1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa mfuko wa kupambana na maradhi ya ukimwi, kifua kikuu na malaria

Jane Nyingi26 Septemba 2007

Wafadhili wanaosimamia mfuko wa kupambana na maradhi ya ukimwi, kifua kikuu na malaria wameanza mkutano wa kuchangisha fedha zitakazosadia katika vita hivyo.Mkutano huo unaofanyika Berlin Ujerumani unanuia kuchangisha dolla billioni 8 katika kupambana na magonjwa hayo matatu sugu.

https://p.dw.com/p/CH7e

Mwenyeji wa mkutano huo wa siku tatu,ujerumani iliuanzisha kwa kuahidi kutoa euro millioni 600 katika mfuko huo katika muda wa miaka mitatu ijayo. Waziri wa maendeleo na nchi za nje Heidemarie Wieczorek-Zeul alitangaza pia kuwa ujerumani itaisamehe Indoneshia deni inaloidai la euro millioni 50 kwa masharti kuwa Jarkata itatoa fedha kugharamia mipango ya mfuko huo.

Waziri huyo amesema hatua hiyo itaipa nafasi Indonesia kutumia euro millioni 25 zinazohitajika kwa dharura kupambana na maradhi ya ukimwi, kifua kikuu na malaria. Waziri Zeul aliyataka mataifa mengine tajiri kuyasadia mataifa maskini kwa kuchukua mwelekeo sawa na huo wa Ujerumani.Hii ni mara ya kwanza kwa ujerumani kusamehe deni ili taifa husika kutumia fedha hizo moja kwa moja katika huduma zake za afya.

Katika muda wa kuelekea kuanza kwa mkutano huo, shirika la umoja mataifa la kupambana na ugonjwa wa ukimwi lilikuwa limetishia ukosefu wa raslimali, na hata mwanamuziki mashuhuri wa mwindoko ya rock Bono kuyataka mataifa tajiri kuongeza kiasi cha fedha yanachotoa katika mfuko wa kupambana na maradhi hayo matatu sugu.

Katika taarifa kupitia kikundi chake kinachotetea maslahi ya bara africa DATA, Rono aliyataka mataifa manane tajiri duniani na hasa ujermani kama rais wa klabu cha mataifa hayo kuongeza kiasi cha fedha ilichoahidi katika mkutano wao wa kilele mwezi juni, wa kutoa dolla billiioni 60 katika muda wa miaka kadhaa ijayo kukabiliana na ugonjwa wa ukimwi.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa mjini Geneva,shirika la umoja wa mataifa la kukabiliana na ugonjwa wa ukimwi lilisema kuwa fedha zinazotolewa kukabiliana na kutibu maradhi ya ukimwi zinapaswa kuongezwa mara nne ya kiasi cha sasa katika muda wa miaka mitatu ijayo na kufikia dolla billioni 42.2 ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.

Mfuko huo ambao hutegemea msaada kutoka mataifa mbalimbali na makampuni makubwa unahitaji kati ya dolla billioni 12-18 ili kugharamia mipango iliyoko sasa na kuanzisha mingine kati ya mwaka 2008 na mwaka 2010.

Siku ya kuamkia mkutano huo uingereza ilitangaza kuwa itatumia pauni billioni moja kupambana na maradhi ya ukimwi,kifua kikuu na malaria kupitia mfuko huo katika muda wa miaka minane ijayo

Mfuko huo wa kimataiafa wa kupambana na maradhi ya ukimwi,kifua kikuu na malaria ulizinduliwa miaka mitano iliyopita kwa msisitizo wa aliyekuwa katibu mkuu wa umoja wa mataifa Koffi Annan na kufikia sasa umetumia kiasi cha dolla billioni 7 kama msaada wa kugharamia mipango 450 katika mataifa 136.

Pia inadaiwa umeokoa maisha ya watu millioni 2 kwa kugharamia dawa kwa wanaougua ukimwi´na kifua kikuu .