1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa mazingira kuanza mjini New York

23 Septemba 2014

Mkusanyiko mkubwa kabisa wa viongozi wa dunia katika mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi unafunguliwa leo(23.09.) huku kukiwa na miito kuchukua hatua kuiweka sayari hii katika njia kuelekea kuzuwia ongezeko la ujoto.

https://p.dw.com/p/1DHO5
Proteste in Indien vor dem UN-Klimagipfel am 23.09.2014
Wanaharakati vijana wakitoa kauli mbiu yao , "Hatua na sio maneno".Picha: AFP/Getty Images

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon anaongoza mkutano huo uliowaleta pamoja viongozi 120 , ukiwa ni mkusanyiko mkubwa wa viongozi wa ngazi ya juu tangu mkutano uliofanyika mjini Copenhagen kuhusu mabadiliko ya tabia nchi uliomalizika bila kupatikana muafaka mwaka 2009.

Wanadiplomasia na wanaharakati wa mazingira wanaliona tukio hilo kuwa ni muhimu katika kujenga msukumo kabla ya mkutano utakaofanyika mjini Paris baadaye mwaka 2015 ambao utaangalia upatikanaji wa makubaliano ya kupunguza gesi zinazoharibu mazingira baada ya mwaka 2020.

Greenpeace UN Ban-Ki Moon
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na wanaharakati wa mabadiliko ya tabia nchiPicha: Michael Nagle /Greenpeace

Lakini viongozi wa China hawahudhurii mkutano huo , nchi ambayo ni mtoaji mkubwa wa gesi hizo zinazoharibu mazingira , pamoja na India , nchi iliyoko katika nafasi ya tatu ya kwa uchafuzi wa mazingira, na hii inaweka kiwingu cha shaka kuhusu mafanikio ya mkutano huo.

Hakuna muda wa kupoteza

Mabadiliko ya tabia nchi ni suala muhimu kwa wakati huu, amesema katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.

"Najisikia hamasa kubwa kutokana na nguvu na hamasa za sauti za watu. Ni matumaini yangu sauti hizi zitafika kwa viongozi wakati watakapokutana Septemba 23. Mabadiliko ya tabia nchi ni suala muhimu katika wakati huu. Na hakuna muda wa kupoteza."

Ban Ki-moon atazindua mkutano huo akiwa pamoja na makamu wa rais wa zamani wa Marekani na mwanaharakati wa mazingira Al-Gore, mcheza sinema maarufu Leonardo DiCaprio, mcheza sinema kutoka China Li Bingbing na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Rajendra Pachauri , mkuu wa jopo la mazingira la Umoja wa Mataifa.

Leo DiCaprio New York Protest 21.09.2014
Mcheza sinema maarufu DiCaprio akiwa katika maandamano mjini New YorkPicha: Reuters/Eduardo Munoz

Viongozi baadaye watazungumza mmoja baada ya mwingine, kuanzia rais Barack Obama wa marekani akiwakilisha nchi ya pili duniani kwa utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira hadi waziri mkuu Enele Sopoaga wa taifa la visiwa vya Tuvalu, ambalo linakabiliwa na uwezekano wa kufutika duniani kutokana na kupanda kwa kiwango cha maji ya bahari.

Wanaharakati hawana matumaini hata hivyo

Licha ya hamasa kubwa kutoka kwa wanaharakati wa mazingira kwa uwezo wa mkutano huo kuwa ni kichocheo , baadhi wanauona kuwa unamapungufu ya kile kinachohitajika kuchukua hatua za dhati juu ya mazingira.

Friedensnobelpreisträger Galerie
Mwanaharakati makamu wa rais wa zamani wa Marekani Al-GorePicha: AP

Mamia ya waandamanaji walizuwia njia karibu na soko la hisa , katika hatua iliyopewa jina la Wall Street imefurika.

"Madaraka yako mikononi mwa watu hawa wakati watakapo rejea katika mataifa yao na miji na makabila na kuanza kufanya kazi inayokusudiwa. Watakwenda pamoja na Umoja wa Mataifa."

New York Demonstration Flood Wall Street 22.9.2014
Maandamano dhidi ya soko la hisa la Wall Street mjini New YorkPicha: picture-alliance/dpa/Justin Lane

Hatua hiyo imekuja karibu na siku ya kimataifa siku ya Jumapili ya kuchukua hatua na imewaleta pamoja watu wanaokadiriwa kufikia 310,000 katika mitaa ya mjini New York katika kile wanaharakati wanachosema ni maandamano makubwa kabisa kuwahi kufanyika kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre / afpe

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman