1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa NATO na nchi za Ghuba

24 Aprili 2008

NATO yataka kutanua ushirikiano kati yake na nchi za Mediterranian kujumuisha zile za Ghuba za kiarabu.

https://p.dw.com/p/DnsI

Leo unafanyika mkutano wa siku moja huko Bahrein kati ya shirika la ulinzi la magharibi NATO na nchi zilizojiunga na Baraza la ushirikiano la nchi za ghuba-Gulf Cooperation Council (GCC).

Shabaha ya siku zijazo ya NATO ni kutanua ushirikiano wake na nchi zinazopakana na Bahari ya kati (Mediterranian) kujumuisha pia zile za kiarabu ziliopo Ghuba la uajemi.

►◄

Kuimarisha ulinzi na usalama ulimwenguni na mikoani ndio shina la kikao hiki baina ya NATO-shirika la ulinzi la magharibi na wanachama wa baraza la ushirikiano la nchi za ghuba (GCC).

Mbele ya Katibu mkuu wa NATO Jaap de Hoop Scheffer na waziri wa nje wa Bahrein, Shikh Khalid Al-Khalifa ,wajumbe maarufu wa NATO wanakutana na waakilishi wa serikali pamoja na wataalamu kutoka Ghuba kuzungumzia leo maswali ya masilahi ya pamoja na kutafuta uwezekano wa kushirikiana karibu zaidi.

Huu ni mkutano wa kwanza wa aina hii tangu pale miaka 4 nyuma ulipoanzishwa ushirikiano wa Istanbul-ambamo hivi sasa nchi 4 za Baraza la Ushirikiano wa nchi za ghuba (GCC) zimejiunga -nazo ni Kuweit,Bahrein,Umoja wa Falme za kiarabu na Qatar.

Oman na saudi Arabia hadi sasa hazikujiunga na ushirika huu.

Baada ya shirika la NATO kuimarisha usuhuba wake na nchi zinazopakana na bahari ya kati-Mediterranian-,ikalenga kutanua ushirikiano huo kuzijumuisha pia nchi za kiarabu katika Ghuba .Ushirika huu wa kijeshi unazipa nchi zenye hamu ya kujiunga msaada katika kuongoza shughuli zao za usalama na kutarajia nchi hizo kushirikiasna na NATO katika sekta ya ulinzi.

Kwa jicho la hali ya wasi wasi iliopo katika Ghuba, jukumu hili linapata uzito katika kuzingatia maswali ya ushirikiano wa kiulinzi.Hali nchini Irak imeacha athari zake katika Ghuba lakini pia mvutano na jirani Iran na mradi wake wa kinuklia.

Isitoshe, wataliban wa afghanistan wanaungwamkono katika Umoja wa Falme za kiarabu-Emirates- na hata mtandao wa Al Qaeda wa Osma Bin Laden kitambo sasa unahurumiwa Baraarabu nzima.Na unawaandikisha wafuasi wake huko.

Ushirikiano mkubwa na Bahrein na nchi nyengine za Ghuba hauna maana kuwa NATO sasa inajaribu kutia mguu wake katika ghuba.

Katibu mkuu wa NATO Jaap de Hoop Scheffer karibuni hivi alihakikisha kwamba shirika lake lingependa kutuwama katika ushirikiano,kutoa misaada ya mafunzo na ya mipango.Kuhusu Bahrein NATO ina azma ya kufunga mapatano ya kubadilishana habari yatakayozinufaisha pande zote mbili.

Kwa wasi wasi wote uliopo juu ya matatizo yasiopatiwa bado ufumbuzi katika eneo hili, NATO haiwezi wala haikusudii kwenda mbali zaidi ya ushirikiano.Kwani hata katika mgogoro wa wapalestina na Israel ,NATO haina ufumbuzi na halitachangia kuleta ufumbuzi huo,isipokuwa tu imeombwa kufanya hivyo na pande zinazohusika .