1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa mawaziri wa fedha wa zoni ya Euro mjini Brussels

16 Mei 2011

Mawaziri wa fedha wa zoni ya Euro wataunga mkono msaada wa fedha kwa Ureno,wakati wa mkutano wao wa leo unaogubikwa na kisa cha kukamatwa mkuu wa shirika la IMF,Dominique Strauss-Kahn .

https://p.dw.com/p/11HJq
Sarafu ya EuroPicha: picture-alliance/dpa

Dominique Strauss-Kahn alikuwa ashiriki mkutanoni wakati mawaziri wa fedha wa nchi 17 za zoni ya Euro watakapotia saini msaada wa dharura wa Euro bilioni 78 kwaajili ya Ureno.Lakini nafasi yake inashikiliwa na naibu mkurugenzi mkuu anaeshughulikia masuala ya Ulaya,Nemat Shafik.

Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya iliyojadili utaratibu wa kupatiwa msaada Ureno,na kabla ya hapo Ugiriki na Ireland,kwa ushirikiano pamoja na shirika la fedha la kimataifa IMF,imezisuta hoja kwamba kukamatwa Strauss-Kahn kunaweza kuwa na madhara ya aina yoyote yale kwa mipango ya kuisaidia Ureno.

"Nnapendelea kuwahakikishia walimwengu,masoko ya hisa na vyombo vya habari,maamuzi yaliyopangwa hayataathirika na mikakati inayopangwa kuanzishwa pia haitaathirika" amesema hayo msemaji wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya mbele ya waandishi habari hii leo mjini Brussels.

Verhaftung Strauss-Kahn
Dominique Strauss-Kahn akiongozana na polisi mjini New YorkPicha: dapd

Maoni kama hayo yametolewa apia na waziri wa fedha wa serikali kuu ya Ujerumani Wolfgang Schäuble aliyesema alipohojiwa na vituo vya televisheni vya ARD na ZDF:

Majibu,na maelezo yote tunayoyahitaji kutoka kwa shirika la fedha la kimataifa,tutayapata.IMF ni taasisi kubwa yenye uwezo wa kupitisha maamuzi na kuendeleza kazi zake."

Amadeu Altafaj ambae ni msemaji wa kamishna anaeshughulikia masuala ya kiuchumi Olli Rehn amesema pia kwamba anaamini kisa cha kukamatwa Dominique Strauss-Kahn hakitokorofisha mikakati inayoendelea kwaajili ya Ugiriki na Ireland au maamuzi yanayaopangwa kupitishwa hii leo kuhusu Ureno."

Brüssel Eurogruppe Portugal
Waziri wa fedha wa Ureno Fernando Teixeira dos Santos, kushoto akizungumza na kamishna wa masuala ya uchumi Olli Rehn mjini BrusselsPicha: AP

Mawaziri wa fedha wa zoni ya Euro wanatazamiwa kuzungumzia kuhusu misaada ziada kwa Ugiriki iliyopatiwa mkopo wa Euro bilioni 110 mwaka jana .

Shirika la fedha la kimataifa limechangia kwa takriban thuluthi moja katika misaada yote iliyokubaliwa hadi sasa Euro bilioni 110 kwaajili ya Ugiriki,Euro bilioni 85 kwaajili ya Ireland na msaada utakaotiwa saini leo hii mjini Brussels wa Euro bilioni 78 kwaajili ya Ureno.Na Dominique Strauss-Kahn amechangia pakubwa katika kufikiwa makubaliano hayo.

Mawaziri wa fedha wa zoni ya Euro watazungumzia pia kuhusu fuko la Euro bilioni 500 litakalodhamini utulivu wa sarafu ya Euro-mkakati utakaoanza kutumika mwaka 2013.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/afp/reuters,dpa

Mhariri:Abdul-Rahman