika mjini Dubai mnamo Desemba.

Mahitaji ya kuanzishwa kwa mfuko wa kusaidia nchi maskini yalioathiriwa sana na mabadiliko ya tabianchi yamekuwa lengo la mazungumzo ya hali ya hewa ya Umoja wa Mataifa tangu miaka 30 iliyopita na hatimaye kuanzishwa rasmi kwenye mkutano wa COP27 nchini Misri.